1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani Wiki hii

25 Julai 2014

Ziara ya siku 3 ya rais wa Ufaransa Afrika Magharibi,matumaini ya kupatikana amani katika jamhuri ya Afrika Kati na mkataba wa kibiashara kati ya halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya na mataifa 6 ya kusini mwa Afrika

https://p.dw.com/p/1CiuG
Wanajeshi wa Ufaransa waliowekwa Gao,kaskazini ya MaliPicha: JOEL SAGET/AFP/Getty Images

Tunaanza moja kwa moja na ziara ya rais wa Ufaransa barani Afrika,ziara iliyomulikwa na magazeti tofauti ya humu nchini.

"Ufaransa inajiimarisha kijeshi barani Afrika" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya Berliner Zeitung.Katika ziara yake ya siku tatu iliyoanzia Côte d'Ivoire,kupitia Niger na kumalizikia Tchad rais Hollande amefungua njia ya kuwekwa kikosi cha kupambana na ugaidi katika eneo la Sahel."Tunataka kubuni mkakati utakaorahisisha kuingilia kati haraka kijeshi" alisema rais wa Ufaransa mwishoni mwa ziara hiyo mjini Ndjamena.Huko ndiko watakakowekwa sehemu kubwa ya wanajeshi 3000 wa Ufaransa wanaotarajiwa kuanza shughuli zao agosti mosi ijayo-linaandika gazeti la Berliner Zeitung.Opereshini Barkhane itaenea katika nchi tano za Afrika:Mauritania,Mali,Niger,Burkina Faso na Tchad.Berliner Zeitung linazungumzia pia azma ya Ufaransa kushirikiana na vikosi vya Marekani katika Opereshini hizo na kukumbusha kituo cha madege yasiyokuwa na rubani ya Marekani kinakutikana Niamey mji mkuu wa Niger.

Na viongozi wa Afrika wanasema nini?

Suala kama Ufaransa ilishauriana na viongozi wa Afrika kuhusu mpango huo-hakuna aliyelijibu linaandika Berlinere Zeitung lililomnukuu waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian aliyefuatana na rais Hollande katika ziara hiyo,akisema"mataifa mengi yanaunga mkono opereshini hizo."Berliner Zeitung linakumbusha miaka michache iliyopita hali ilikuwa nyengine kabisa;rais Mahamadou Issoufou wa Niger alipinga kuwepo wanajeshi wa Ufaransa katika nchi hiyo ambako katika eneo lake la kaskazini makampuni ya Ufaransa yanachimba migodi ya urani kwaajili ya vinu vyao vya nishatai ya nuklea. Hata rais Idriss Déby wa Tchad,licha ya kusema vikosi hivyo vinahitajika,amesisitiza lakini viwekwe kwa muda maalum tu na kwamba mnamo siku zinazokuja mataifa ya Afrika ndio yanayobidi kudhamini usalama wao-linamaliza kuandika Berliner Zeitung.

Neues Deutschland linazungumzia pia mkakati wa kujiimarisha kijeshi Ufaransa barani Afrika likimulika zaidi maandamano ya wapinzani wa ziara hiyo pamoja na kutiwa ndani kwa muda wale wote walionyanyua sauti kuipinga.

Makubaliano ya Brazzaville yataheshimiwa?

Hali katika jamhuri ya Afrika kati nayo pia ilimulikwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani wiki hii,wakiyawekea matumaini makubaliano ya kuweka chini silaha yaliyofikiwa katika mkutano wa Brazaville.Lilikuwa pia Berliner Zeitung lililozungumzia mfarakano na matumizi ya nguvu yasiyokuwa na mwisho katika nchi hiyo na kusema kuingilia kati wanajeshi 2000 wa Ufaransa na 6000 wa kulinda amani kutoka nchi za Afrika hakujasaidia kukomesha mzozo huo unaoendelea kwa muda wa miezi 16 hivi sasa.Berliner Zeitung limechapisha uchunguzi wa maoni uliosimamiwa na shirika la madaktari wasiojali mipaka katika kambi moja ya wakimbizi nchini Tchad, unaoonyesha kila watatu kati ya familia 3500 aliyeulizwa maoni yake,amesema amempoteza jamaa yake mmoja.Uchunguzi huo unabainisha katika mzozo wa Jamhuri ya Afrika kati,watu milioni moja wamepoteza maskani yao na maelefu kupoteza maisha yao.

Umoja wa ulaya wasaini Ushirikiana wa kibiashara na nchi sita za Afrika

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu mkataba wa biashara huru kati ya halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya an mataifa sita ya Afrika kusini mwa jangwa la sahara."Kibweta cheusi cha biashara huru" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya die Tageszeitung inayozungumzia kuhusu kutiwa saini makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya na Botswana,Lesotho,Mozambik,Namibia,Afrika Kusini na Swaaziland."Makubaliano hayo yatafungua njia ya maendeleo,kubuniwa nafasi za kazi na ukuaji wa kiuchumi"limeandika gazeti hilo la mji mkuu lililowanukuu maafisa wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya-lakini kama yaliyoandikwa yanaweza kuthibitishwa-hakuna ajuaye.Gazeti linasema halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya haitaki bado kuchapisha waraka huo-Unabidi kwanza uchungzwe kisheria na baadae uidhinishwe na mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya na taasisi za Umoja huo.Baada ya kutafasiriwa ndipo waraka wa makubaliano hayo utakapoweza kuchapishwa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/BASIS/Presser/

Mhariri: Josephat Charo