1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma awasili Libya

30 Mei 2011

Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini amewasili Libya kwa kile kinachoitwa "kutafuta suluhisho la amani la mgogoro" unaoiakabili nchi hiyo, huku baadhi ya makamanda wa Muammar Gaddafi wakiripotiwa kumuacha mkono.

https://p.dw.com/p/11QrQ
Rais Jacob Zuma (kulia) na mwenzake wa Urusi, Dmitry Medvedev
Rais Jacob Zuma (kulia) na mwenzake wa Urusi, Dmitry MedvedevPicha: AP

Alipowasili uwanja wa ndege mjini Tripoli, Rais Zuma alipokelewa kwa zulia jekundu na viongozi kadhaa wa Libya, ingawa Gaddafi hakuonekana uwanjani hapo.

Bendi ya muziki ya watoto wadogo waliokuwapo uwanjani hapo, ilimuimbia Rais Zuma wimbo wa Kiingereza: "We want Gaddafi" yaani tunamtaka Gaddafi, huku watoto hao wakipeperusha bendera za Libya na kuinua picha za Gaddafi.

Baadaye televisheni ya nchi hiyo ilimuonesha kiongozi huyo wa Afrika ya Kusini akizungumza na watu waliotajwa kuwa ni wazee wa makabila mbalimbali.

Hii ni ziara ya pili kwa Zuma tangu mgogoro huu uanze, ambapo ile ya mara ya kwanza haikuwa na maendeleo makubwa, baada ya upande wa waasi na wa serikali kutafautiana juu ya suala la msingi la kuondoka ama kubakia madarakani kwa Gaddafi, likiwa kama sharti muhimu la kufikia makubaliano.

Mwanzoni ilikuwa imevumishwa kwamba, ziara hii ya Zuma ingelizungumzia suala hilo la kuondoka kwa Gaddafi, lakini baadaye ofisi ya Zuma ilikanusha jambo hilo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika ya Kusini, Maite Nkoana-Mashabane, amesema kwamba anachokitafuta Rais Zuma ni kusitishwa kwa mapigano ili majadiliano ya kufanya mageuzi ya kisiasa nchini Libya yaanze.

"Ziara hii ni ya kufuatilia pendekezo la mpango wa amani la Umoja wa Afrika, ambalo linasema kwamba tatizo tunalokabiliana nalo Libya ni la kisiasa. Kwa hivyo, hatuamini kuwa suluhisho la kijeshi linaweza kutatua matatizo ya kisiasa." Nkoana-Mashabane aliwaambia waandishi wa habari mapema leo.

Hata hivyo, suluhisho hilo la kisiasa linakabiliwa na changamoto kubwa ya kuendelea kwa mashambulio ya kijeshi kutoka kila upande, wa Gaddafi, wa waasi na wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, huku ikihofiwa kwamba nchi za Magharibi kupitia NATO, zinakwenda mbali mno katika operesheni yao dhidi ya Gaddafi.

Ingawa NATO inakataa kwamba, hailengi kumuondoa madarakani kiongozi huyo wa Libya, kwa kuwa hilo si miongoni mwa maagizo ya Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini matukio kadhaa ya mashambulio ya NATO yanaelekeza huko.

Admirali wa jeshi la Marekani, Samuel Locklear, anayeongoza kamandi ya operesheni ya NATO kutokea Naples, Italia, alikataa uwezekano wa kupeleka wanajeshi wa miguu nchini Libya kwa sasa, lakini akasema wanaweza kufanya hivyo baada ya Gaddafi kuanguka. Locker ameyasema hayo leo akiwa kwenye Jukwaa la NATO huko Varna, Bulgaria.

Wakati huo huo, Shirika la Habari la AFP limeripoti kwamba viongozi nane wa ngazi ya juu wa jeshi la Libya wamemuacha mkono Gaddafi na kwamba watazungumza na waandishi wa habari leo hii mjini Rome, Italia.

"Miongoni mwa viongozi hao nane wa kijeshi, wamo majenerali wanne. Wote wamejiunga na mapinduzi. Na sasa wako Rome." Amesema Mkuu wa Kitengo cha Habari cha Baraza la Mpito la Kitaifa la Libya, Mahmoud Shammam.

Ingawa hakuna undani zaidi wa wanajeshi hao, Ijumaa iliyopita, shirika la habari la Tunisia, TAP, liliripoti kwamba kundi la wanajeshi wa Libya, wakiwemo viongozi wa ngazi za juu, walikuwa wamewasili Tunisia kupitia baharini. Kwa mujibu wa TAP, kundi hilo la watu 34, wakiwemo pia raia wa kawaida, liliwasili kwa kutumia mashua mbili ndogo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Othman Miraji