1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afghanistan yawaachia wafungwa 900 wa Taliban

Daniel Gakuba
27 Mei 2020

Serikali ya Afghanistan imewaachia mamia ya wafungwa wa Taliban, kama ishara ya nia njema kufuatia uamuzi wa Taliban kusitisha mapigano wakati wa sikukuu ya Eid el-Fitr. Taliban imesema itarudisha fadhila hiyo.

https://p.dw.com/p/3coTl
Afghanistan - Bagram Gefängnis in Parwan
Picha: picture-alliance/AP/R. Gul

Kulingana na ripoti ya serikali mjini Kabul, jumla ya wafungwa 900 wa Taliban wameachiwa huru kutoka magereza mbali mbali nchini humo, sambamba na tukio la kihistoria la usitishwaji wa mapigano uliopendekezwa na wanamgambo wa Taliban, kuadhimisha sikukuu ya Waislamu ya Eid el-Fitr.

Wafungwa 600 waliachiwa kutoka gereza la wahalifu sugu la Bagram karibu na mji mkuu, Kabul, ambako bado Marekani ina kambi kubwa ya kijeshi.

Serikali ya Afghanistan ilikuwa imeahidi kuwaachia huru wataliban 2000, kama jibu lake kwa uamuzi wa Wataliban kutangaza ahueni ya vita kwa muda wa siku kusherehekea kumalizika kwa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Muda huo ulimalizika jana, lakini imekuwepo miito kuwataka wanamgambo hao kuurefusha, na msemaji wao amelithibitishia shirika la habari la Associated Press kuwa walikuwa wakilitafakari suala hilo.

Tukio la kihistoria

Afghanistan Befreiung Taliban Gefangene in der Provinz Parwan
Wafungwa walioachiwa wakisafirishwa kwenda mjini KabulPicha: picture-alliance/AP Photo/R. Gul

Hii ni mara ya pili pekee ambapo Taliban na serikali ya Kabul wamekubaliana kusitisha mapigano, katika muda wa miaka 19 ya vita baina yao.

Mmoja wa wafungwa walioachiwa, Abdul Wasi kutoka jimbo la Kandahar, aliliambia shirika la habari la AFP mara tu baada ya kutoka gerezani, kuwa alikuwa mpiganaji wa kijihadi.

''Niliambiwa kupigana vita vitakatifu hadi pale askari wote wa kigeni watakapokuwa wamefurushwa kutoka nchi yetu,'' alisema Wasi mwenye umri wa miaka 27, ambaye amesota jela kwa miaka minane.

Aliongeza kuwa anafurahia makubaliano yaliyofikiwa baina ya kundi la Taliban na Marekani, ambayo yanasafisha njia ya vikosi vyote vya kigeni kuondoka Afghanistan ifikapo Mei mwaka ujao.

''Wanajeshi wa kigeni wakiondoka, hatutapigana tena.'' Alimalizia Wasi alipokuwa akipanda basi lilimpeleka mjini Kabul pamoja na wataliban wengine walioachiwa.

Wataliban kulipa wema kwa wema

Afghanistan bei Kabul | Bagram-Gefängnis, Freilassung von Taliban
Wengi wa wafungwa walioachiwa walikuwa katika gereza la BagramPicha: Reuters/M. Ismail

Uongozi wa Taliban umekaribishwa hatua hiyo ya serikali ya kuwaachia wafungwa wao. Msemaji wa kundi hilo Suhail Shaheen aliandika katika mtandao wake wa Twitter, kuwa kuachiwa kwa wenzao 900 ilikuwa ishara ya maendeleo mema, na kuongeza kuwa kundo lake pia litarudisha fadhila hiyo kwa kuwaachia wafungwa wengi wa upande wa serikali.

Msemaji wa Baraza la Usalama wa Taifa mjini Kabul Javid Faisal amewatolea wito wataliban kurefusha muda wa usitishwaji wa mapigano, ili mazungumzo yaliyocheleweshwa baina ya serikali na kundi hilo la wanamgambo yaweze kuanza.

Amesema kuwa ikiwa Wataliban wataitikia wito huo, serikali pia itaendeleza usitishaji wa mapigano.

Mazungumzo kati ya pande hizo yalitarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 10 Machi lakini haikuwezekana, na fursa hii ya kusitisha uhasama na kubadilishana wafungwa inaleta matumaini ya muafaka wa kuyafufua.

 

APE, AFPE