1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

2018 ulikuwa mwaka mbaya kwa waandishi wa habari wa Ulaya

Sylvia Mwehozi
13 Februari 2019

Ripoti ya baraza la Umoja wa Ulaya kuhusu uhuru wa vyombo vya habari inaonyesha kuwa mwaka 2018 ulikuwa mwaka mbaya zaidi kwa waandishi wa habari barani Ulaya tangu kumalizika kwa vita baridi. 

https://p.dw.com/p/3DGnG
Bildkombi - Raif Badawi und Jamal Khashoggi

Ripoti hiyo ya baraza la Ulaya ya mwaka 2019 iliyopewa kichwa cha habari Demokrasia hatarini, imebaini  kuwa uhuru wa vyombo vya habari katika nchi wanachama uko katika hali mbaya tangu kumalizika kwa vita baridi. Ripoti hiyo iliyotolewa kwa ushirikiano na Jukwaa la ulinzi na usalama wa waandishi wa habari, inasema mashambulizi dhidi ya wanataaluma wa habari yameongezeka maradufu katika kipindi cha miaka michache iliyopita.

Waandishi wa habari wawili waliuawa mwaka 2018 kuhusiana na kazi zao, akiwemo Jan Kuciak wa Slovakia pamoja na Jamal Khashoggi ambaye kifo chake katika ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul bado kinachungzwa. Jukwaa hilo lilipokea taarifa za mashambulizi mengine kadhaa ikiwa ni pamoja na mabomu ya kwenye magari, shambulio la visu, uchomaji wa mali na uvamizi wa ofisi za magazeti.

Lakini mashambulizi hayo si tu yalikuwa ya kimwili bali ripoti inaeleza kuwa mwaka 2018 ulionekana kuelekea zaidi kwenye mashambulizi ya maneno na unyanyapaa wa umma dhidi ya vyombo vya habari na waandishi habari binafsi katika nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Slowakei Bratislava Demonstrationen nach Journalistenmord
Maandamano mjini Bratislava ya kupinga kuuawa kwa Jan KuciakPicha: Reuters/R. Stoklasa

Mfano wa mashambulizi hayo ni kauli zilizotolewa na viongozi wa siasa zikiwemo za wale waliosema wanasikitika kwamba bado waandishi wa habari hawajatoweka kabisa duniani na hata kutoa orodha ya wandishi wa habari ambao walidiriki kukosoa serikali na kuwaita wasaliti.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo waandishi wa habari 130 bado walikuwa kizuizini hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana wengi ni nchini Uturuki. Nchi hiyo imesalia kuwa taifa lenye idadi kubwa duniani lenye waandishi wa habari walioko gerezani, ambapo zaidi ya waandishi 200 walikamatwa tangu kushindwa kwa jaribio la mapinduzi mnamo mwaka 2016.

Aidha, ripoti hiyo imekosoa utamaduni wa kushindwa kwa mamlaka za serikali katika kuwatambua, kuwashitaki na kuwaadhibu wale wote wanaohusika na uhalifu wa vurugu dhidi ya waandishi. Nchi 47 wanachama wa Baraza hilo waliahidi kuchukua hatua za kukomesha kinga mwaka 2016 lakini hakuna hatua iliyopigwa. Ripoti inapendekeza hatua za haraka kuchukuliwa ili kuwalinda wafanyakazi dhidi ya mashambulizi hayo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi

Mhariri: Daniel Gakuba