1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Adama Barrow atangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais Gambia

Saleh Mwanamilongo
6 Desemba 2021

Maelfu ya wafuasi wa Barrow walisherehekea ushindi huo kwenye mitaa ya Mji Mkuu Banjul,ingawa wapinzani wake walipinga matokeo yaliyotangazwa Jumapili jioni.

https://p.dw.com/p/43spB
Gambia Präsident Adama Barrow | Amtsübernahme & Einweihungszeremonie in Bakau
Picha: Reuters/T. Gouegnon

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Alieu Momarr Njai alimtangaza Barrow kuwa mshindi, katika matokeo ya mwisho saa chache baada ya wagombea wa upinzani kupinga matokeo ya awali yaliyompa Barrow nafasi ya kuongoza.

Barrow alishangiliwa na umati wa wafuasi wake alipohutubia kwa hali ya furaha na unyenyekevu mkubwa na kuwataka wafuasi wake kuwaheshimu waliowapigia kura wapinzani wake katika uchaguzi aliouita kuwa huru, wa haki na wa uwazi.

"Ninawaomba wafuasi wangu wote kusherehekea ushindi kwa njia ya amani. Tunakumbushwa kwamba waliotaka kuunga mkono wagombea wengine ni Wagambia na haki yao ya kufanya hivyo lazima iheshimiwe daima.",alisema Barrow.

Barrow apata ushindi mpana

Barrow, ambaye kuchukua kiti cha urais miaka mitano iliyopita kulimaliza zaidi ya miaka 20 ya udikteta, alipata zaidi ya asilimia 53 ya kura, kulingana na matokeo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi. Mpinzani wake mkuu Ousainou Darboe alishika nafasi ya pili na asilimia 27.7.

Rais Adama Barrow akishangiliwa na wafuasi wake mjini Banjul
Rais Adama Barrow akishangiliwa na wafuasi wake mjini BanjulPicha: Sally Hayden/SOPA Images/ZUMA Press Wire/Zumapress/picture alliance

Uchaguzi wa Jumamosi, wa kwanza tangu dikteta wa zamani Yahya Jammeh kukimbilia uhamishoni, unaonekana kuwa muhimu kwa demokrasia changa ya Afrika Magharibi.

Kabla ya matokeo kamili kutangazwa, wapinzani watatu wa Barrow walikuwa wamepinga matokeo ambayo yalimpa uongozi wa mapema.

''Hatua yoyote iko mezani''

Mgombea wa upinzani nchini Gambia Ousainou Darboe wa chama cha UDP
Kiongozi wa upinzani nchini Gambia Ousainou Darboe wa chama cha UDP Picha: Getty Images/AFP/Seyllou

Kwenye taarifa ya pamoja mpinzani mkuu Darboe na wagombea wengine wawili walisema wamekataa matokeo yaliyotangazwa na hatua yoyote iko mezani kuchukuliwa.

Wananchi wa Gambia walimiminika kwenye vituo vya kupigia kura Jumamosi kuchagua ni nani angeongoza nchi yao,ndogo zaidi barani Afrika ,kwa miaka mitano ijayo, na waliojitokeza kufikia asilimia 87, kulingana na matokeo rasmi.

Jumuiya ya Ecowas yapongeza uchaguzi

Mapema Jumapili, Ernest Bai Koroma, mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), alitoa wito kwa wagombea wote "kukubali matokeo ya uchaguzi kwa nia njema. Akisema hakutakuwa na mshindi au aliyeshindwa, bali mshindi mmoja tu, raia wa Gambia.

Uchaguzi huo unatazamwa kwa karibu kama mtihani wa mabadiliko ya kidemokrasia nchini Gambia, ambapo Jammeh alitawala kwa miaka 22 baada ya kutwaa madaraka katika mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu mwaka 1994.