1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zoezi la kuhesabu kura Iran limeanza

Sekione Kitojo
20 Mei 2017

Wairan walipiga kura katika uchaguzi wa rais hapo jana,(19.05.2017)uchaguzi ambao ulikuwa na ushindani mkali kati ya mwanasiasa mwenye msimamo wa wastani Hassan Rouhani na mhafidhina mwenye msimamo mkali Ebrahim Raisi.

https://p.dw.com/p/2dHCw
Iran wahlen 2017
Kiongozi mkuu wa Iran Ali Khamenei akipiga kuraPicha: Irna

Zoezi la  kuhesabu  kura  limeanza  nchini  Iran leo Jumamosi  baada  ya  wapiga  kura  kujitokeza  kwa  wingi katika  uchaguzi  ambao  bila  kutarajiwa  umekuwa wenye mvutano  mkubwa  baina  ya  rais  wa  sasa  Hassan Rouhani , ambaye  anataka  kurejesha  mahusiano  ya kawaida  na  mataifa  ya  magharibi, dhidi  ya  jaji  mwenye msimamo  mkali  ambaye  anasema  kwamba  rais  wa sasa tayari  amekwenda  mbali  mno.

Präsidentschaftswahlen Iran
Wapiga kura wakipiga kura zao nchini Iran katika uchaguzi wa Ijumaa Mei 19, 2017Picha: Irna

Zaidi  ya  wapiga  kura  milioni 40 walipiga  kura, imesema wizara  ya  mambo  ya  ndani , ikiashiria  kwamba  watu waliojitokeza  wanafikia  asilimia 70 katika  uchaguzi uliofanyika  jana  Ijumaa , karibu sawa  na  jinsi  watu walivyojitokeza  kupiga  kura  katika  uchaguzi  wa  mwaka 2013 wakati  Rouhani  alipoingia  madarakani  kwa  ushindi wa  kishindo.

Upigaji  kura  ulirefushwa  kwa  masaa  sita kwasababu watu  wengi  bado  walikuwa  katika  mistari. Magazeti nchini  Iran yamesifu jinsi  watu  walivyojitokeza  kupiga kura, yakiandika  vichwa  vya  habari  kama "ushindi  wa kihistoria kwa  Wairani".

Kasi ya mabadiliko imekuwa ndogo

Iran wahlen 2017
Wapiga kura nchini IranPicha: Mehr

Tovuti  za  habari zinazounga  mkono mageuzi zimesema Rouhani  alikuwa  mshindi. Hata  hivyo  hawakutoa ushahidi, lakini  watu  kujitokeza  kwa  wingi  kunaweza kuelemea  upande  wa  Rouhani, ambapo wasi wasi mkubwa  wa  waungaji  wake  mkono ni kuchoshwa miongoni  mwa  wapiga  kura  wanaopendelea  mageuzi waliovunjwa  moyo  na  kasi  ndogo  ya  mabadiliko.

Rouhani , mwenye  umri  wa  miaka  68, ambaye  aliingia madarakani  akiahidi  kuiweka  Iran karibu  na  mataifa ulimwenguni na  kuwapa  raia  wake  uhuru  zaidi nyumbani , anakabiliana  na  upinzani  mkali  bila  kutarajia kutoka  kwa  Ebrahim Raisi  mwenye  msimamo  mkali, anayeungwa  mkono  na  kiongozi  mkuu  nchini  humo Ali Khamenei.

Uchaguzi  huo  ni  muhimu "kwa  hali  ya  baadaye  ya jukumu  la  Iran  katika  eneo  hilo  na  dunia  kwa  jumla", Rouhani , ambaye  alipata  makubaliano  na  mataifa makubwa  yenye  nguvu  kuiondolea  nchi  hiyo  vikwazo vya  kiuchumi, alisema  baada  ya  kupiga  kura.

Iran Präsidentschaftswahlen
Wakati wa kampeni ya urais nchini IranPicha: MIZAN

Raisi mwenye  umri  wa  miaka 56 , amemshutumu Rouhani  kwa  kuuvuruga  uchumi  wa  nchi  hiyo  na amesafiri  hadi  katika  maeneo wanakoishi  masikini, akizungumza katika  mikutano  akiahidi  mafao zaidi  ya kijamii   na  ajira.

Matokeo yataheshimiwa

Anaaminika  kuwa  anaungwa  mkono  na  majeshi  yenye ushawishi  mkubwa  nchini  humo  ya  walinzi  wa mapinduzi, pamoja  na  uungwaji  mkono  mkubwa   wa kiongozi  mkuu  nchini  humo Khamenei, ambaye madaraka  yake  yanapindukia  yale  ya  rais aliyechaguliwa  ambae  lakini  kwa  kawaida  hujiweka mbali  na  shughuli  za  kila  siku za  kisiasa.

"Naheshimu  matokeo  ya  kura  za  wananchi  na  matokeo yataheshimiwa  nami  pamoja  na  wananchi," Raisi alisema  baada  ya  kupiga  kura, kwa  mujibu  wa  shirika lisilokuwa  rasmi  la  habari  Fars.

Iran Präsidentschaftswahlen
Waungaji mkono rais wa sasa Hassan RouhaniPicha: IRNA

Hata  hivyo , Raisi   alijitokeza  katika  wizara  ya  mambo ya  ndani  mjini  Tehran  siku  ya  Ijumaa  na  kulalamikia upungufu wa  karatasi  za  kupigia  kura katika  vituo  vingi vya  kupigia  kura, kwa  mujibu  wa  shirika  la  habari  la Fars. Makaratasi  zaidi  ya  kupigia  kura  yalipelekwa katika  vituo, shirika  hilo  lilisema.

Insert Repoti Kitojo

Mhariri:Saumu Yusuf