1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika ina fursa nuri kabisa katika mkutano wake wa hali ya hewa

27 Agosti 2008

Afrika ina fursa nzuri kabisa katika mazungumzo ya Umoja wa Mataifa juu ya hali hewa kuhakikisha kwamba bara hilo maskini kabisa duniani linapatiwa msaada wa kubaliana na ongezeko la kiwango cha joto duniani.

https://p.dw.com/p/F5zM

Inaelezwa kwamba Afrika bado iko nyuma katika suala la kuvutia uwekezaji wa teknolojia zenye kuzingatia utunzaji wa mazingira.

Mkutano wa Umoja wa Mataifa juu ya hali ya hewa unahudhuriwa na mataifa 160 umeanza mjini Accra Ghana tarehe 21 mwezi huu wa Augusti na kumalizika leo tarahe 27.

Mkuu wa Sekreteriat ya Umoja wa Mataifa ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa Yvo de Boer amesema Afrika bado ingali iko nyuma katika suala la kuvutia uwekezaji wa teknolojia zenye kutunza mazingira ili kupunguza ongezeko la gesi zenye kuathiri mazingira na katika kupata msaada kujirekebisha na athari za ukame, mafuriko,kupanda kwa bahari na mvua zisizotabirika.

Akizungumza katika mkutano huo wa hali ya hewa mjini Accra Ghana de Boer ameyahimiza mataifa ya Afrika kusisitiza maslahi yao kuhusiana na mkataba mpya wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa ambao unatazamiwa kufikiwa mwishoni mwa mwaka 2009 mjini Copenhagen Danmark.

Amesema kwa kweli amejaribu kusisitiza kwamba mchakato huo utakaohitimishwa Copenhagen ni fursa nzuri kabisa kwa nchi za Afrika kuhakikisha kwamba mkataba ujao unakidhi mahitaji yao katika njia bora zaidi.

de Boer anasema mataifa ya Afrika yanahitaji kuunda kile ambacho ni muhimu kwao kukichukulia hatua katika mambo yote mawili ya kupunguza utowaji wa gesi zenye kuathiri mazingira na kujirekebisha kwa kwenda na hali ya taathira ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Ameitaka Afrika ielewe kile inachokipendelea.

Cave Zaahidi mratibu wa hali ya hewa wa shirika la mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP alihudhuria mkutano huo na kuzinduwa repoti ya shirika hilo ambapo amesema ruzuku nyingi za nishati mara nyingi huzinufaisha kampuni na wale wenye kutowa zana badala ya waatu maskini katika jamii na baadhi ya ruzuku hizo huenda hata zisiwafikie maskini.

Mataifa ya Afrika ni miongoni mwa yale ambayo hajajachukuwa hatua kubwa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanalaumiwa kusababishwa kwa kiasi kikubwa na gesi za matumizi ya nishati tokea kufikiwa kwa maendeleo makubwa ya viwanda ambayo hujulikana kama Mapinduzi ya Viwanda licha ya bara hilo kuwa miongoni mwa mabara yalio rahisi kabisa kuathirika na mabadiliko ya hali ya hewa.

China,India na Brazil zimevutia uwekezaji zaidi kuliko Afrika chini ya mradi wa Umoja wa Mataifa ambao unaziwezesha nchi za kitajiri kuwekeza katika miradi ya ulimwengu wa nchi zinazoendelea kupunguza utowaji wa gesi zenye kuathiri mazingira miradi kama vile ya mashamba ya kuzalisha umeme kwa kutumia nguvu za upepo au kutokomeza gezi za viwandani.

Afrika inatajwa kuwa bado kufaidika na mipango hiyo ilioko hivi sasa.

Hata hivyo repoti nyengine ya Umoja wa Mataifa iliotolewa mapema wiki hii imesema mammbo yumkini yakawa yameanza kubadilika kwamba miradi safi ya nishati imekuwa ikijitokeza katika nchi kama vile Msumbiji Mali,Madagascar na Kenya.

Mkutano huu wa Accra umepiga hatua ya maendeleo katika kufafanuwa jinsi ya kusaidia kupunguza ukataji misitu ya maeneo ya joto ambacho ni chanzo cha takriban asilimia 20 gesi zenye kuathiri mazingira kutokana na harakati za binaadamu

Zaahidi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira UNEP pia amesema kufanyia mageuzi ruzuku za nishati kwa mara nyengine ni fursa ilio wazi kwa nchi kuchangia zaidi kwa agenda ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Nchi katika mkutano huo wa Accra zimefikia maelewano mazuri juu ya namna zinavyotaka kukabiliana na ukataji wa misitu na kuwazawadia watu kwa utunzaji wa misitu.

Repoti ya Jopo la Umoja wa Mataifa mwaka jana inakadiria kwamba hadi watu milioni 250 barani Afrika watakuwa wanaishi katika maeneo yenye shida ya usambazaji wa maji.