1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zu Guttenberg arejea katika jukwaa la kisiasa

Oumilkher Hamidou13 Desemba 2011

Mbinu za zu Guttenberg, kutaka kurejea katika jukwaa la kisiasa baada ya kashfa ya kughushi shahada ya uzamifu na makadirio ya maisha kwa wenye kipato cha chini ni miongoni mwa mada kuu magazetini.

https://p.dw.com/p/13Rd6
Karl-Theodor zu Guttenberg
Karl-Theodor zu GuttenbergPicha: picture-alliance/dpa

Tuanzie na kisa cha zu Guttenberg aliyeajiriwa kuwa mshauri wa kamishna wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels. Gazeti la Badischer Neueste Nachrichten linaandika kuwa hata kama zu Guttenberg wiki hii amesababisha lawama kali kutolewa, kimoja amefanikiwa.

Gazeti hilo linahoji kuwa Ujerumani nzima inamtaja yeye tu. Na mara nyingi ndivyo inavyokuwa hivyo: mwenye ulimi mkali ndie anaeshinda. Zaidi ya hayo zu Guttenberg anajivunia kipaji ambacho hata wakosoajia wake wakubwa wanaungama. Na raia wa kawaida je?

Wao hawatakawia, kama si leo, basi kesho, itafika siku tu wataisahau kashfa ya zu Guttenberg kughushi shahada ya uzamifu. Ataendelea kuonekana hapa na pale na pengine muda si muda atajitokeza pamoja na mkewe. Na kwa namna hiyo anaweza kurejesha upya imani ya umma iliyomponyoka. Kwamba katika jamii kiu ya kuwa na mwanasiasa nyota na mkewe kama wao ni kikubwa, hali hiyo imemdhihirikia zu Guttenberg tangu zamani.

Gazeti la Braunschweiger Zeitung linajiuliza kama zu Guttenberg anafaa kweli kuendesha shughuli hizo mpya. Jibu ni tusubiri tuone. Mtu hahitaji kuwa shabiki wa mwanasiasa huyo kuweza kugundua kwamba yeye ni stadi wa kujitembeza. Pengine atafanikiwa kweli kuusaidia Umoja wa Ulaya unaodorora katika masuala ya mtandao na tawala za mabavu.

Karl-Theodor zu Guttenberg
Karl-Theodor zu GuttenbergPicha: picture-alliance/dpa/Halifax International Security Forum

Lawama zitahanikiza ikiwa atashindwa kufanikisha kilichomleta katika Umoja wa ulaya. Hadi wakati huo lakini kuna kifungu cha sheria kinachomlinda nacho kinasema:mtu hawezi kuhukumiwa mara mbili kwa kosa moja.

Mada ya pili magazetini inahusu msimamo wa kanisa kuhusiana na biashara ya silaha nchini Ujerumani. Gazeti la "Ludwigsburger Kreiszeitung" linaandika: kuwa mara zote uamuzi kuhusu biashara ya nje unapitishwa kuambatana na masilahi ya kiuchumi na sio kutumikia amani. Zaidi ya hayo, kuna maamuzi yanayopitishwa kichini chini mfano wa ile biashara ya silaha kwa Saud Arabia.

Serikali kuu ya Ujerumani mpaka sasa imenyamaza kimya. Wakati umewadia wa kuzidisha makali ya vizuiwi vya biashara ya silaha. Muhimu zaidi ni kuhakikisha bunge linakuwa na sauti katika maamuzi kama hayo yanayopitishwa. Na hilo ndilo dai lililotolewa hivi karibuni na baraza la makanisa. Na onyo lao la serikali kuu linabidi ilizingatie.

Kanisa la Kiinjili
Kanisa la KiinjiliPicha: Pfarrerin Petra Schulze

Mada yetu ya mwisho inahusiana na makadirio ya maisha kwa wenye kipato cha chini. gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger linaandika kuwa kupungua makadirio ya maisha miongoni mwa baadhi ya tabaka ya wananchi bila ya shaka sio sababu ya hoja kwamba watu wastaafu wakiwa na umri wa miaka 67.

Hata kama maelefu ya watu hawatoishi muda mrefu kama ilivyokuwa ikitarajiwa tangu miaka kumi nyuma, sehemu kubwa ya wakaazi haihusiki na makadirio hayo. Watu wengi zaidi wanakula pensheni kwa muda mrefu zaidi katika wakati ambapo idadi ya wale wenye uwezo wa kuchangia katika fuko la malipo ya uzeeni inaendelea kupungua.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Othman Miraji