1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya10 Mei 2013

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya Jukwaa la Uchumi wa Dunia na kambi ya wakimbizi wa Dadaab nchini Kenya

https://p.dw.com/p/18Vsq
Rais Jacob Zuma kwenye Jukwaa la Uchumi wa Dunia,Cape Town
Rais Jacob Zuma kwenye Jukwaa la Uchumi wa Dunia, Cape TownPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la "DerTagesspiegel" limeandika juu ya Jukwaa la 23 la Uchumi wa Dunia lililofanyika mjini Cape Town nchini Afrika Kusini.

Bara la Afrika lashuhudia unomi

Wajumbe zaidi ya 1,000 walikutana kwenye kongamano hilo kujadili maendeleo ya uchumi ya bara la Afrika katika muktadha wa ustawi wa uchumi wa kuridhisha.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linatilia maanani kwamba katika kipindi cha miaka10 hadi 15 iliyopita bara la Afrika limeshuhudia unomi yaani ustawi wa haraka kutokana na maliasilia. Wajumbe walikutana mjini Cape Town kuzungumzia maendeleo ya bara hilo.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limeandika juu ya mkutano huo kwa kusema ,baada ya kukwama kwa muda wa miaka mingi bara la Afrika sasa linaonyesha matumaini. Bara la Afrika limewasilisha takwimu juu ya ustawi imara kwenye mkutano wa mjini Cape Town. Kwa muda wa miaka mingi bara la Afrika halikutoa mchango wowote katika uchumi wa dunia.

Afrika ilipigwa chenga na jumuiya kimataifa:

Jumuiya ya kimataifa ilikuwa inalipiga chenga bara la Afrika kutokana na siasa zake za chama kimoja,uchumi mbovu,na kutokana na kuzidi kuzama katika madeni na kuendelea kurudi nyuma.

Lakini la "Der Tagesspiegel" limeandika kwamba mambo yamebadilika barani Afrika tokea kuanza kuinukia kwa China inayolihitaji bara hilo ili kuyakidhi mahitaji yake ya nishati.Gazeti hilo limewanukuu wataalamu wa masuala ya uchumi wakisema huenda bara la Afrika likawa mwokozi wa nchi za magharibi zinazokabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi.

Maendeleo barani Afrika
Maendeleo barani AfrikaPicha: dpa

Hata hivyo gazeti hilo limemnukuu mwanauchumi Mkuu wa Goldman Sachs,Jim O' Neill akisema, ili Afrika iweze kuinuka kikweli, itadibi ijenge mifumo thabiti ya huduma za afya na elimu, lakini hasa ijenge mfumo wa utawala bora.

Umasikini unaweza kuondolewa Afrika:

Gazeti la "Die Welt" wiki hii limefanya mahojiano na Jan Walliser anaesimamia kitengo cha Afrika kwenye Benki ya Dunia. Katika mahojiano hayo Bwana Walliser ameeleza matumaini kwamba itawezekana kuupiga vita umasikini barani Afrika.

Gazeti la "Die Welt" limemnukuu afisa huyo wa Benki ya Dunia akisema kwamba eneo la Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara lina nchi 48. Amesema ni eneo kubwa sana lenye matatizo yanayotofautiana.Na pia zipo nchi dhaifu. Lakini licha ya hayo ameeleza , kwamba mtu anaweza kusema nchi hizo hazina matatizo makubwa kuhusu uchumi wa kizio(microeconomics,) na pia hazina matatizo makubwa kuhusu bajeti. Nchi hizo hazilemewi sana na zigo la deni kama hapo awali.Kwa hivyo, kwa msaada wa shirika la maendeleo la kimataifa, IDA, itawezekana kupambana na umasikini katika nchi masikini.

Wasomali waikimbia Dadaab :

Gazeti la "Die Presse" limeandika makala juu ya kambi ya wakimbizi wa kisomali ya Dadaab ya nchini Kenya.Gazeti hilo limeripoti kwamba wakimbizi wa Somalia sasa wanaikimbia kambi hiyo ya wakimbizi ambayo ni kubwa kabisa duniani.Gazeti hilo linaeleza kwamba tokea majeshi ya Kenya yaingie Somalia mnamo mwaka 2011 hali kwenye kambi ya Dadaab imezidi kuwa mbaya.Wakimbizi wengi sasa wanataka kurudi Somalia.

Kambi ya wakimbizi ya Dadaab nchini Kenya
Kambi ya wakimbizi ya Dadaab nchini KenyaPicha: Getty Images

Gazeti la "Die Presse" linafahamisha kwamba watu 460,000 wapo kwenye kambi hiyo.Takriban asilimia 95 ni Wasomali. Wakimbizi wengine wanatoka Sudan ya kusini,Ethiopia na Kongo. Mara kwa mara yanatokea mapambano baina ya jumuiya mbalimbali. Mtu mmoja Abdi Arab amekaririwa na gazeti la "Die Presse" akiarifu kuwa panatokea migogoro baina ya wakimbizi kutoka Somalia na Wasomali wanaotokea katika jimbo la Ogaden nchini Ethiopia.

Kambi ya Dadaab ipo kaskazini mwa Kenya umbali wa kilometa mia moja kutoka kwenye mpaka na Somalia.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman