1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe yaikaba koo Algeria

Bruce Amani
16 Januari 2017

Siku mbili, mechi mbili za kushangaza katika dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika. Algeria ilikabwa sare ya mabao mawili kwa mwili na Zimbabwe katika mchuano wa Kundi B. Ni licha ya mabao mawili kutoka kwa Mahrez

https://p.dw.com/p/2VrqU
Fußball Qualilfikation African Cup of Nation 2017 Äthiopien - Algerien
Picha: Getty Images/AFP/F. Batiche

Lakini sio tu kuwa Algeria ilitekwa sare, bali pia ilihitaji kombora la mbali kutoka kwa Mahrez katika dakika ya 82 hadi wavuni na kuisaidia Algeria kuanza kampeni yake bila kwa kuepuka kichapo mjini Franceville.

Kombe la AFCON tayari limetoa onyo kwa timu zinazoonekana kuwa ni miamba, baada ya wageni Guinea-Bissau kufunga bao la kusawazisha katika dakika ya 90 katika mchuano wa ufunguzi dhidi ya wenyeji Gabon na kutoka sare ya 1-1 mjini Libreville. Ni mechi ambayo pia mshambuliaji wa Borussia Dortmund Pierre Emerick Aubameyang alifunga goli.

Zimbabwe haijacheza AFCON kwa karibu muongo mmoja, na kabla ya dimba kuanza wachezaji walifanya mgomo kulalamikia mishahara na marupurupu, na kisha kabla ya mechi kuanza, wakacheza na jezi za muda maana sare zao hazikufika mjini Franceville kwa muda ufaao

Fussball Africa Cup 2017 - Gabon vs Guinea-Bissau - Pierre Emerick Aubameyang
Aubameyang aliifungua Gabon Picha: picture alliance/AP Photo/Sunday Alamba

Katika mechi ya pili ya Kundi B, Senegal iliepuka kichapo kwa kuilaza Tunisia 2.0. senegal haijawahi kushinda dimba hilo na ni moja ya timu zinazopigiwa upatu wakiongozwa na mshambuliaji wa Liverpool Sadio Mane ambaye alifunga jana penalti. Senegal wanaongoza kundi B wakati Tunisia inashika mkia.

Katika mchuano wa pili wa Kundi A katika siku ya ufunguzi Jumamosi, washindi mara nne wa AFCON Cameroon walitoka sare ya 1-1 na Burkina Faso. Matayarisho ya Cameroon yaligubikwa na habari za kujiondoa wachezaji muhimu akiwemo beki wa Liverpool Joel Matip na mshambuliaji wa Schalke Eric Choupo-Moting.

Kivumbi kinaendelea kutifuliwa tena leo, ambapo nyota wa Togo Emmanuel Adebayor anarejea katika jukwaa kuu la kandanda kwa mara ya kwanza tangu alipoacha kuichezea Crystal Palace msimu uliopita. Adebayor ambaye hana klabu kwa sasa ni nahodha wa Togo wakati wakipambana na mabingwa watetezi Cote d'Ivoire katika Kundi C.

Fussball Africa Cup 2017 - Gabon vs Guinea-Bissau
Guinea Bissau ikisherehekea baada ya kusawazishaPicha: AFP/Getty Images

Mchuano huo utafwatwa na mtanange kati ya Morocco na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao walimaliza katika nafasi ya tatu katika dimba la mwisho miaka miwili iliyopita.

Makamu bingwa wa miaka miwili iliyopita Ghana wanaanza tena jaribio lao la kunyakua kombe la AFCON wakati watashuka dimbani dhidi ya Uganda mjini Port Gentil hapo kesho katika Kundi D.

The black stars wanatafuta kombe lao la tano la AFCON, lakini la kwanza tangu 1982, Muisrael Avram Grant bado anawanoa makali baada ya kuwaongoza wakati walichapwa kupitia penalty dhidi ya Cote d'Ivoire katika fainali ya 2015 nchini Guinea ya Ikweta.

Katika mchuano wa pili kesho, Misri itajitosa tena uwanjani baada ya kuwa nje kwa miaka kadhaa wakati watakutana na Mali. Misri ndio wanaoshikilia rekodi ya kushinda mataji saba ya AFCON lakini hawajashiriki tangu waliposhinda kwa mara ya tatu mfululizo mwaka wa 2010 nchini Angola kwa kuwazaba Ghana katika fainali.

Misri itaongozwa na Mohammed Salah katika safu ya mashambulizi. Kocha wa Mali Alain Giresse anatumai kusababisha mshangao.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Iddi Ssessanga