1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya18 Aprili 2014

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yanaziangilia sura mbili za Nigeria-ustawi wa uchumi na baa la Boko Haram. Mtafaruku katika nyoyo za Wafaransa juu ya mauaji yaliyotokea nchini Rwanda miaka 20 iliyopita.

https://p.dw.com/p/1BkrP
Matumizi ya mabavu katika mitaa ya Nigeria
Matumizi ya mabavu katika mitaa ya NigeriaPicha: SEYLLOU DIALLO/AFP/Getty Images

Gazeti la "Süddeutsche Zeitung "linazungumzia juu ya sura mbili za Nigeria: katika upande mmoja mafanikio ya kiuchumi na katika mwingine, baa la waislamu wanaoifuata itikadi kali, Boko Haram. Gazeti la "Süddeutsche Zeitung"limeandika maoni juu ya hali hiyo.

Linasema wiki iliyopita Nigeria ilitangazwa kuwa nchi ya kwanza kwa nguvu za kiuchumi barani Afrika, na hivyo imeipita Afrika Kusini. Lakini habari zilizofuatia zilikuwa juu ya maafa. Magaidi waliripua bomu kwenye kituo cha basi na kuwaua watu zaidi ya 200 katika mji mkuu Abuja.Muda mfupi baadae wasichana wa shule 100 walitekwa nyara na watu waliokuwa na silaha.

Gazeti la"Süddeutsche Zeitung" linasema matukio hayo mawili yanayokingamana, siyo jambo la kushangaza nchini Nigeria.Matukio hayo yanaonyesha hitilafu zilizomo ndani ya mfumo.

Gazeti hilo linaeleza zaidi kwamba uchumi wa Nigeria sawa na wa nchi nyingine za Afrika unastawi kwa viwango ambavyo havionekani hata katika ndoto za watu barani Ulaya. Hata hivyo ustawi huo unatokana na kuuza nje maliasilia, kama vile mafuta. Wanaonufaika na ustawi huo ni viongozi fisadi. Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita Euro Bilioni 15 zilipotea kutoka kwenye shirika la mafuta la Nigeria.Wananchi wa kawaida hawaambulii kitu.

Ufaransa na mauaji ya kimbari Rwanda

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" wiki hii linauzungumzia mtafaruku uliomo katika nyoyo za wafaransa juu ya mauaji yaliyotokea nchini Rwanda miaka 20 iliyopita.Kwa nini inakuwa vigumu kwa Ufaransa kutathmini pale iliposimama kuhusiana na mauaji hayo.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaeleza kwamba kwa Ufaransa Rwanda ni sawa na kitenzi kinachoashiria jambo lililopita, lakini linalokataa kuondoka.Tokea maafa yawakumbe watu wa Rwanda miaka 20 iliyopita, viongozi wa Ufaransa wamekuwa wanajaribu kuifuta kumbukumbu yoyote juu ya maafa hayo. Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linasema viongozi wa Ufaransa wanakwepa kuijadili dhima ya nchi yao, kabla na wakati wa mauaji ya kimbari.


Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limemnukuu Rais Paul Kagame wa Rwanda akisema wakati wa kuyakumbuka maafa ya miaka 20 iliyopita kwamba Ufaransa ilishiriki moja kwa moja katika matayarisho ya kisiasa ya mauaji ya kimbari. Gazeti hilo linasema kwa Ufaransa, Rwanda ni jeraha la moyoni.Haliondoki.

Wana wa Gaddafi

Gazeti la "die tageszeitung " limearifu kwamba watoto wawili wa Muammar Gaddafi wamefunguliwa kesi nchini Libya. Watoto wa aliekuwa dikteta wa Libya Gaddafi, walikuwa wafikishwe mahakamni jumatatu iliyopita.Lakini watoto hao Saif - al Islam na nduguye Saadi hawakutokea mahakamani.Wanakabiliwa na mashtaka ya rushwa, mauaji na wizi wa fedha za umma.

Mtetezi wa haki za walemavu


Gazeti la "Der Tagesspiegel" wiki hii limechapisha makala juu ya Rebecca Opetsi, mama mmoja mlemavu kutoka Nairobi ambae sasa anaishi nchini Tanzania. Gazeti hilo linatueleza kwamba mama huyo mwenye umri wa miaka 24 alizaliwa na ulemavu na alipoenda shule alikuwa anabaguliwa na watoto wengine.

Watoto wenzake walifikiri Rebecca alikuwa na maradhi ya kuambukiza. Lakini ana ulemavu unaotokana na hitilafu katika uti wa mgongo.Alifanyiwa upasuaji uliosababisha mguu wake upate hitilafu.

Gazeti la "Der Tagespiegel" linatilia maanani kwamba barani Afrika bado wapo watu wanaomini kwamba ulemavu ni laana. Ndiyo sababu Rebecca Opetsi ambae sasa anaishi jijini Dar Es-Salaamu anaendesha harakati za kuwasaidia watoto na wanawake wenye ulemavu kupambana na unyanyapaa. Ametoa mfano kwa kufanya masomo hadi ya chuo kikuu. Ujasiri wake unawahamasisha watu wengi na hasa watoto shuleni.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" limemkariri Rebecca akisema kuwa anataka kupambana na imani potovu juu ya ulemavu

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deustche Zeitungen.

Mhariri:Saumu Yusufu