1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abbott Waziri Mkuu mpya Australia

8 Septemba 2013

Chama cha upinzani cha kihafidhina Australia kimeiingia madarakani Jumamosi(07.09.2013) na kumaliza miaka sita ya utawala wa chama cha Leba kwa kupata imani ya wapiga kura kutokana na ahadi ya kuimarisha uchumi.

https://p.dw.com/p/19dZv
Tony Abbott Waziri Mkuu mpya wa Australia.
Tony Abbott Waziri Mkuu mpya wa Australia.Picha: Getty Images

Chama hicho kimeahidi kukomesha kodi inayochukiwa ya hewa ukaa,kuimarisha uchumi unaodorora na kurudisha utulivu wa kisiasa baada ya miaka kadhaa ya malumbano ya ndani ya chama cha Leba.

Waziri Mkuu Kevin Rudd amesema katika hotuba kwa wafuasi wake kwamba "Nyoyo za wanachama wa Leba ni nzito katika taifa zima na nikiwa kama waziri mkuu wenu na kiongozi wenu bungeni wa chama adhimu cha Leba nchini Australia nakubali kuwajibika."Rudd alitowa kauli hiyo baada ya kumpigia simu kiongozi wa upinzani Tony Abbott kukiri kushindwa kwake katika uchaguzi huo ambapo amesema "Nimejitahidi kwa kadri ya uwezo wangu, lakini haikutosha kuweza kushinda."

Katika hotuba yake hiyo ya kukubali kushindwa Rudd amesema atajiuzulu kama kiongozi wa chama.Amesema anaamini wananchi wa Australia wanahitaji kuanza upya na uongozi wao.

Wakati asilimia 90 ya kura zikiwa tayari zimehesabiwa Tume ya Uchaguzi ya Australia imesema Waliberali wanaongoza kwa asilimia 57 dhidi ya 47 za chama cha Leba.

Wananchi walikuwa wamechoshwa na Leba

Ushindi wa muungano wa kihafidhina unaoongozwa na chama cha Kiliberali umekuja licha kutoshabikiwa kwa Abbott mwenye umri wa miaka 55, mseminari wa Kanisa Katoliki na msomi wa Rhodes ambaye haikuwa rahisi kukubalika na wapiga kura wa kike na aliwahi kupachikwa jina la mtu "asiechagulika" na wapinzani na hata baadhi ya wapiga kura.

Waziri Mkuu wa Australia Kevin Rudd akikiri kushindwa. (07.09.2013)
Waziri Mkuu wa Australia Kevin Rudd akikiri kushindwa. (07.09.2013)Picha: AFP/Getty Images/Greg Wood

Lakini wapiga kura kwa kiasi kikubwa walikuwa wamechoshwa na chama cha Leba na Rudd baada ya kuwapo kwa mapambano ya muda mrefu ya kuwania madaraka kati yake na naibu wake wa zamani Julia Gillard. Gillard ambaye alikuja kuwa waziri mkuu wa kwanza mwanamke wa taifa hilo baada ya kumn'goa Rudd katika uchaguzi wa chama hapo 2010,aliishia kupoteza wadhifa wake kwa Rudd miaka mitatu baadae katika mpinduzi ya chama kama yale yaliopita huko nyuma.

Kisa hicho kikichanganywa na suala la chama cha Leba kukiuka ahadi yake ya uchaguzi kwa kuanzisha kodi inayochukiwa mno kwa wachafuzi wakuu wenye kutowa gesi chafu ya hewa ukaa kuliathiri sana nafasi ya Leba kuweza kuchaguliwa tena.

Kilio kikuu ni uchumi

Baada ya kujipatia ushindi Abbott amewaambia wafuasi wake kwamba anasubiri kwa hamu kuunda serikali mpya yenye uwezo,yenye kuaminika na yenye dhamira na uthabiti na kujipanga kutekeleza ahadi zake kwa wananchi wake.

