1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zimbabwe

Hamidou, Oumilkher28 Oktoba 2008

Mkutano wa dharura wa SADC washindwa kuwatanabahisha mahasimu wawili wa Zimbabwe

https://p.dw.com/p/Fig1
Umaskini umekithiri nchini ZImbabwePicha: Thomas Kruchem



Viongozi wa mataifa ya kusini mwa Afrika wameshindwa jana kuijongeza misimamo ya pande mbili kwa lengo la kuunda serikali ya umoja wa taifa nchini Zimbabwe na kwa namna hiyo kuyanusuru makubaliano ya kugawana madaraka yanayozorota tangu wiki sita zilizopita.


Rais Robert Mugabe na kiongozi wa chama cha upinzani cha MDC,Morgen Tsvangirai,wameondoka baada ya saa 13 za majadiliano pamoja na viongozi mashuhuri wa mataifa wanachama wa jumuia ya maendeleo kusini mwa Afrika,SADC,baada ya kukubaliana paitishwe mkutano wa kilele utakaowahuzsisha viongozi wengi zaidi wa jumuia hiyo..


Baada ya juhudi za mwanzo kushindwa October 20 iliyopita,SADC ilifanikiwa kuwaleta katika meza ya mazungumzo,chama tawala na upande wa upinzani wa Zimbabwe,wakihudhuria pia rais wa Afrika Kusini,Kgalema Motlanthe na wawakilishi wa kundi la pande tatu,akiwemo rais Armando Guebuza wa Msumbiji na mawaziri wawili wa kutoka Swaziland na Angola.


Walitaraji kuwatanabahisha Mugabe na Tsvangirai wakubaliane namna ya kugawana nyadhifa muhimu za mawaziri wa serikali ya umoja wa taifa,kama ilivyotajwa katika makubaliano ya September 15 iliyopita,ili kuikwamua Zimbabwe toka mzozo wa kisiasa uliofuatia kushindwa chama tawala katika uchaguzi mkuu mwishoni mwa mwezi March uliopita.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotangazwa mwishoni mwa mkutano huo, pande hizo mbili bado zinazozana kuhusu suala la nani anastahiki kukabidhiwa wizara ya ndani.


Taarifa hiyo inazitaka pande hizo mbili ziwajibike kwa dhati kusaka ufumbuzi wa kudumu na kuwatolea mwito wakati huo huo viongozi 15 wa mataifa wanachama wa jumuia ya SADC wakutane katika mkutano wa dharura kabla ya hali ya mambo haijazidi kuwa mbaya.


"Umma wa Zimbabwe unakabiliwa na mitihani mikubwa na shida ambazo haziwezi kupatiwa ufumbuzi kabla ya kwanza serikali ya umoja wa taifa kuundwa"-imetajwa katika taarifa hiyo ya SADC.


Mkaazi mmoja wa Zimbabwe anasema:


"Ndio wanasema wanakufa kwa njaa:hakuna chakula,hakuna chochote."


Watu wanane wamejeruhiwa na 50 kukamatwa, mita 300 karibu na jengo mkutano huo ulikokua unafanyika,baada ya polisi kutumia gesi za kutoa machozi kuwatawanya wanafunzi na wanaharakati wa haki za binaadam waliokua wakidai serikali ya umoja wa taifa iundwe haraka.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amezihimiza pande zinazozozana nchini Zimbabwe zifikie haraka makubaliano ili,kama alivyosema "kuiokoa Zimbabwe na matatizo ya kisiasa na kuweza kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayowasumbua wazimbabwe.