1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya31 Mei 2013

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yanaungalia msimamo wa nchi za Afrika dhidi ya Mahakama Kuu ya Kimataifa ya mjini the Hague, ICC . Pia yameandika juu ya vifo vya watoto wanaotahiriwa nchini Afrika Kusini.

https://p.dw.com/p/18hy6
Viongozi wa Afrika waipinga Mahakama ya Kimataifa, ICC
Viongozi wa Afrika waipinga Mahakama ya Kimataifa,ICCPicha: picture alliance/ZUMAPRESS.com

Gazeti la "Süddeutsche" limeandika juu ya msimamo wa nchi za Afrika kuhusu Mahakama Kuu ya Kimataifa ya mjini The Hague,ICC. Gazeti hilo linasema katika makala yake kwamba katika kuadhimisha mwaka wa 50 tokea kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika, viongozi wa nchi hizo walikusudia kuonyesha umoja wa bara lao.

Gazeti la "Süddeutsche"limeandika kwamba katika maadhimisho ya mwaka wa 50 tokea kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika ,OAU ,viongozi wa nchi na wakuu wa serikali walipitisha uamuzi juu ya mambo mawili muhimu ili kusisitiza umoja wao.

Jeshi la pamoja:

Kwanza kulianzisha jeshi la pamoja litakalokuwa na uwezo wa kuingilia kati kwa haraka katika nchi yoyote pale itakapohitajika. Lengo ni kuondokana na utepetevu wa hadi sasa, kama ilivyoshuhudiwa nchini Mali hivi karibuni ambako Waislamu wenye itikadi kadi waliiteka sehemu ya kaskazini ya nchi kwa muda fulani bila ya Umoja wa Afrika kuweza kuchukua hatua yoyote.

Pili viongozi wa Afrika wameitaka Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague iache kuwaandama Waafrika.

Na gazeti la"Berliner Zeitung" limeandika kwamba uhusiano baina ya nchi za Afrika na Mahakama Kuu ya Kimataifa,ICC umefikia kiwango cha chini kabisa, baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn kusema kwamba Mahakama hiyo inawawinda Waafrika kwa sababu za kibaguzi

Polisi wa Uganda na vyombo vya habari:

Polisi wa Uganda wamekuwa wanavutana na vyombo vya habari kuhusiana na barua inayodaiwa kuandikwa na Jenerali mmoja alieikimbia nchi.Kwa mujibu wa barua hiyo Rais Yoweri Museveni anapanga kumuua yeyote yule anaepinga mwanawe kuwa mrithi wake wa urais. Hizo ni habari zilizoandikwa na gazeti la "die tageszeitung" Gazeti hilo linaarifu kwamba polisi walizivamia ofisi za magazeti ya "Daily Monitor na "Red Pepper" ili kuzipekua, katika juhudi za kuitafuta barua hiyo.

Gazeti la "die tageszeitung" limeripoti kuwa mtoto wa Museveni,Muhoozi Keinerubaga mpaka sasa hajaonyesha nia ya kuwa Rais wa Uganda,na badala yake anajistarehesha katika klabu za burudani za usiku.

Watoto na vijana wafa kutokana na tohara:

Gazeti la "Süddeutsche" wiki hii pia limeandika juu ya vifo vinavyotokea kila mwaka nchini Afrika Kusini kutokana na jadi ya tohara. Gazeti hilo limeripoti kuwa vijana wasiopungua 30 wamekufa mnamo mwezi wa Mei pekee nchini Afrika Kusini kutokana jadi ya kutahiri. Gazeti hilo limefahamisha kwamba kila mwaka wanakufa watoto kadhaa wakiwa jandoni, lakini safari hii idadi imekuwa kubwa mno.

Gazeti hilo limearifu kuwa watoto hao wanakufa kutokana na kuvuja damu nyingi baada ya kutahiriwa na wengine wanakufa kutokana na maambukizi.Gazeti la "Süddeutsche" limemnukuu Rais Jacob Zuma akisema kuwa taifa lote la Afrika Kusini limeshtushwa na vifo vya watoto na vijana hao.

Wasio na ujuzi wajipenyeza katika jadi ya kutoa tohara:

Rais Zuma amesema,kila mwaka watoto na vijana wanakufa katika mikono ya wale ambao walipaswa kuwalinda na kuwaendeleza.Amesema ni jambo lisilokubalika kwamba, kila wanapofikia katika hatua muhimu ya maisha yao, vijana wanayapoteza maisha hayo kwa njia ya maumivu makali. Gazeti la "Süddeutsche" limeripoti kwamba uchunguzi wa kwanza umeonyesha kuwa watu wasiokuwa na ujuzi wamejiingiza katika shughuli za kuitekeleza jadi ya kuwapa watoto na vijana tohara.

Mwandishi: Mtullya Abdu./Deutsche Zeitungen:

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman