1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

...

27 Februari 2015

Magazeti ya Ujerumani yanakumbusha kilichotokea miaka130 iliyopita katika mji wa Berlin-yaani mwanzo wa kuligawanya bara la Afrika na pia yanazungumzia juu ya kupingwa sheria ya kupambana na ugaidi nchini Kenya

https://p.dw.com/p/1EixP
Wakoloni wa Ulaya walikutana Berlin kugawana bara la Afrika
Wakoloni wa Ulaya walikutana Berlin kugawana bara laAfrikaPicha: picture-alliance/dpa

Gazeti la Süddeutsche linakumbusha juu ya mkutano uliofanyika katika mji wa Berlin miaka 130. Mkutano huo ulikuwa wa wajumbe wa nchi za Ulaya waliojadiliana juu ya kugawana bara la Afrika baina yao ili kulitawala. Katika makala iliyochapishwa na gazeti hilo la "Süddeutsche" Horst Köhler " anasema dunia inapaswa kuendelea kuukumbuka udhalimu huo.

Uchu wa Ulaya kulitaka bara la Afrika ulianza miaka130 iliyopita.

Katika makala yake Horst Köhler, aliekuwa Rais wa Ujerumani anasema uchu wa Ulaya wa kulimezea mate bara la Afrika na watu wake ulianzia kwenye mkutano huo wa Berlin. Horst Köhler anakumbusha kwamba, tarehe 26 ya mwezi wa Februari, miaka 130 iliyopita ilikuwa siku ambapo mkutano juu ya kuligawa bara la Afrika ulimalizika kwenye ofisi ya Waziri Mkuu Otto von Bismarck katika mtaa wa Wilhelm mjini Berlin.

Rais huyo mstaafu Horst Köhler anakumbuska katika makala juu ya mkutano wa kulitawala bara la Afrika kwamba ,Otto von Bismarck aliekuwa Waziri mkuu wa Mfalme wa Ujerumani ,alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo uliohudhuriwa na nchi 12 za Ulaya, pamoja na Marekani. Lengo la mkutano lilikuwa kujadili njia za kuepusha migongano baina ya wakoloni barani Afrika.

Ushindi wa watetea haki za binadamu nchini kenya

Gazeti la "die tageszeitung" limezinukulu taarifa zinazosema kuwa serikali ya Kenya imeonyeshwa kadi ya manjano. Gazeti hilo linaeleza kwamba wajumbe wa upinzani pamoja na asasi za watetezi wa haki za binadamu wamefanikiwa kuyapunguza makali ya sheria juu ya kupambana na ugaidi nchini Kenya .

Gazeti la "die tageszeitung" limearifu kwamba kutokana na shinikizo la wapinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu mahakama kuu ya Kenya imeamua kuziondoa ibara mbili zilizokuwamo katika sheria hiyo juu ya kupambana na ugaidi. Endapo ingepita kama ilivyokusudiwa na serikali ,sheria hiyo ingeliubana uhuru wa vyombo vya habari na pia idadi ya wakimbizi nchini ingeliwekewa mpaka. Maana yake ni kwamba maalfu ya wakimbizi kutoka Sudan na Somalia wangelifukuzwa nchini.

Gazeti la "die tageszeitung" linakumbusha kwamba sheria hiyo kwanza ilipitishwa mnamo mwezi wa Desemba, na ilitiwa saini haraka na Rais Uhuru Kenyatta.

Suala la ardhi laanza kutokota nchini Afrika Kusini !
Gazeti la "Süddeutsche " limechapisha makala juu ya suala la ardhi nchini Afrika Kusini. Gazeti hilo limeripoti kwamba watu weusi nchini humo wanataka ardhi igawanywe upya. Gazeti hilo limefahamisha kuwa wazalendo wanamtaka Rais Jacob Zuma achukue hatua haraka.

Gazeti la "Süddeutsche" limeeleza kwamba licha ya kung'olewa mfumo wa kibaguzi miaka zaidi ya 20 iliyopita sehemu kubwa ya ardhi yenye rutuba, bado imo katika mikono ya weupe .

Gazeti la "Süddeutsche" limefahamisha kwamba Rais Zuma ametangaza sheria mpya ya ardhi;watu kutoka nje wataruhusiwa tu kukodi ardhi na kwa wananchi,mtu mmoja ataruhusiwa kumiliki ardhi isiyozidi ukubwa wa hekta alfu 12.

Gazeti la "Süddeutsche" linaeleza kuwa suala la ardhi linaweza kuuwasha moto nchini Afrrika Kusini,kwani lilianzia mnamo mwaka 1913, wakati ambapo wabaguzi waliipitisha sheria ya ardhi ,iliyowapa watu weupe haki ya kumiliki zaidi ya asilimia 90 ya ardhi yenye rutuba.

Jee uhuru umetuletea nini

Gazeti hilo limewanukulu watu waliozaliwa baada ya kuondolewa mfumo wa kibaguzi mnamo mwaka wa 1994.Rika hilo linauliza "jee tumekipata kitu gani baada ya kuwa huru".? Tokea mwaka huo ni sehemu ndogo tu ya ardhi yenye rutuba iliyorudi katika mikono ya watu weusi nchini Afrika kusini.Wazungu bado wanamiliki sehemu kubwa ya ardhi.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed KHELEF