1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zoezi la kuwasaka wagombea Urais Marekani laanza.

Mohammed AbdulRahman3 Januari 2008

Mkusanyiko wa IOWA kuanza kutoa muangaza

https://p.dw.com/p/CjqY
Barack Obama anayewania kuwa rais wa kwanza mweusi nchini Marekani akihutubia huko Newton-Iowa.Picha: AP Photo

Wapiga kura katika kile kinachojulikana kama mkusanyiko wa IOWA huko Marekani watatoa muangaza wa wale wagombea urais kutoka vyama vyote viwili Demokratic na Republican, watakaoekewa nafasi ya kuweza kuingia Ikulu ya Marekani. Chini ya utaratibu wa uchaguzi huo wa rais nchini Marekani mkusanyiko huo ndiyo unaotoa changamoto katika kinyanganyiro cha kumpata mgombea Urais.

Kwa hakika kinyanganyiro hicho ambapo mamilioni ya dola hutumika katika kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa rais wa 2008 kinaanzia huko IOWA kwa siku tatu za mchuano kati ya Wademokrats Bibi Hilary Clinton na Mabwana Barack Obama na John Edwards. Wagombaea wote wamekua wakilizuru jimbo hilo na kuwa na mikutano kadhaa ya hadhara wakiwasihi wapiga kura kuwachagua, na kuepusha uwezekano wa kubwagwa. Obama aliuambia mkusanyiko wa watu 2,000 kuwa „Huu ndiyo wakati wetu wa kuweka alama ya kihistoria, moyo huu wa uwezekano huo.

Akaongeza seneta huyo mwenye umri wa miaka 46 na anayewania kuwa rais wa kwanza mweusi katika historia ya Marekani kuwa“mkianza na mimi basi hatutoshinda tu katika mkusanyiko huu bali pia duru ya uchaguzi wa mgombea chamani na tutashinda pia uchaguzi mkuu.“

Kwa upande wa Warepublican Mike Huckbee anayeongoza katika maoni ya wapiga kura anakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa Mitt Romney katika kuwania kuwa mgombea wa chama chao, huku wakifuatwa na John McCain. Inaelekea yeyote atakyekosa nafasi tatu bora katika hatua hii ya awali, atakua amewekwa pabaya katika kinyanganyiro hicho.

Baadhi ya wagombea ambao wamekua kwa mwaka mzima sasa wakiwania kura za IOWA wamekua mbioni katika kufanya mikutano ya hadhara na matangazo ya televisheni kuelezea misimamo na sera zao.

Mdemokrat Hilary Clinton ameahidi kuiongoza Marekani kinyume na hali ya sasa chini ya George W. Bush Bibi Clinton alisema „ Baada ya miaka saba hatimae tuna nafasi ya kuwa na mwanzo mpya.“

Maoni ya wapiga kurra yanaonyesha mchuano mkali kati ya Clinton na Obama kila mmoja akiwa na asili mia 28 ya kura na Edwards akifuata kwa kasoro ya pointi 2 katika nafasi ya tatu.

Kwa Warepublican Huckabee ana asili mia 28, Romney asili mia 26 na McCain katika nafasi ya tatu kawa asili mia 22.

Baada ya IOWA mchuano mwengine wa wagombea utakua katika jimbo la Newhempshire.Kinyanganyiro hicho kitaishia katika uchaguzi wa wajumbe wa vyama vyao baadae utakaoamua nani awe mgombea na watakaoteuliwa na vyama hivyo kuchuana katika uchaguzi huo wa rais wa Marekani mwezi Novemba.