1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zoezi la kuhesabu kura kuendelea Jamhuri ya Afrika ya Kati

7 Januari 2016

Karibu wagombea wote 30 waliowania kiti cha urais katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, kwa sasa wanaunga mkono zoezi la kuhesabu kura liendelee, licha ya 20 kati ya hao awali kutaka zoezi hilo lisitishwe.

https://p.dw.com/p/1HZqY
Picha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, kimesema kuwa karibu ya asilimia 77 ya kura tayari zimeshahesabiwa hadi sasa baada ya uchaguzi mkuu nchini humo kufanyika Disemba 30, 2015, ambao unatarajiwa kumaliza mzozo uliodumu kwa miaka mitatu na kusababisha maelfu ya watu kuuawa.

Kwa mujibu wa maafisa wa uchaguzi, Mawaziri Wakuu wawili wa zamani wanaongoza katika uchaguzi huo na wanatazamiwa kuchuana tena katika duru ya pili ya uchaguzi iliyopangwa kufanyika Januari 31.

Anicet Georges Dologuele amepata kura 259,211 ambazo zimehesabiwa hadi saa, huku Faustin-Archange Touadera akiwa amepata kura 222,391. Hakuna mgombea mwingine yeyote ambaye amepeta zaidi ya kura 135,000.

Waziri Mkuu wa zamani, Faustin-Archange Touadera
Waziri Mkuu wa zamani, Faustin-Archange TouaderaPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Umoja wa Mataifa umesema taarifa yake hiyo imetolewa baada ya kufanyika mkutano siku ya Jumanne kati ya wagombea wa kiti cha urais na maafisa waandamizi, akiwemo Parfait Onanga-Anyanga, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon na mkuu wa kikosi cha kulinda amani nchini humo, Balla Keita.

Awali wagombea 20 walitaka zoezi la kuhesabu kura lisitishwe

Taarifa hiyo imesema wagombea 28 wa urais wameonyesha kwamba wanataka zoezi la kuhesabu kura liendelee na watatumia tu ngazi ya kisheria iwapo watataka kuelezea malalamiko yao. Awali wagombea 20 waliwataka maafisa kusitisha zoezi la kuhesabu kura kutokana na kile walichokiita hitilafu zilizojitokeza wakati wa upigaji kura. Tangu siku ya Jumanne, angalau watano kati yao wamebadilisha msimamo wao.

Umoja wa Mataifa ni kiungo muhimu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako waasi wa Kiislamu na wanamgambo wa Kikristo mara kwa mara wamekuwa wakiwalenga raia. Kiasi ya moja ya tano ya watu milioni 5 wa nchi hiyo masikini, wamelazimika kuyakimbia makaazi yao.

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, Bangui
Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, BanguiPicha: Getty Images/AFP/M. Longari

Mzozo wa nchi hiyo ulizuka mwaka 2013, wakati ambapo waasi wa Seleka ambao wengi wao ni Waislamu walipotwaa mdaraka kwenye taifa hilo lenye Wakristo wengi, hivyo kuchochea ghasia kutoka kwa wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka.

Catherine Samba-Panza alikuwa rais wa mpito mwezi Mei, 2014 huku akiwa na mamlaka ya kuingoza nchi hiyo kuelekea katika uchaguzi wa kidemokrasia, katika kipindi cha mpito kilichoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Tangu wakati huo, ghasia za kijamii na kidini zimekuwa zikizuka hapa na pale, licha ya kuwepo wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa pamoja na vikosi vya Ufaransa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef