Faustin Kayumba: Serikali ya Rwanda inahangaisha upinzani | Afrika | DW | 01.02.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Afrika

Faustin Kayumba: Serikali ya Rwanda inahangaisha upinzani

Kayumba Nyamwasa ambaye amekuwa akiishi uhamishoni nchini Afrika Kusini tangu mwaka 2010, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, kazi ya serikali ya Rwanda imekuwa ni kuwatishia na kuwahangaisha wapinzani.

Mkuu wa zamani wa jeshi la Rwanda Faustin Kayumba Nyamwasa anayeishi uhamishoni ameishutumu serikali ya Rwanda kwa kuwatisha na kuwahangaisha wapinzani, baada ya waendesha mashtaka wa serikali kutoa waranti wa kukamatwa kwake.

Kulingana na tovuti ya habari nchini Rwanda Igihe, ambayo ina mafungamano na utawala wa Rais Paul Kagame, ofisi ya mwendesha mashtaka ilitoa waranti wa kukamatwa kwa jenerali Kayumba Nyamwasa pamoja na viongozi wa kundi jipya la waasi kwa jina P5.

Kundi la P5 linavijumuisha vyama vitano vya upinzani nchini Rwanda, kikiwemo chama cha Rwanda National Congress (RNC) chake Kayumba Nyamwasa ambacho serikali ya Rwanda inakishutumu kwa kuchochea uasi, madai ambayo RNC imekanusha.

 

Vitisho dhidi ya wapinzani Rwanda.

Kayumba Nyamwasa ambaye amekuwa akiishi uhamishoni nchini Afrika Kusini tangu mwaka 2010, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, kazi ya serikali ya Rwanda imekuwa ni kuwatishia na kuwahangaisha wapinzani. Ameongeza kuwa ukimpinga Rais Kagame, labda atakuua au atakufunga jela la sivyo atakuhangaisha.

Kumekuwa na majaribo manne ya kumuua Kayumba Nyamwasa.

Hakuna kauli yoyote iliyotolewa na serikali ya Rwanda huku Afrika Kusini ikisema haijafahamishwa kuhusu waranti hizo, ambazo zimemlenga pia shemeji yake Kayumba Nyamwasa, Frank Ntwali na Kennedy Gihana ambaye ni wakili anayefanya shughuli zake Afrika Kusini.

Rais wa Rwanda Paul Kagame

Rais wa Rwanda Paul Kagame

Mkuu huyo wa zamani wa jeshi la Rwanda amesema waranti wa kukamatwa kwake uliotolewa Januari 18, ni njama tu ambazo zimekusudiwa kubadili mtizamo na mawazo kuhusu uchunguzi upya ulioanza mjini Johannesburg Januari 16, dhidi ya mauaji ya mpinzani wa Rwanda Patrick Karegeya, ili jumuiya ya kimataifa pamoja na vyombo vya habari vijihusishe mno na suala la waranti badala ya uchunguzi unaoendelea.

Kulikuwa na uhusiano kati ya serikali na wauaji wa Karegeya?

Karegeya ambaye alikuwa mkuu wa zamani wa ujasusi wa Rwanda na pia mpambe wa Rais Kagame, alipatikana amekufa katika chumba cha hoteli ya kifahari mjini Johannesburg Januari 1, 2014. Hakuna yeyote ambaye ameshtakiwa kuhusiana na kifo chake.

Mnamo Januari 21, ofisi ya mwendesha mashtaka ya Afrika Kusini ilisema kulikuwa na uhusiano wa karibu kati ya utawala wa Kagame na washukiwa wanne wa Rwanda ambao walitoka nchini Afrika Kusini punde tu baada ya Karegeya kuuawa. Mmoja kati ya washukiwa hao ndiye alimhifadhia Karegeya hoteli.

Serikali ya mjini Kigali aghalabu hulaumiwa kwa kuwatishia wapinzani walioko uhamishoni kwa kutaka kuwaua, madai ambayo Kagame amekuwa akikanusha.

 

Mhariri: Josephat Charo