1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Addis Ababa. Mengistu ahukumiwa bila kuwapo.

13 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCjq

Mahakama kuu nchini Ethiopia imehukumu bila kuwapo dikteta wa zamani Mengistu Haile Mariam kwa mauaji ya halaiki pamoja na makosa mengine.

Mengistu , ambaye hivi sasa anaishi nchini Zimbabwe, amehukumiwa kwa uhalifu aliofanya wakati wa utawala wake wa Kimax kutoka mwaka 1974 hadi 1991.

Wakati wa kipindi kinachojulikana kama cha kitisho, mwaka 1977, maelfu ya watu waliuwawa ama kupotea wakati kanali huyo wa zamani alipojaribu kuigeuza Ethiopia kuwa taifa la wafanyakazi linalofuata misingi ya Urusi. Kesi hiyo mjini Addis Ababa imechukua muda wa miaka 12. Ni watuhumiwa 34 tu kati ya 106 waliokuwapo mahakamani. Mengistu aliondolewa madarakani mwaka 1991 na waziri mkuu wa sasa wa Ethiopia Meles Zenawi. Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe ameahidi kutomrejesha Mengistu wakati wote akiwa hajihusishi na shughuli za kisiasa.