1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yakabiliwa na kishindo cha Umoja wa Afrika

19 Juni 2015

Mkutano wa kilele wa 25 wa umoja wa Afrika uliogubikwa na madai ya kutaka akamatwe rais wa Sudan pamoja na bima ya kupambana na majanga ndizo mada zilizopewea umuhimu magazetini wiki iliyopita

https://p.dw.com/p/1FjfJ
Rais Jacob Zuma wa Afrika kusini akiamkiana na viongozi wanaohudhuria mkutano wa 25 wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini JohannesburgPicha: picture-alliance/dpa/Gcis/Siyasanga Mbambani

Tuanzie lakini na mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Johannesburg. "Mzee Mugabe, shujaa wetu" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti la mjini Berlin, die Tageszeitung linalosema rais huyo wa Zimbabwe, akiwa mwenyekiti wa mkutano huo wa kilele ametumia maneno yanayofaa alipotamka "Afrika inabidi ijiokoe yenyewe. Wengi wanamsifu Robert Mugabe kuwa ni mtu mwenye kuona mbali, linaandika gazeti la die Tageszeitung linalohisi lakini kisa cha Bashir kimeufuja mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Afrika. Mugabe ndiye aliyehimiza vitega uchumi katika sekta ya usafiri kwa kutumia reli, ndege na tenknolojia ili Afrika ijiendeleze yenyewe. Kama zamani Mugabe alikuwa akizitaja nchi za magharibi kuwa ndio chanzo cha matatizo ya Afrika, hivi sasa anasema ufumbuzi wa matatizo hayo unakutikana Afrika. "Tuache kusafirisha mali ghafi ya Afrika, tunahitaji viwanda na nafasi za kazi kwa wananchi wetu ili kuzuwia wimbi la waafrika, wake kwa waume na watoto wanaoyatia hatarini maisha yao katika bahari ya Mediterania ili kutafuta kazi kwengineko. Die Tageszeitung limemaliza ripoti yake kwa kuzungumzia jinsi rais Mugabe na viongozi wengine wa Umoja wa Afrika walivyosifu kuundwa kanda ya biashara huru-TFTA inayozihusisha nchi 26 za Afrika.

Umoja wa Afrika wawapa kinga viongozi

Kiwingu kilichotanda wakati wa mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Johannesburg, kimezungumziwa pia na gazeti la Die Welt. "Muimla Omar al Bashir yuko njiani kurejea nyumbani" ndio kichwa cha maneno cha gazeti hilo linalosema rais huyo wa Sudan anasakwa na korti kuu ya kimataifa ya uhalifu mjini The Hague kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu wa vita, uhalifu dhidi ya ubinaadamu na mauwaji ya halaiki ya watu laki tatu. Licha ya yote hayo Afrika kusini inamwachia kutoroka. Die Welt linakumbusha hii si mara ya kwanza kwa Umoja wa Afrika kuonyesha mshikamano na Bashir. Mwaka 2012, mkutano wa kilele ulipokuwa uitishwe Malawi na nchi hiyo ya kusini mwa Afrika kutishia Bashir angekamatwa, mkutano huo wa kilele ulihamishiwa kufumba na kufumbua nchini Ethiopia. Die Welt linasema Umoja wa Afrika unatoa kinga kwa viongozi wanaohudhuria mikutano ya kilele kwa hivyo yaliyotokea Johannesburg si mapya hata kama nchini Afrika kusini kuliko katika nchi yeyote nyengine ya Afrika suala la ushirikiano pamoja na ICC limeingizwa katika madftari ya sheria ya nchi hiyo. Kisa cha al Bashir ndicho kitakachoamua kuhusu mustakbal wa korti kuu ya kimataifa ya uhalifu ICC linamaliza kuandika die Welt kwa kusema ikiwa ndege iliyopigwa chapa Sudan 01 imeondoka bila ya shida katika uwanja wa kijeshi wa Waterkloof, Bashir akiwa ndani yake, basi itegemewe pia kwamba ndege hiyo hiyo itaendelea kutuwa na kuondoka katika viwanja vya nchi nyingi zaidi za Afrika.

Bima ya majanga barani Afrika

Mada yetu ya mwisho katika ukurasa huu wa Afrika katika magazeti ya Ujerumani wiki hii imeripotiwa na gazeti la Der Tagesspiegel. "Pesa badala ya Mavuno" ndio kichwa cha maneno cha ripoti ya gazeti hilo inayozungumzia kuhusu bima iliyoanzishwa miaka miwili iliyopita na Umoja wa Afrika ya kinga dhidi ya ukame. Mataifa matatu yameshafaidika na bima hiyo iliyopewa jina "Uwezo wa kukabiliana na majanga barani Afrika-ARC. Mauritania, Niger na Senegal zilikumbwa na ukame mwaka 2014 na kupatiwa jumla ya dala milioni 26. Kenya pia imejiunga na bima hiyo tangu dakika ya mwanzo mradi huo ulipoanzishwa na mataifa matano mengine yamejiunga hivi sasa ambayo ni Gambia, Burkina Faso, Mali, Malawi na Zimbabwe. Mradi huo wa bima ya kukabiliana na majanga ya ukame unaendelezwa kwa ushirikiano miongoni mwa mengineyo pamoja na shirika la bima la Ujerumani New Re. Pindi ukifanikiwa mradi huo unaweza siku za mbele kushughulikia pia hasara zinazotokana na dharuba, mafuriko au hata maradhi ya kuambukiza-linamaliza kuandika Der Tagespiegel.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Basis/Presser/All

Mhariri:FE: Josephat Charo