1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

A. Kusini yafanya mnada wa pembe za Faru mtandaoni

Lilian Mtono
24 Agosti 2017

Afrika Kusini kwa mara ya kwanza imefanya mnada wa pembe za faru kupitia mtandaoni, ingawa hatua hiyo imepingwa vikali na makundi ya uhifadhi yanayodai kwamba biashara hiyo inaweza kuchochea ujangili

https://p.dw.com/p/2imCY
Kenya nördliches Weißes Nashorn
Picha: DW/Andrew Wasike

Afrika Kusini kwa mara ya kwanza imefanya mnada wa pembe za faru kupitia mtandaoni, ingawa hatua hiyo imepingwa vikali na makundi ya uhifadhi yanayodai kwamba mauzo yanayokubalika kisheria na ya ndani, yanaweza kuhamasisha wawindaji haramu. Mnada huo ulifunguliwa jana jumatano.

Mnada huo wa siku tatu ulioratibiwa na mmiliki wa hifadhi kubwa kabisa duniani ya ndovu ulifunguliwa katika dakika za mwisho mwisho baada ya vuta-nikuvute ya kisheria na kuuchelewesha kwa siku mbili.

John Hume, anayemiliki faru 1,500 katika hifadhi yake iliyopo kaskazini mwa Johannesburg, ana kiasi cha tani sita za pembe hizo za faru na ananuia kuuza vipande 264 vyenye uzito jumla wa kilogramu 500.

Alizipata pembe hizo baada ya kuwalaza wanyama hao na kuzikata pembe, mbinu ambayo anasema ni ya kibinaadamu na inawazuia wawindaji haramu. 

Wanaharakati walipinga mnada huo wakihofia utahamasisha usafirishaji haramu na kufifisha mkakati wa miaka 40 wa kimataifa wa kukabiliana na biashara ya pembe za faru, ambazo zina soko kubwa katika bara la Asia, kama mtaalamu wa masuala ya usafirishaji haramu wa wanyamapori, Julian Rademeyer, alivyozungumza na shirika la habari la AFP.

Südafrika Kampf gegen die Wilderei
Mmoja ya Faru kama anavyoonekana baada ya kukatwa pembePicha: Reuters/S. Sibeko

Amesema pia kwamba taasisi za serikali hazina uwezo wa kudhibiti biashara za ndani, wakati pia kukiwa na upungufu wa rasilimali za kuwasaidia polisi kufuatilia mitandao ya wawindaji na wafanyabiashara haramu. 

Hakukutolewa tamko lolote na serikali kufuatiwa kufunguliwa kwa mnada huo, ambao unakuja baada ya mahakama ya juu ya nchi hiyo kuondoa zuio la miaka minane la biashara ya ndani ya pembe za faru mwezi Aprili.  

Mvutano wa kisheria ulichelewesha kufunguliwa kwa mnada huo kwa siku mbili, lakini Hume alipewa kibali cha mnada siku ya Jumatatu.

Wauzaji hawakutoa bei ya kuanzia kwa wazabuni, lakini mzabuni muhimu anahitaji kulipa dola za Kimarekani 7,570, kama gharama za kujiandikisha na ni wazabuni waliojiandikisha tu wanaweza kuingia kwenye mchakato wa zabuni hiyo.

Siku ya Jumatatu, Waziri wa Masuala ya Mazingira Edna Molewa alisema serikali ilikuwa inafunga kila mwanya unaoweza kutengeneza ujanja wa kukwepa kanuni za kimataifa. 

Pembe za faru zinauzwa kwa gharama kubwa katika bara la Asia, ambako inakadiriwa kilo moja huuzwa kwa hadi Euro 50,000 katika masoko ya ulanguzi, na kuzidi hata gharama ya dhahabu. Pembe hizo zina protini aina ya keratini, sawa na iliyopo kwenye kucha za binaadamu na huuzwa katika muundo wa poda na hutumiwa kama tiba ya saratani na maradhi mengine.

Mwandishi: Lilian Mtono/AFP/AP
Mhariri: Mohammed Khelef