1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya2 Novemba 2012

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya adhabu ya kifungo cha miaka minane jela iliyotolewa kwa mwanasiasa wa upinzani nchini Rwanda. Pia yameandika juu ya hatari ya magaidi wa al-Qaeda barani Afrika.

https://p.dw.com/p/16c2d
Mwanasiasa wa upinzani nchini Rwanda Victoire Ingabire.
Mwanasiasa wa upinzani nchini Rwanda Victoire Ingabire.Picha: AP

Gazeti la "die tageszeitung" limeandika juu ya hukumu ya kifungo cha miaka minane iliyotolewa jumanne iliyopita kwa mwanasiasa wa upinzani Victoire Ingabire. Mahakama ya mjini Kigali ilimtia hatiani kwa mashataka ya ugaidi na kwa kukana kutokea mauaji halaiki nchini Rwanda.

Gazeti la "die tageszeitung" linasema katika makala yake kwamba hukumu hiyo imeshutumiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu. Hata hivyo hukumu hiyo siyo kali kama ilivyohofiwa hapo awali. Upande wa mashataka ulitaka Ingabire apewe adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Wakati huo huo gazeti la "die tageszeizung" limevikariri vyombo vya habari vya nchini Rwanda vikiarifu kwamba Ingabire anaweza kusamehewa ikiwa ataitambua hukumu iliyotolewa ,kwa sababu tayari ameshatumikia muda wa miaka miwili jela! Victoire Ingabire ni kiongozi wa chama cha United Democratic Forces ambacho hakijaruhusiwa kusajiliwa nchini Rwanda.

Gazeti la "Süddeutsche "linayazungumzia madai ya serikali ya Sudan juu ya kushambuliwa kiwanda chake cha silaha na ndege za Israel. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba Israel bado haijayajibu madai hayo. Hata hivyo gazeti hilo limemnukuu Jenerali mmoja Amos Gilad akisema katika mahojiano na Radio kwamba Sudan ni nchi hatari ya kigaidi inayoungwa mkono na Iran. Katika makala yake gazeti hilo pia linasema kwamba, kwa kweli,Sudan ni nchi inayotumiwa kama njia ya kupenyezea silaha katika Ukanda wa Gaza na pia ni mahala ambapo makundi yanayohusiana na al-Qaeda yanajenga kambi.Kwa mujibu wa taarifa za wapinzani, zilizokaririwa na gazeti la "Süddeutsche Zeitung" kiwanda kilichoshambuliwa na ndege za Israel kilijengwa na kusimamiwa na Iran.

Gazeti la "Die Zeit" linapiga mbiu ya mgambo juu ya mtandao wa al-Qaeda barani Afrika. Linasema mtandao huo bado haujashindwa.Gazeti hilo linaeleza kwamba magaidi wa al-Qaeda wanaendelea kuwapata watu wa kuwaunga mkono barani Afrika. Linauliza jee ,ll-Qaeda bado ni hatari,? Linajibu swali hilo kwa kukumbusha kwamba tareha 11 mwezi wa Septemba, yaani ilipotimia miaka 11 tokea kufanyika mashambulio katika miji ya New York na Washington, ubalozi mdogo wa Marekani ulivamiwa katika mji wa Benghazi nchini Libya. Watumishi wa kibalozi wanne waliuawa ikiwa pamoja na balozi Christopher Stevens. Wanaotuhumiwa kufanya mauaji hayo ni wanajihadi wa Libya wanaohusiana na al-Qaeda.

Gazeti la "Die Presse" linaitupia macho ripoti ya Benki ya Dunia juu ya wakulima wa Afrika. Katika ripoti yake Benki ya Dunia inasema kuwa wakulima wa Afrika wangeliweza kuyakidhi mahitaji ya chakula ya bara hilo bila ya matatizo yoyote lakini vizingiti vya biashara vinalizuia bara hilo kufanya biashara na mabara mengine. Gazeti la "Die Presse" linaeleza: "Wakati ambapo uchumi wa nchi za magharibi umeshuka,uchumi wa nchi za Afrika kusini ya jangwa la Sahara unastawi kwa asilimia 5" .Gazeti la "Die Presse" limeikariri ripoti ya Benki ya Dunia ikisema kwamba, endapo bara la Afrika lingelikuwa nchi moja, mwananchi wa wastani mwenye kipato cha dola 1,700 angelikuwa mtu wa tabaka la kati.

Lakini Benki ya dunia imesema kilimo hakiendi sambamba na maendeleo hayo.Bado mamilioni ya watu wanasibika na njaa. Gazeti la "Die Presse" limeikariri ripoti ya Benki ya Dunia ikisema wakulima wa Afrika wanakabiliwa na vizingiti vingi na kutokana na hali hiyo biashara kati ya nchi za Afrika inatatizika. Matokeo yake ni kwamba asilimia 95 ya nafaka inayoagizwa inatoka nje ya Afrika.!

Mwandishi:Mtullya abdu:Deutsche Zeitungen:

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman