1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani.

Abdu Said Mtullya21 Juni 2013

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya uchaguzi wa Zimbabwe na juu ya wakimbizi kutoka Afrika waliokwama katika mji wa Hamburg nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/18uBw
Waziri Mkuu wa Zimbabwe Morgan Tsvangirai,apinga terehe ya uchaguzi
Waziri Mkuu wa Zimbabwe,Morgan Tsvangirai,apinga tarehe ya uchaguziPicha: picture alliance/AP

Gazeti la "Süddeutsche" linasema Rais Mugabe wa Zimbabwe na Waziri Mkuu wake Morgan Tsvangirai wanazozana juu ya tarehe ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini humo. Gazeti hilo limeripoti kwamba wananchi wengi wa Zimbabwe sasa wana wasiwasi juu ya kuripuka tena kwa ghasia nchini mwao.

Gazeti hilo linasema mzozo juu ya tarehe ya kufanyika uchaguzi unasababisha taharuki miongoni mwa wananchi wa Zimbabwe.Watu wanahofia kutokea tena kwa umwagikaji damu kama ilivyotukia wakati wa uchaguzi wa Rais wa mwaka wa 2008. Mugabe anataka uchaguzi ufanyike tarehe 31 mwezi ujao wakati Waziri Mkuu wake Morgan Tsvangirai anaipinga tarehe hiyo.

Mageuzi kwanza kabla ya uchaguzi:

Gazeti la "Süddeutsche" linaeleza kuwa Waziri Mkuu Tsvangirai anataka kwanza Bunge liyaidhinishe mageuzi yanayohitajika kufanyika kabla ya kuitishwa kwa uchaguzi huo.Tsvangirai analalamika kwamba Rais Mugabe na chama chake cha Zanu PF anajaribu kuyazuia mageuzi hayo.Gazeti la "Süddeutsche" linaarifu kwamba Rais Mugabe alitoa amri wiki iliyopita ya kufanyika uchaguzi huo tarehe 31 mwezi wa Julai.

Idadi ya watu kufikia zaidi ya Bilioni 10 :

Gazeti la "Der Tagesspiegel" wiki hii limechapisha makala juu ya utabiri wa kuongezeka kwa idadi ya watu duniani, kwa kuliangalia bara la Afrika.Gazeti hilo linasema hali itakuwa ngumu barani Afrika kutokana na ongezeka hilo ,linalotabiriwa kufikia binadamu Bilioni 10,9 .

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linaeleza kuwa wataalamu wanakubaliana kwamba idadi ya watu itaongezeka katika nchi zinazoendelea mnamo kipindi cha miaka10 ijayo. Gazeti hilo limeikariri ripoti ya Umoja wa Mataifa ikisema kuwa hadi mwaka wa 2100 idadi ya watu barani Afrika itafikia Bilioni 4,2

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limemnukulu Profesa wa Ujerumani Thomas Büttner, aliewahi kufanya kazi kwenye kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia idadi ya binadamu, akisema kuwa katika nchi kama Uganda,Malawi na Niger idadi ya watu itaongezeka mara tano hadi kufikia mwaka huo wa 2100.Amesema nchini Uganda watu wataongezeka mara 30.

Gazeti la "Der Tagesspiegel"limeikariri ripoti ya Umoja wa Mataifa ikisema kuwa wanawake milioni 80 wanapa uja uzito bila ya kupenda katika nchi zinazoendelea .Ripoti hiyo imeshauri kuwekwa kwa mkakati wa kuzuia ujauzito kama njia ya kupunguza umasikini.

Wakimbizi kutoka Afrika kufukuzwa Ujerumani?

Gazzeti la"Süddeutsche" limearifu katika makala yake kwamba wakimbizi 300 kutoka Afrika wako katika mji wa Hamburg wakiwa wamekwama.Gazeti hilo limeripoti kwamba serikali ya jimbo la Hamburg inakusudia kuwafukuza Waafrika hao.

Gazeti hilo linaeleza kwamba Polisi wa jiji la Hamburg waliwagundua watu hao miezi mitatu iliyopita. Walikuwa wanalala chini ya madaraja na katika bustani za mapumziko.Wengi wao ni wahamiaji kutoka nchi kama Mali na Ghana.Watu hao walienda Libya, lakini waliaondoka kuvikimbia vita vya mwaka 2011.Kutoka hapo waliingia nchini Italia.

Gazeti la "Süddeutsche" linaarifu zaidi kwamba serikali ya Italia ilitoa kiasi cha Euro 500 kwa kila mmoja pamoja na visa ya nchi za Ulaya.Vibali hivyo vimewawezesha kuenda katika jiji la Hamburg. Serikali ya jiji hilo haijui la kufanya juu ya Waafrika hao 300, lakini ingelipendelea kuwafukuza haraka kwa kadri itakavyowezekana.

Wakaazi wa Hamburg washikamana na Waafrika hao:

Gazeti la "Süddeutsche" limeripoti kwamba wakaazi wa jiji la Hamburg wanayo maoni tafauti na yake ya serikali ya jiji lao. Klabu ya washabiki ya "St .Pauli" ya jiji hilo imetoa mwito wa kuwasaidia Waafrika hao. Na idadi ya watu wanaojitolea kuwasaidia inaongezeka kila siku.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen:

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman