1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abiy Ahmed aapishwa kwa muhula mpya kuongoza Ethiopia

Sylvia Mwehozi
4 Oktoba 2021

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameapishwa kwa muhula mpya wa miaka mitano, lakini hatua hiyo inahatarishwa kudhoofishwa na kuongezeka kwa vita katika mkoa wa kaskazini wa Tigray. 

https://p.dw.com/p/41E9i
 Äthiopien Neuer Ministerpräsident Abiy Ahmed Ali Kombobild AM

Chama cha waziri mkuu Abiy cha Prosperity kilipata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa bunge mapema mwaka huu katika kura ambayo ilikosolewa na wakati huo huo pia kupingwa na vyama vya upinzani lakini ikielezewa na waangalizi wa nje kuwa bora kuliko chaguzi zilizopita. 

"Mimi, Abiy Ahmed Ali, leo katika baraza la wawakilishi la wananchi, ninakubali kuteuliwa kuwa waziri mkuu, na ninaahidi kuchukua majukumu na kuwa mwaminifu kwa katiba na majukumu niliyopewa na wananchi", alisema Abiy wakati akiapishwa na jaji mkuu Meaza Ashenati. Ni wakuu watatu wa nchi wa Afrika waliohudhuria hafla ya kuapishwa kwa Abiy kutoka Nigeria, Senegal na nchi jirani ya Somalia.

Wakati wapiga kura waliposhiriki uchaguzi wa bunge, maelfu wengine wameuawa katika mzozo unaoendelea kwenye mkoa wa kaskazini wa Tigray na maelfu wengine wanakabiliwa na hali inayokaribia kuwa baa la njaa, kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa. Mzozo huo umeutia dosari utawala wa Abiy ambaye ni mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka 2019 aliyopatiwa kwa juhudi zake za kurejesha uhusiano na nchi jirani ya Eritrea pamoja na mageuzi ya kisiasa.

Äthiopien Mekele | Pro-TPLF Rebellen
Waasi wa kundi la TPLF mkoani TigrayPicha: YASUYOSHI CHIBA/AFP

Haijawa wazi ikiwa kuapishwa kwa Abiy kutabadili mwelekeo wa vita baina ya vikosi vya serikali na waasi wa kundi la TPLF, ambalo lilikuwa likidhibiti madaraka kabla ya Abiy aingie madarakani. Mgogoro huo uliodumu kwa miezi 11 unadhoofisha uchumi wa Ethiopia, moja ya nchi ambayo uchumi wake ulikuwa ukikua kwa kasi barani afrika na ukitishia pia kumtenga Abiy ambaye wakati mmoja alionekana kama mpatanishi wa amani wa kikanda. Mgogoro huo sasa umeenea katika mikoa ya jirani ya Afar na Amhara.

Wiki iliyopita, serikali ya Ethiopia ilikabiliwa na ukosoaji kutoka Marekani na nchi kadhaa za Umoja wa Ulaya baada ya kuwatimua maafisa saba wa Umoja wa Mataifa iliowatuhumu kwa kuunga mkono vikosi vya Tigray. Serikali inakabiliwa na shinikizo kubwa wakati raia wakianza kukabiliwa na kitisho cha njaa huko Tigray katika kile kilichoelezewa na Umoja wa Mataifa kuwa "mzingiro wa kibinadamu". Marekani imetishia vikwazo zaidi kama upelekaji misaada ya kiutu mkoani Tigray utaendelea kuzuiwa na ikiwa pande zote katika mzozo huo hazitochukua hatua kuelekea amani.