1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abadi ataka kura ya uhuru wa Wakurdi ifutwe

Mohammed Khelef
27 Septemba 2017

Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi, ametaka kura ya maoni iliyowapa Wakurdi haki ya kuunda taifa lao ifutwe mara moja katika wakati ambapo uhasama kati serikali yake na ya Wakurdi ukizidi kushamiri.

https://p.dw.com/p/2koW2
Irak Haider al-Abadi, Ministerpräsident
Picha: Reuters TV

Licha ya kwamba matokeo rasmi ya kura hiyo hayatangazwa wazi, lakini inafahamika kuwa wapigakura wengi waliamua kuihuisha ndoto ya karne nzima sasa ya kuwa na taifa huru la Wakurdi.

Hata hivyo, kiongozi wa muda mrefu wa Wakurdi nchini Iraq, Masoud Barzani, anasema kura hiyo haitapelekea kutangazwa moja kwa moja kwa uhuru na badala yake inapaswa kutumika kufungua milango ya majadiliano zaidi.

Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni usiku wa jana, Barzani alimtolea wito Abadi kutokufunga mlango wa majadiliano, akisema ni "majadiliano pekee yatakayotatuwa matatizo."

"Tunaihakikishia jumuiya ya kimataifa juu ya utayarifu wetu wa kuingia kwenye mazungumzo na serikali ya Iraq," alisema Barzani, akisisitiza kwamba kura ya maoni haikukusudiwa kuuchora mpya mpaka kati ya Kurdistan na Iraq, wala kuweka mwengine.

Lakini Abadi, ambaye tangu awali aliikataa kura hiyo akisema iko kinyume cha sheria, amewaambia wabunge hivi leo kwamba hakutakuwa na hoja yoyote ya kuyatumia matokeo ya kura hiyo kama msingi wa majadiliano.

"Kura ya maoni lazima ifutwe na majadiliano yaanze kwa kuzingatia katiba ya nchi. Kamwe hatutafanya majadiliano kwa kuzingatia matokeo ya kura hii ya maoni," alisema Abadi bungeni asubuhi ya leo, huku akiapa kuwa serikali yake itahahakikisha kuwa mkoa mzima wa Kurdistan unaheshimu katiba ya Iraq.

Dunia yawashinikiza Wakurdi

Irak Kurden-Führer Massud Barsani
Kiongozi wa Wakurdi nchini Iraq, Masoud Barzani, anataka serikali kuu ianze majadiliano kwa kuzingatia matokeo ya kura ya maoni.Picha: picture-alliance/dpa/AP/K. Mohammed

Shinikizo dhidi ya Wakurdi limeongezeka tangu kura hiyo ipigwe, si kutoka serikali kuu mjini Baghdad pekee, bali hata kutoka Uturuki, ambako serikali ya huko imetishia kuchukuwa hatua kadhaa, ikiwemo ya kukata njia za usafirishaji kwa ajili ya mkoa huo.

Wakitaka kuihuisha ndoto ya muda mrefu ya kuwa na dola lao wenyewe, Wakurdi waliamua kuendelea na mipango yao ya kuitisha kura hiyo ya maoni wakikaidi upinzani mkali kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, zikiwemo Marekani na Umoja wa Mataifa.

Kura hii imezua wasiwasi wa machafuko na uwezekano wa mapigano ya kijeshi yatakayowahusisha Wakurdi, ambao ni washirika muhimu katika mashambulizi ya kimataifa dhidi ya kundi la kigaidi lijiitalo Dola la Kiislamu (IS).

Mbali na Iraq na Uturuki, Syria na Iran nazo pia zina idadi kubwa ya Wakudri wanaokaa kwenye eneo linalotambuliwa kama Kurdistan, mpakani mwa mataifa hayo manne, na ambalo Wakurdi wanalitambua kama taifa lao. 

Mataifa hayo yanaichukulia hatua hii ya kuitishwa kura ya maoni ya uhuru, kuwa ni njama ya kuyamega na kuyanyang'anya ardhi zake.

Kura hii ya maoni, hata hivyo, hailazimishi kuheshimiwa na mataifa mengine wala haiitamki Kurdistan moja kwa moja kuwa ni huru, lakini inaonekana na Wakurdi wengi kuwa ni hatua kubwa sana kuelekea uwezekano wa kuundwa kwa taifa lao wenyewe.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo