1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan: Mkakati usio na maelezo

Mohammed Abdulrahman
23 Agosti 2017

Afghanistan ndiyo vita vya muda mrefu vya Marekani. Rais Donald Trump anataka  kuviendeleza, lakini katika hotuba yake ya hivi karibuni, ameshindwa kufafanua vitaendelea kwa muda gani na nini hatima ya vita hivyo.

https://p.dw.com/p/2igHQ
USA Präsident Donald Trump in Phoenix
Rais wa Marekani Donald Trump, akihutubia mjini PhoenixPicha: Reuters/A. Brandon

Kilicho kipya ni kauli ya Trump tu kwamba  " Sisi sio tena wajenzi wa taifa. Tunawauwa magaidi." Kwa  kauli hiyo amejitenga na  matamshi  ya  watungaji sera wengi wa magharibi.  Wakati wote Marais wa zamani Barack Obama na George W.Bush walikuwa  wakizijumuisha sera zao za kijeshi pamoja na  masuala ya demokrasia na  haki za binaadamu kukikosekana suluhisho la  kisiasa. Hivi sasa  Trump pia  haonekani kuzingatia suluhisho la kisiasa.

Katika hotuba yake Trump aliweka wazi kwamba kujiingiza Afghanistan ni  suala la maslahi kwa Marekani. Alitaja juu ya matatizo yaliyopo ambayo yatatatuliwa kwa sababu yeye ni mfumbuzi wa matatizo. Akisema, " Mwishoe,  tutashinda." Alijiepusha kuzungumzia njia ya kisiasa, akisisitiza tu kwamba "majeshi yetu yatapigana ili kupata ushindi."

Trump alisema kwamba kuanzia sasa ushindi utamaanisha wazi kabisa kwamba ni kuwashambulia maadui, kulikandamiza kundi linalojiita dola la kiislamu - ISIS. Kulivuruga kundi la Al Qaeda na kuwazuwia Wataliban kutwaa madaraka Afghanistan pamoja na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Marekani kabla hayatatokea. Bila shaka atakuwa na kibarua kizito. Swali ni jee kitatokea nini wakati wanajeshi wa marekani watakapokuwa wakirudishwa nyumbani kwenye majeneza?

Nyongeza ya ndege zisizo na rubani

Afghanistan US-Drone MQ-9 Reaper
Ndege inayorushwa bila ya rubani nchini AfghanistanPicha: picture-alliance/AP Photo/US Air Force/Lt. Col. Leslie Pratt

Mkakati wa Trump kuhusu Afghanistan unamaanisha kuweko kwa ndege zaidi zisizokuwa na rubani-drones, mashambulizi zaidi ya anga na mapigano zaidi. Zaidi ya yote vita na vifo zaidi. Chini ya uongozi wa Trump Marekani imerudi tena vitani uamuzi ambao bila shaka haitawapendeza washirika wake katika Jumuiya kujihami ya NATO. Matamshi makali aliyoyatoa dhidi ya Pakistan pia si jambo jipya. Trump alisema, "hatuwezi kubakia kimya kuhusu Pakistan kuwa mahala salama kwa makundi ya kigaidi - Taliban na wengine na ambayo ni kitisho kwa kanda hiyo na nje ya eneo hilo. Miaka ya nyuma kulisikika kauli za aina hiyo kutoka kwa Obama, Clinton, Cheney na Rumsfeld juu ya tabia ya Pakistan ya undumila kuwili, lakini pamoja na hayo hakuna kiliochobadilika.

Hivi sasa kama ilivyokuwa katika kipindi cha miaka 16 ya kujiingiza Marekani nchini Afghanistan, uwanja wa mapigano umewahusisha wengi wenye masilahi yao. Hapa si Pakistan pekee inayohusika bali pia India, Iran, Urusi, China na Saudi Arabia. Kila moja inatafuta mshirika nchini Afghanistan na ushirika huo hubadilika kwa kuzingatia mtu atanufaika vipi na kutoka kwa nani. Hatua ya mmoja huwa pigo kwa mwengine na kwa miongo kadhaa hali hiyo imechangia katika vita vya kiitikadi na kijeshi nchini Afghanistan.

Afghanistan haina serikali yenye umoja badala yake imegawika chini ya uongozi wa rais Ashraf Ghani na Wazri mkuu mtendaji Abdullah Abdullah. Makamu wa rais Abdul Rashid Dostum amekimbilia Uturuki kuepuka uchunguzi juu ya madai ya kutekwa nyara wapinzani wake wa kisiasa na ubakaji.

Trump anapaswa kutambua kwamba ushindi Afghanistan si jambo rahisi. Utawezekana tu kwa mazungumzo magumu. Hii ndiyo hali halisi hii leo. Kimsingi hakuna mkakati mpya  bali ni muendelezo wa vita visivyokuwa na mshindi. Wakati wote ugaidi na vitisho vimechukua nafasi kujaza pengo la kisiasa.

Mwandishi:  Mohammed Abdul-Rahman /Sandra Petersmann-DW

Mhariri: Josephat Charo