Waziri Mkuu mteule Tony Abbott akitangaza ushindi uchaguzi mkuu wa Australia. (07.09.2013)
Waziri Mkuu mteule Tony Abbott akitangaza ushindi uchaguzi mkuu wa Australia. (07.09.2013)Picha: Getty Images

Abbott ambaye atakuwa waziri mkuu wa tatu wa Australia katika kipindi cha miezi mitatu ijayo atadhamiria kukomesha kipindi kisicho cha kawaida cha kukosekana utulivu wa kisiasa nchini humo.

Kutelekezwa kwa chama cha Leba kunamaanisha kukataliwa kwa vishindo kwa serikali yenye viti vichache bungeni kuwahi kuwepo nchini humo tokea Vita Vikuu vya Pili vya Dunia. Wapiga kura walikuwa wanachukia muafaka na makubaliano yaliofikiwa likiwemo suala la kodi ya gesi ya hewa ukaa kati ya chama cha Leba,chama kidogo cha Kijani na wabunge wa kujitegemea ili kuweza kuidumisha serikali yao ya mseto ilio dhaifu na mara nyengine ya vurugu katika kipindi cha miaka mitatu iliopita.

Sera za serikali mpya

Abbott ameapa kuifuta kodi ya hewa ukaa kuanzia mwezi wa Julai mwaka 2014 ikiwa ni miaka miwili baada ya kuanza kutekelezwa,serikali mpya ya Australia pia imeahidi kupunguza matumizi ya msaada wa kigeni wakati ikielekeza juhudi zake katika kuirudisha bajeti iwe na fedha za ziada.Chama cha Leba kimetumia mabilioni ya dola katika miradi ya kuchochea uchumi ili kuepuka kushuka kwa uchumi wa nchi hiyo. Lakini kupunguwa kwa mapato ya kodi za makampuni kutokana na kuzorota kwa sekta ya madini kumekilazimisha chama cha Leba kuvunja ahadi yake ya kuirudisha bajeti kwenye fedha za ziada katika mwaka wa mwisho wa fedha.

Tony Abbott akibusiwa na mkewe Margaret wakati wa kupiga kura mjini Sydney. (07.09.2013).
Tony Abbott akibusiwa na mkewe Margaret wakati wa kupiga kura mjini Sydney. (07.09.2013).Picha: Reuters

Waziri Mkuu wa zamani wa chama cha Leba Bob Hawke amelaumu kushindwa kwa chama hicho kutokana na kushindwa kwake kuwa na umoja.

Abbott anakabiliwa na changamoto ngumu ya kisiasa kufikiria jinsi ya kuzuwiya ongezeko la watu wanaotafuta hifadhi ambao huwasili nchini Australia kwa kutumia mashua. Waliberali wameahidi kutumika kwa sera mpya zenye kulitaka jeshi la majini la nchi hiyo kuzirudisha boti za wakimbizi zinakotokea Indonesia.Haiko wazi iwapo Abbott ataweza kufanikisha mabadiliko ya sheria bungeni lakini ametishia kuitisha uchaguzi na mapema iwapo baraza la Seneti litakwamisha mabadiliko hayo.

Kwa hiyo haiwezekani kuwepo kwa kipindi cha fungate kwa Abbott wakati akiurithi uchumi unaozorota ulioathiriwa na kudhoofika kwa neema ya sekta ya madini ambayo ililiepuesha taifa hilo lenye utajiri wa rasilmali na kuporomoka kwa uchumi wakati wa msukosuko wa fedha duniani.

Abbot amesema " Katika kipindi cha miaka mitatu, kodi ya hewa ukaa itakuwa imekwenda,mashua zitazuiliwa bajeti itarudi kwenye mkondo wa kuwa na fedha za ziada na njia kuelekea karne ya 21 hatimae zitakuwa tayari."

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP

Mhariri: Amina Abubakar