1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ADDIS ABABA: Mkutano wa Umoja wa Afrika wafanyika leo

29 Januari 2007
https://p.dw.com/p/CCWo

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika umeanza leo mjini Addis Ababa Ethiopia. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon anahudhuria mkutano huo huku akijiandaa kufanya mazungumzo na Sudan juu ya ukiukaji wa haki za binadamu katika jimbo al Darfur.

Ombi la Sudan kutaka kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Afrika linapingwa na baadhi ya wanachama 53 wa umoja huo. Shirika la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, linasema Umoja wa Afrika utajiharibia sifa na kujiweka katika hali ya kutoaminiwa ikiwa utaichagua Sudan kuwa mwenyekiti wake.

Serikali ya rais Omar el Bashir inapinga madai kwamba inawasaidia wanamgambo wa Janjaweed wanaolaumiwa kwa ubakaji, mauaji na mashambulio ya miaka minne katika eneo la Darfur na haitaki kuwaruhusu wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kujiunga na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Afrika.

Watu takriban laki mbili wameuwawa na wengine milioni 2.5 kulazimika kuyahama makazi yao, tangu vita vilipoanza kwenye jimbo la Darfur mnamo mwaka wa 2003.