1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFCON: Cameroon na Cote D'Ivoire katika tathmini

20 Januari 2015

Cote D'Ivoire inaingia dimbani muda mfupi ujao kupambana na Guinea, wakati Cameroon Simba wa Nyika inawasubiri Mali mjini Malabo katika kinyang'anyiro cha kuwania ubingwa wa mataifa ya Afrika nchini Guinea ya Ikweta.

https://p.dw.com/p/1ENMe
Elfenbeinküste Fußball Nationalmannschaft
Kikosi cha Tembo wa Cote D'IvoirePicha: I. Sanogo/AFP/Getty Images

Jinamizi la fainali za kombe la dunia lililoikumba Cameroon anasema kocha Mjerumani Volker Finke ni jambo lililopita na kikosi chake kiko tayari kuanza kampeni ya kombe hili.

Licha ya kwamba Didier Drogba hayuko tena katika kikosi cha Tembo wa Cote D'Ivoire lakini mzuka wake unaweza kunyemelea kambi ya tembo hao wakati kikosi cha Cote D'Ivoire kitakapoingia dimbani kupambana na Guinea katika ufunguzi wa michezo ya kundi D.

Mali Fußball Nationalmannschaft
timu ya taifa ya MaliPicha: H. Kouyate/AFP/Getty Images

Kustaafu kwa nyota huyo katika jukwaa la kimataifa la soka kumeingiliana na matokeo mabaya ya Cote D'Ivoire, ambayo haikuweza kuonesha umahiri wake katika michuano ya kufuzu kucheza fainali hizi na kuingia tu katika mashindano haya ya mwaka 2015 kibahati bahati.

Hata kuwapo kwa nyota mwingine Yaya Toure hakukuweza kuondoa hali ya kuyumba yumba iliyojitokeza tangu fainali za kombe la dunia wakati wakipita katika michezo ya kufuzu pamoja na michezo ya maandalizi ya kabla ya mashindano haya.

Kamerun Fußball Nationalmannschaft
Simba Wanyika CameroonPicha: P.-P. Marcou/AFP/Getty Images

Mwanzo utakaofanyiwa tathmini

Wanakabiliwa na mwanzo wenye utata katika michuano hii dhidi ya Guinea katika uwanja wa Nuevo Estadio de Malabo katika mji mkuu wa Guinea ya Ikweta katika mchezo wa kundi D leo jioni.

Mchezo huo utafuatiwa na mchezo mwingine utakaokuwa pia uchunguzi wa baada ya fainali za kombe la dunia , ambapo , mara hii Cameroon , ambayo imeonesha mshangao pamoja na kufufuka kwa haraka baada ya muda wa kutisha nchini Brazil.

Fußball WM 2014 Brasilien - Kamerun
Maafa yaliyowakumba cameroon nchini Brazil, hapa Brazil ikicheza na cameroonPicha: picture-alliance/dpa

Ni kiasi gani Simba hao wanyika wamebadilika tangu kupigwa kumbo katika fainali za kombe la dunia katika duru ya makundi, kwa kufungwa michezo yote mitatu na kujidhalilisha katika mgomo wao kuhusu fedha , kikosi hicho kinakuwa chini ya uchunguzi wakati watakapocheza mchezo wao wa kwanza leo usiku dhidi ya Mali.

Hata hivyo kocha wa Simba hao wa Nyika, Mjerumani Volker Finke amesema maafsa yaliyokikumba kikosi chake katika kampeni ya kombe la dunia ni jambo lililopita na wako tayari sasa kuanza kampeni mpya katika kombe hili la mataifa ya Afrika.

FIFA WM 2014 Kamerun vs Kroatien 18.06.2014
Wachezaji wa Cameroon wakipigana makonde uwanjani katika kombe la duniaPicha: Reuters

"Nafikiri hisia na jinsi ya kufikiri vimebadilika. Miezi miwili ama mitatu iliyopita imekuwa ya utulivu na ya faragha," amesema Mjerumani huyo, ambaye aliwashangaza watu wengi kwa kuendelea kuifunza timu hiyo baada ya kombe la dunia.

Jana katika michuano ya kundi C, Algeria iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Afrika kusini na Senegal ikaishinda Ghana kwa mabao 2-1. Mzunguko wa pili unaanza kesho kwa timu za kundi A kupambana , ambapo katika uwanja wa Bata wenyeji Guinea ya Ikweta itapambana na Burkina Faso na baadaye Gabon itakwaana na Jamhuri ya Congo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Idd Ssessanga