1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abiria 155 wanusuruka kifo kufuatia ajali ya ndege Marekani.

Jane Nyingi/ AFPE16 Januari 2009

Katika tukio la kimiujiza ndege ya abiria ya shirika la ndege la marekani imetua katika mto Hudson mjini Newyork na abiria wote 155 wamenusurika.

https://p.dw.com/p/GZi0

Rubani wa ndege hiyo anatajwa kuwa shujaa,kwa ujasiri wake wa kutua ghalfa na bila matatizo yeyote ,mtoni, baada ya injini zote mbili kushindwa kufanya kazi.

Ndege hiyo ambayo ililazimika kutua ghafla punde baada ya kupaa , ilikuwa inasafiri kutoka uwanja wa ndege wa La Guarda mjini Newyork kwenda Charlotte, Carolina ya kaskazini. Kwa mujibu wa ripoti za halmashauri ya wanja za ndege mjini humo injini zote mbili za ndege hiyo zilidinda kufanya kazi baada ya kugonga kundi la ndege.

Vyombo vya ulinzi wa pwani ya Marekani pamoja na wenzao wa kuzima moto waliwasili katika eneo la tukio kwa haraka ili kusadia katika shughuli za ukoaji.Baadhi ya abiria walikuwa wamekwama kwenye mkia wa ndege hiyo huku wengine wakielea katika mto Hudson.

Kutokana na wasiwasi baadhi yao pia walikuwa wamepanda juu ya mkia wa ndege hiyo ili kutafuta usadizi wa aina yeyote.Maafisa wa ulinzi wa pwani ya marekani wanasema abiria waliokuwa wakielea mtoni wangeweza kufanya hivyo kwa kati ya dakika tano hadi kumi.

"Katika muda wa dakika chache tusikilia mlio mkubwa, na ndege kutingika kidogo. kisha baadaye moshi mdogo ukajitokeza ulionekana kama unatokana na moto.Na moja kwa moja ndege ikabadili mwendo na rubani hangeweza kuidhibiti tena,tuligundua kuna kitu kibaya kilichokuwa kikiendelea."

Rubani wa ndege hiyo Chesley Sullenberger ameendelea kupongezwa kutokana na kufanikiwa kuiwezesha ndege itue ghalfa bila kusababisha maafa yeyote.Hata hivyo mmoja wa abiria alivunjika miguu yote miwili,huku madaktari wakiwatibu abiria 78 kutokana na majeraha madogo madogo abiria, hao wengine waliondoka bila majeraha.

"Inaonekana rubani alifanya ujasiri kwa kuiwezesha ndege hiyo itue mtoni na kuhakikisha kila mtu anatoka nje".

Wachunguzi wa ajali za anga nchini Marekani tayari wamewasili mjini Newyork kuchunguza kilichosababisha ajali hiyo japokuwa swala la ugaidi limefutiliwa mbali.

Rais wa marekani George Bush pia alimsifu rubani huyo na kusema ujasiri wake umesadia kutosababisha maafa yeyote ya abiria walikuwa ameabiri ndege hiyo ya AirBus 320

Rubani wa ndege hiyo amekuwa katika taaluma hiyo kwa zaidi ya miaka 40 na pia anamiliki kampuni ya kutoa ushauri kuhusu usalama wa usafiri.Rubani Sullenberger pia ni mwenyekiti wa chama kimoja kikuu cha marubani nchini Marekani.

Ajali hii inatokea miaka 27 baada ya ndege nyingine ya Florida boeing 737-222 kuanguka katika mto Potomac mjini Washington januari 13 mwaka 1982,abiria 78 walifariki.