1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya16 Februari 2013

Pamoja na mengine wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika habari za kushtusha juu ya mwanamichezo maarufu wa Afrika Kusini Oscar Pistorius.

https://p.dw.com/p/17fJU
Mwanamichezo maarufu wa Afrika Kusini Oscar Pistorius,matatani
Mwanamichezo maarufu wa Afrika Kusini Oscar Pistorius, matataniPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "Bild Zeitung" limeandika taarifa juu ya mwanamichezo maarufu Oscar Pistorius wa Afrika Kusini,aliefikishwa mahakamani kufuatia mauaji yaliyotokea nyumbani kwake.

Gazeti hilo limearifu kuwa alieuawa kwa kupigwa risasi alikuwa mpenzi wa mwanamichezo huyo Reeva Steenkamp.Gazeti limeripoti kuwa Pistorius alifyatua risasi kutokana na kufikiria jambazi aliingia ndani ya nyumba yake.

Gazeti la "Bild Zeitung"linauliza jee Pistorius alifyatua risasi kwa makosa?

Gazeti hilo limearifu kuwa Polisi wa Afrika Kusini wanao uhakika kwamba Pistorius ndiye aliefyatua risasi.Risasi nne zilifyatuliwa,na kumpata marehemu kichwani na katika sehemu nyingine za mwili.Gazeti la "Bild Zeitung" limeandika katika taarifa yake kwamba watu nchini Afrika Kusini wameshtushwa sana na mkasa huo.

Gazeti la "Süddeutsche Zeitung"wiki hii limeandika juu ya mgogoro wa Mali.

Gazeti hilo limearifu kwamba watu katika mji wa Gao wanaishi na hofu kubwa kila siku.Gazeti hilo limeandika kwamba hofu ya kutokea mashambulio imetanda miongoni mwa watu katika mji wa Gao uliopo kaskazini.

Gazeti la"Süddeutsche limeripoti kuwa wanajeshi wa Ufaransa walilitegua bomu la kilo 600 Jumatano iliyopita katika mji wa Gao.Bomu hilo lilikuwa limefichwa katika nyumba moja ambamo Waislamu wenye itikadi kali walikuwa wanaishi. Gazeti la"Süddeutsche"limemkariri kiongozi wa kundi la waislamu wenye itikadi kali nchini Mali akisema kuwa wapiganaji wao wataendelea kupambana na wanajeshi wa Ufaransa na wengine wote wanaoshirikiana nao.

Gazeti la"Frankfurter Allgemeine"pia limeandika juu ya mgogoro wa nchini Mali.Limezikariri taarifa zinaonyesha kwamba majeshi ya Ufaransa bado hayajawashinda kabisa waasi,licha ya kufanikiwa kuingia kwa haraka na kuwatimua waasi hao kwenye miji fulani.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" pia limearifu juu ya mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa nchi za Umoja wa Ulaya waliokutana mjini Dublin kuujadili mgogoro wa Mali.Mjumbe wa Ufaransa alisema kwenye mkutano huo kwamba pana hatari kubwa ya wapiganaji wenye itikadi kali,kuingia Mali kutokea nchi za jirani na kuwaunga mkono waasi wa nchi hiyo.

Gazeti la"die tageszeitung"limeandika makala inayotilia maanani juhudi za wanasiasa wa Kenya katika kuepusha machafuko kama yale yaliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.

Gazeti la"die tageszeitung"limeandika kuwa mnamo wiki tatu zijazo watu wa Kenya watashiriki katika uchaguzi wa Rais na bunge.Na kwa mara ya kwanza wagombea Urais walipambana kwa hoja katika mjadala uliotangazwa na vyombo vya habari moja kwa moja.Gazeti la"die tageszeitung" linaaarifu kwamba katika hoja zao wanasiasa wa Kenya waliyazungumzia masuala ya umasikini,ufisadi udhaifu wa miundombinu na njaa.Lakini gazeti hilo linatilia maanani kwamba kitovu cha mjadala wa wanasiasa hao kilikuwa ,mauaji yaliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka wa 2007.

Timu ya taifa ya Nigeria imelibeba kombe la ubingwa wa kandanda wa mataifa ya Afrika nchini Afrika Kusini.Anaefurahi zaidi juu ya ushindi huo ni kocha wa timu hiyo Stephen Keshi.Gazeti la "Die Welt" linaeleza kuwa muda mfupi tu baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa uwanjani,tajiri mkubwa anefanya biashara ya simu nchini Nigeria Mike Adenuga alitangaza donge la dola laki 2 kwa ajili ya kocha wa Nigeria Stephen Keshi.Tajiri huyo pia atalipa mshahara wa kocha huyo kuanzia sasa.

Mwandishi: Mtullya Abdu:Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Khelef