1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AFRIKA KATIKA MAGAZETI YA UJERUMANI.

Abdu Said Mtullya9 Septemba 2011

Magazeti ya Ujerumani yakariri tuhuma kwamba Kamanda wa waasi nchini Libya ni Al- Qaeda?

https://p.dw.com/p/12W5t
Waasi wakiimarisha usalama mjini TripoliPicha: dapd

Pamoja na masuala mengine magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya Somalia,tuhuma juu ya uhusiano baina ya utawala wa Gaddafi na mashirika ya ujasusi ya nchi za magharibi.

Magazeti hayo pia yamechapisha makala juu ya kesi inayomkabili aliyekuwa Rais Misri Hosni Mubarak.

Gazeti la Süddeutsche limechapisha makala juu ya Somalia. Katika makala hiyo gazeti hilo linazungumzia juu ya mkutano wa siku tatu uliofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu kwa lengo la kutafuta amani. Gazeti la Süddetsche Zeitung limeandika kuwa wanasiasa wa Somalia wamekubaliana juu ya kuleta maridhiano lakini wengi wana mashaka iwapo lengo hilo litafikiwa, na hivyo kuweza kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Somalia.

Gazeti la Süddeutsche limearifu katika taarifa yake kwamba baada ya siku tatu za majadiliano wanasiasa wa Somalia waliupitisha mpango wa kuleta amani. Viongozi wa pande mbalimbali wamejiwajibisha kuleta mageuzi nchini Somalia katika kipindi cha mwaka mmoja ili kuuimarisha usalama na kuwawezesha watu wa nchi hiyo kuichagua serikali mpya kwa ajili ya wote.

Wakati huo huo gazeti hilo limekumbusha juu ya wasomali 750,000 waliomo katika hatari ya kukumbwa na maafa ya njaa. Gazeti hilo limezikariri taarifa za Umoja wa Mataifa zilizosema kuwa majimbo mengine ya kusini mwa Somalia yameongezeka katika orodha ya sehemu zinazokabiliwa na baa la njaa.

Gazeti la Kölner Stadt Anzeiger pia limeandika juu ya Somalia. Katika makala yake gazeti hilo linasema jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutafuta suluhisho la kisiasa nchini Somalia.

"Juhudi za kueleta haki" Hicho ni kichwa cha habari katika gazeti la Berliner Zeitung juu ya kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa Misri Hosni Mubarak. Mubarak alifikishwa mbele ya mahakama mjini Cairo kwa mara ya tatu Jumatano iliyopita. Gazeti la Berliner Zeitung limeripoti juu ya ghasia zilizotokea nje ya mahakama zilizofanywa na watu wanaotaka haki itendeke. Watu hao walipambana na wale ambao bado wanamuunga mkono Mubarak.

Gazeti la Berliner Zeitung limemkariri mama mmoja miongoni mwa wale wanaotaka haki itendeke, akisema kuwa bila ya Mubarak na watoto wake kupewa adhabu, ili kulipiza kifo cha mtoto wake na vya watu wengine 800, Misri haitakuwa imejenga mwanzo mpya baada ya mapinduzi kufanyika. Mubarak anakabiliwa na madai ya kusababisha vifo vya watu hao.

Gazeti la die Welt limechapisha makala juu ya tuhuma za kuwapo ushirikiano baina ya utawala wa Gaddafi na mashirika ya ujasusi ya Marekani CIA na MI6 la Uingereza. Katika makala yake gazeti hilo pia limeandika juu ya kamanda wa waasi Abdel Hakim Belhaj mwenye historia yenye dosari. Gazeti la die welt limeandika kuwa Kamanda Belhaj ni mtu mwenye haiba ya pande mbili.

Katika Libya mpya yeye yumo kwenye sehemu ya uongozi. Tokea wiki kadhaa sasa Belhaj ni kamanda wa waasi katika mji wa Tripoli. Wadhifa huo unamweka katika nafasi ya kuwa mwakilishi wa kuwasiliana na wajumbe wa nchi za jumuiya ya kujihami ya NATO. Lakini Gazeti la Die Welt limearifu kuwa nyaraka za shirika la ujasusi CIA zimeonyesha kwamba mtu huyo ni mwanaitikadi kali wa kiislamu na pia ana ustadi wa mikakati ya kijeshi. Pamoja na hayo anatuhumiwa kuwa na uhusiano na mtandao wa kigaidi wa al Qaida, kwani mnamo miaka ya nyuma aliwahi kupigana nchini Afghanistan na Somalia. Lakini katika upande wa nani? Gazeti la die Welt linauliza katika makala yake?

Baada ya vyombo vya habari kuchapisha habari juu ya tuhuma za uhusiano uliokuwapo baina ya utawala wa Gaddafi na mashirika ya ujasusi ya Marekani na ya Uingereza, gazeti la Handelsblatt limechapisha habari juu ya biashara ya silaha kati ya China na utawala wa Gaddafi. Katika makala yake gazeti hilo limeeleza kuwa nyaraka zilizokutwa katika ofisi ya Gaddafi zinaonyesha kuwa Wachina walimuuzia Gaddafi silaha.

Gazeti hilo limemnukuu msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China akithibitisha kufanyika mazungumzo juu ya kumuuzia Gaddafi silaha thamani ya dola milioni 200. Lakini msemaji huyo ameeleza kuwa hakuna mkataba uliofikiwa na wala hakuna silaha zilizopelekwa Libya.

Mwandishi /Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Josephat Charo