1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abe apata ushindi wa Kishindo uchaguzi Japan

Sekione Kitojo
22 Oktoba 2017

Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe ameshinda kwa kishindo uchaguzi ulioitishwa kabla ya wakati wake leo Jumapili (22.10.2017),na kumpatia mamlaka yanayoimarisha msimamo wake ambao tayari ni wa vita dhidi ya Korea kaskazini.

https://p.dw.com/p/2mJeV
Japan Wahlen - Shinzo Abe
Picha: Reuters/T. Hanai

Muungano wa  kihafidhina  wa  waziri  mkuu  Abe unaelekea  kupata ushindi  wa  viti 311 katika  bunge  lenye  viti 465 , kwa  mujibu wa matokeo  ya  awali  yaliyochapishwa  na  kituo cha  televisheni  cha binafsi  cha  TBS, na  kumfanya  kiongozi  huyo  wa  Japan  kuwa kiongozi  aliyeshika  madarakani  kwa  muda  mrefu  zaidi  nchini humo.

Japan Parlamentswahlen Shinzo Abe
Waziri mkuu wa Japan Shinzo AbePicha: Reuters/Kim Kyung-Hoon

Ushindi  huo wa  kishindo  bila  shaka  utaweza  kutia  nguvu dhamira  ya  Abe  kupambana  na  hatari  ya  kinyuklia  inayoletwa na  Korea  Kaskazini , wakati mshirika  huyo  muhumi  wa  Marekani katika  kanda  hiyo  akiongeza  mbinyo  dhidi  ya  utawala  wa Pyongyang  baada  ya  kufyatua  makombora  mawili  juu  ya  anga ya  Japan katika  muda  wa  mwezi  mmoja.

Abe  alikuwa  anaelekea  kupata  "ushindi  wa  kishindo," gazeti  la kila  siku  la  Yomiuri  limesema  katika  tovuti  yake.

Mamilioni  ya Wajapan  walijitokeza  kupiga  kura  licha  ya  mvua kubwa  na  upepo  mkali , wakati  kimbunga  kiliposhambulia  taifa hilo  na  wengi  wakipiga kura  zao mapema  baada  ya  kutolewa tahadhari  kutokana  na  kimbunga  hicho.

"Naunga  mkono  msimamo  wa  Abe  katika  kuipa  Korea  kaskazini mbinyo," alisema  mpiga  kura  mmoja, Yoshihisa Lemori, wakati akipiga  kura  yake  huku  mvua  kubwa  ikinyesha  mjini  Tokyo.

Upinzani dhaifu

Chama  cha  waziri  mkuu  Abe  cha  Liberal Democratic , LDP , kimefaidika  kutokana  na  upinzani  uliodhaifu  na  uliogawika, wakati vyama  vikuu  viwili  vilivyokuwa  vikipambana  nae  vikiwa vimeundwa  wiki  kadhaa  tu  zilizopita.

Japan Wahlen zum Unterhaus Wahlkampagne
Kiongozi wa chama cha Upinzani cha Hope Yuriko KoikePicha: picture-alliance/AP/Yomiuri Shimbun/M. Inagaki

Uungwaji  mkono  kwa  chama  cha  Matumaini , Hope  kilichoasisiwa na  gavana  maarufu  wa  mjini  Tokyo Yuriko Koike uliyeyuka  baada ya  kupata  nguvu  kubwa  mwanzoni  na  kilikuwa  kikielekea kushinda kiasi  ya  viti  50  bungeni, matokeo  yaliyotolewa  na televisheni  ya  TBS yameonesha.

Akizungumza  kutoka  mjini  Paris ambako  alikuwa  akihudhuria  tukio fulani  akiwa  kama  kiongozi wa  mji  mkubwa  duniani, Koike aliliambia  shirika  la  habari  la  NHK kwamba  anahofia , "matokeo mabaya  sana".

Chama  kipya  cha  siasa  za  wastani  za  mrengo  wa  kushoto cha Constitutional Democratic kimepata  matokeo  kidogo  mazuri  kuliko ilivyotarajiwa  lakini  hata  hivyo  kiko  nyuma  sana  ya  Abe.

"Ushindi  wa  chama  cha  LDP ni  kutokana  na  upande  wa upinzani  kutoweza  kuunda  umoja," mtaalamu  wa  masuala  ya kisiasa  Mikitaka Maysuyama   kutoka  taasisi  ya   taifa  ya  mitaala ya  stadi  za  sera , ameliambia  shirika  la  habari la  AFP.

Haijafahamika  mara  moja  baada  ya  uchaguzi  huo iwapo muungano  wa  vyama  vinavyomuunga  mkono  Abe  utabaki  na wingi  wake  wa  theluthi  mbili."

Japan Wahlen
Mpiga kura akiweka kura yake katika sanduku la kura chinini Japan Picha: picture-alliance/AP Photo/E.Hoshiko

Wingi  wa  aina  hiyo utamruhusu Abe kupendekeza  mabadiliko katika  katiba ya  Japan  iliyowekwa  na  Marekani  ambayo inayalazimisha  majeshi  yake "kukataa  vita" na  kuyaweka  majeshi yake  kuwa  ni  ya  kujilinda  tu.

Muda  mfupi  wa  kampeni  wa  siku  mbili ulitawaliwa  na  masuala ya  uchumi  na  mzozo  wa  kimataifa   kuhusiana  na  Korea Kaskazini , ambayo  imetishia  "kuizamisha "Japan ndani  ya  bahari.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe

Mhariri: Yusra Buwayhid