1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma atupwa jela kwa kuipuuza mahakama

29 Juni 2021

Rais wa zamani wa Afrika Kusini Jacob Zuma amehukumiwa kifungo cha miezi 15 jela baada kupuuza amri ya mahakama ya kumtaka kufika mbele ya tume maalum inayochunguza madai chungunzima ya rushwa enzi ya utawala wake.

https://p.dw.com/p/3vlWg
Jacob Zuma | Korruptionsverfahren
Picha: Phill Magakoe/Reuters

Hukumu hiyo iliyotolewa na kaimu jaji mkuu wa Afrika Kusini  Sisi Khampepe bila ya Zuma mwenyewe kuwepo mahakamani ni ya kwanza katika hisotria ya taifa hilo kwa rais mstaafu kuhukumiwa kifungo gerezani.

Jaji  Khampepe amesema kwamba Zuma ametiwa hatiani kwa kosa la kutoheshimu na kuipuuza mahakama baada ya kushindwa kutii amri ya kufika mbele ya tume ya mahakama inayochunguza madai ya rushwa, uhujumu wa taifa na udanganyifu enzi ya utawala wake.

Uamuzi huo umetolewa na mahakama ya katiba ambacho ndicho chombo cha zaidi cha utoaji haki nchini Afrika Kusini na kushindwa kwa Zuma kufika mbele ya tume iliyoundwa na mahakama kumetajwa kuwa ni kitendo kikubwa cha dharau kubwa.

Akisoma hukumu hiyo Jaji Khampepe alisema "Jacob Zuma anahukumiwa kifungo cha miezi 15. Bwana Zuma anaamriwa kujisalimisha mwenyewe kwenye kituo chochote cha polisi cha Afrika kusini au cha mjini Johannesburg ndani ya siku tano tangu kutolewa kwa amri hii"

Ukaidi wa Zuma ni wa tangu zamani 

Sisi Khampepe | südafrikanische Richterin
Kaimu Jaji Mkuu wa Afrika Kusini Sisi KhampepePicha: Siphiwe Sibeko/REUTERS

Ikumbukwe kuwa tangu mwanzo Zuma alikwishaeleza kutokuwa tayari kufika mbele ya tume ya mahakama ambayo hadi sasa imekwishasikiliza ushahidi unaomuhusisha moja kwa moja kiongozi huyo wa zamani na makosa kadhaa.

Kupitia barua yake ya kurasa 21 aliyomwandikia jaji mkuu wa Afrika Kusini, ambayo mahakama imeitaja kuwa ya "fedheha", Zuma alidai kwamba yuko tayari kwenda jela lakini siyo kujieleza mbele ya tume hiyo.

Katika barua hiyo ambayo yeye mwenyewe aliiweka wazi kwa umma, Zuma anadai kwamba mwenyekiti wa tume hiyo ambaye ni naibu jaji mkuu Raymond Zondo hatomtendea haki na kwamba ushahidi uliowasilishwa dhidi yake umechochewa kisiasa.

Familia ya Gupta na madai ya rushwa wakati wa utawala wa Zuma 

Südafrikas ehemaliger Präsident Raymond Zondo
Mwenyekiti wa Tume ya kuchunguza tuhuma za rushwa enzi ya utawala wa Jacob Zuma, Raymond Zondo.Picha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Baadhi ya mawaziri wa zamani, maafisa wa ngazi ya juu wa serikali na wakuu wa mashirika ya umma ni miongoni mwa wale waliotoa ushahidi unaomuhusisha Zuma na kashfa chungunzima za rushwa.

Wengi wamesema wamesema kwamba wakati akiwa rais Zuma aliruhusu baadhi ya watu kutoka familia ya Gupta inayohusishwa na kashfa kadhaa nchini Afrika Kusini kushinikiza uteuzi wa mawaziri na hata namna ya kufikiwa kwa mikataba ya fedha nyingi kwenye kampuni za umma.Madai yote hayo lakini yanakanushwa na Zuma mwenyewe.