1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zuma na Uchaguzi Mkuu Afrika Kusini.

Halima Nyanza/DPAE16 Aprili 2009

Hata kabla ya uchaguzi mkuu wa Afrika kusini kufanyika, mshindi tayari ameshatabiriwa.

https://p.dw.com/p/HYVd
Kiongozi wa Chama tawala cha Afrika kusini, Jacob Zuma, ambaye anatarajiwa kushinda katika uchaguzi ujao nchini humo.Picha: picture-alliance/dpa

Zimesalia siku saba kabla ya , Waafrika kusini kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa nne nchini humo ukiwa ni pamoja na ule wa serikali za Mitaa, tangu waafrika weusi nchini humo kuanza kuwa na haki ya kupiga kura baada ya kumalizika siasa za ubaguzi wa rangi nchini na mtengano 1994. Ingawa vyama 11 vinashiriki katika kinyang'anyiro hicho, mshindi tayari anajulikana--Chama tawala cha nchi hiyo cha African National Congress ANC na kiongozi wake Jacob Zuma, ambaye hivi karibuni aliibuka mshindi katika kashfa ya rushwa iliyokuwa ikimkabili.


Jacob Zuma ambaye karibuni tu, amesherehekea miaka 67 ya kuzaliwa kwake aliibuka tena kukiongoza chama hicho tawala cha Afrika kusini cha ANC, mwezi Decemba 2007, baada ya kumshinda mpinzani wake, aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Thabo Mbeki, ambaye miaka miwili nyuma, alimfukuza Bwana Zuma katika nafasi yake ya Umakamu wa Rais wa nchi hiyo, baada ya rafiki wa Bwana Zuma na mshirika wake kibiashara, Schabir Shaik kukutwa na hatia ya kumhonga Bwana Zuma.


Katika kipindi hiki ambacho tuhuma zote za rushwa na ufisadi dhidi yake zikiwa zimeondolewa, kiongozi huyo wa ANC ameonekana wazi kuwa atachaguliwa katika uchaguzi ujao wa Rais nchini humo.


Jacob Zuma ambaye amezaliwa katika wilaya ya Nkandla kwenye jimbo la Kwa Zulu-Natal mwezi Apriil mwaka 1942, alijiunga na chama hicho cha ANC akiwa na miaka 17.


Kama wanaharakati wengine wa nchi hiyo waliokuwa wakipigania uhuru na demokrasia, Zuma aliwahi kukamatwa, kufungwa pamoja na kuishi uhamishoni kwa miaka 15, na alirejea nchini mwake mwaka 1990.


Tangu kufanyika kwa uchaguzi wa kidemokrasi mwaka 1994, baada ya kumalizika kwa utawala wa kibaguzi, Jacob Zuma alishika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama chake cha ANC na katika serikali pia.


Na sasa wakati akijiandaa kuwa Rais ajaye wa nchi hiyo, Bwana Zuma anasema atafanya kazi bila ya kuchoka kuweza kuinua maisha ya watu wa nchi hiyo na wakati huohuo kupambana na rushwa serikalini.


Aidha amesema hatawavumilia wale wote watakaojiunga na chama hicho tawala cha ANC, kwa ajili ya kujitajirisha.


Aidha akitoa ujumbe wake kwa wapiga kura, Jacob Zuma anasema iwapo atakuwa Rais wa nchi hiyo, serikali mpya ya ANC, itatekeleza wajibu wake.


Hata hivyo katika kura ya maoni iliyopigwa hivi karibuni, Wa Afrika kusini wengi wamepoteza imani na chama hicho tawala, ingawa wengi bado watakipigia kura katika uchaguzi huo utakaofanyika Aprili 22.


Mgogoro wa viongozi katika chama hicho tawala cha ANC, ulisababisha chama hicho kugawanyika na hatimaye kuundwa kwa chama kipya cha Congree of the People, ambacho nacho pia kinashiriki katika uchaguzi huo.

Licha ya Bwana Zuma kutarajia kushinda katika uchaguzi huo wa Rais ujao nchini humo, ameelezwa kuwa bado anakazi kubwa ya kufanya.


Mwandishi: Halima Nyanza/DPAE

Mhariri:M.Abdul-Rahman