1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

7 wakamatwa jijini London kwenye msako

Zainab Aziz
23 Machi 2017

Polisi nchini Uingereza wamesema wanaamini mashambulizi ya jana yanahusiana na ugaidi wa makundi yenye itikadi kali za Kiislamu. Hadi kufikia sasa polisi wamewakamata takriban watu 7 katika miji ya London na Birmingham.

https://p.dw.com/p/2ZnoM
Großbritannien Terroranschlag in London | Westminster Bridge am Tag danach
Picha: Reuters/D. Staples

Watu wanne waliuwawa kwenye shambulio hilo katika daraja la Westminster huko mjini London mahala yaliko majengo ya serikali ikiwa ni pamoja na bunge la Uingereza. Afisa mkuu wa kitengo cha kukabiliana na ugaidi nchini Uingereza Mark Rowley amewaambia waandishi wa habari kwamba maafisa wa polisi walifanya msako kwenye makao mbalimbali na kuwakamata watu saba kutoka miji ya London, Birmingham na miji mingineyo.

Idadi ya watu waliouwawa kwenye mashambulio hayo ni watu wanne, mwanamke anayekadiriwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 40, mwanamume mwenye umri wa miaka 48 na afisa wa polisi Keith Palmer aliyekuwa anatimiza majukumu yake ya kazi katika maeneo ya nje ya bunge wakati alipochomwa kisu na mshambuliaji huyo, Keith alikuwa na miaka 48. Wa nne ni mshambuliaji mwenyewe ambaye aliuwawa kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi. Mkuu wa kitengo cha kupambana na ugaidi nchini Uingereza Mark Rowley alipoulizwa na wandishi wa habari juu ya uraia wa mshambuliaji huyo aKwa wakati huu hawezi kusema zaidi juu mshambuliaji huyo kutokana na uchunguzi unaoendelea na vilevile hawezi kuwatambulisha waliouwawa kwa sababu raia hao wanatoka katika nchi mbalimbali na kwamba bado wanawasiliana na nchi walikotoka raia hao pamoja na familia zao.

UK | Mark Rowley, Chef der Anti-Terroreinheit von New Scotland Yard
Mkuu wa kupambana na ugaidi Uingereza Mark RowleyPicha: Getty Images/AFP/J. Tallis

Rowley alieleza kuwa katika mashambulio hayo ya jana watu 40 walijeruhiwa  ambapo watu 29 walipelekwa hospitali na kati ya watu hao 7 wamo katika hali mahututi.  Kwa mujibu wa waziri wa ulinzi wa Uingereza Sir Michael Fallon uchunguzi unaendelea kubaini iwapo mshambuliaji huyo alikuwa anaungwa mkono na watu au kundi lolote. Hata hivyo polisi wamesema wanaamini mshambuliaji huyo alikuwa peke yake na kwamba alikuwa shabiki wa ugaidi wa kimataifa.

Mshambuliaji huyo aliliendesha gari lake na kuwagonga watu kwa kudhamiria kwenye daraja la Westminster kabla ya kuligongesha gari lake katika lango la Bunge.  Baadae alimshambulia ofisa wa polisi kwa kumchoma kisu kabla ya yeye mwenyewe kupigwa risasi na kuuwawa na polisi. Kiwango cha mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Uingereza kilikuwa kiko juu kumaanisha kulikuwa na uwezekano mkubwa wa shambulio la kigaidi kutokea wakati wowote. Mji wa London umekuwa ukilengwa na mashambulio ya kigaidi katika mwongo huu.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE/AFPE/RTRE

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman