1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika haina silaha za nuklia

2 Septemba 2009

Afrika,bara la pili kwa ukubwa baada ya Asia,inabeba bendera ya zoni ya nchi 53 zilizojitakasa na silaha za kinuklea-zoni yenye jumla ya wakaazi bilioni moja.

https://p.dw.com/p/JNfe
Nembo ya shirika la Atomiki IAEA

Hali hii inamaanisha mojawapo ya maeneo tajiri kabisa kwa maadini ya Uranium limetakasika na silaha za kinuklea.

Shirika la kimataifa la nguvu za atomiki,IAEA na Umoja wa Afrika,wametangaza kati kati ya mwezi Agosti kwamba,mkataba wa kuligeuza bara la Afrika liwe bara lililosafika kwa silaha nuklea-NWFZ umeanza kufanya kazi.

Burundi Flagge
Bendera ya Burundi

Hali hiyo imewezekana baada ya Burundi kuwa taifa la 28 kuidhinisha mkataba huo July 15 mwaka huu.Algeria na Burkina Fasso zilikua nchi za kwanza za kiafrika kuidhinisha mkataba huo mnamo mwaka 1998-miaka miwili baada ya mkataba huo kutiwa saini.

Eneo la kusini la dunia limetakata

Hali hii imejiri huku ripoti zikihanikiza kuhusu harakati zilizokithiri za makampuni yanayoungwa mkono na nchi za Ulaya na China za kuchimba maadini ya Uranium barani Afrika.Kwa hivyo limepatikana hakikisho hivi sasa kwamba eneo la kusini la dunia limetakasika na silaha za kinuklea.

Mkataba huo unazitaka pande zote ziheshimu makubaliano yaliyofikiwa pamoja na shirika la kimataifa la nguvu za atomiki-IAEA.Makubaliano hayo yanaalingana na yale ya mkataba wa kutosaambaza silaha za kinuklea-NPT.

Afrika i salama

Mkataba huo pia unazitaka pande zote zihakikishe usalama wa zana zake za kinuklea,mitambo na vifaa,zizuwie visiibiwe au kuingia mikononi mwa watu kinyume na sheria pamoja pia na kuhakikisha hakuna hujuma zozote zitakazofanyika dhidi ya vituo vya kinuklea katika eneo husika.

Mkataba huo unaitambua Afrika kuwa ni zoni iliyotakasika na asilaha za kinuklea.Mkataba huo umeandaliwa mijini Johannesburg na Pelindaba mwezi June mwaka 1995 na kutiwa saini mjini Cairo April 11 mwaka 1996.

Mkataba huo unajulikana pia kama "Mkataba wa Palindaba" kutokana na kituo cha utafiti wa kinuklia cha Palindaba,magharibi ya Pretoria nchini Afrika kusini.Kituo cha Palindaba ni kituo kikuu cha utafiti wa kinuklea nchini Afrika kusini,ambacho kinasimamiwa na shirika la nishati ya kinuklea ya Afrika kusini.Huko ndiko mabomu ya kinuklea ya Afrika kusini yalikokua yakitengenezwa na kuhifadhiwa katika miaka ya 70.

"Kuanzishwa zoni huru kwa silaha za kiafrika barani Afrika-NWFZ,sawa na na zoni nyengine kama hizo katika eneo la Latin Amerika,na Caribean,Kusini Mashariki ya asia,Eneo la Pacifik ya kusini na Asia ya kati,ni hatua muhimu katika kuleta hali ya kuaminiana na kuimarisha usalama wa kimkoa,na itachangia katika juhudi za kuikomboa dunia toka silaha za kinuklea" amesema hayo mkurugenzi mkuu wa shirika la kimataifa la nguvu za Atomoki-IAEA,Mohammed El Baradei.

Atomenergiebehörde Direktorium El Baradei
Kiongozi wa IAEA Mohamed ElBaradeiPicha: picture-alliance /dpa

Amesema shirika la IAEA linaunga mkono sayansi ya kinuklea na teknolojia vitumike kwa masilahi ya amani..Mkurugenzi mkuu wa shirika la IAEA ameongeza kusema tunanukuu:"Anaamini matumizi ya teknolojia hiyo ya kinuklea barani Afrika yatasaidia kuimarisha shughuli za kiuchumi na maendeleo ya jamii barani Afrika.

Utaratibu wa kutaka kulitakasa bara la Afrika na silaha za kinuklea ulianza tangu mwaka 1964,pale viongozi wa taifa na serikali wa Umoja wa zamani wa Afrika walipokutana mjini Cairo.

Mwandishi:Oummilkheir Hamidou/IPS

Mhariri:M.Abdul-Rahman