1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bilionea mweusi, Afrika Kusini

4 Julai 2015

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya uchaguzi wa bunge nchini Burundi na mashambulio yaliyofanywa na magaidi kaskazini mwa Afrika. Magazeti hayo pia yamendika juu ya Bilionea wa kwanza mweusi nchini Afrika Kusini

https://p.dw.com/p/1FseO
Polisi walinda usalama baada ya mashambulio ya kigaidi nchini Tunisia
Polisi walinda usalama baada ya mashambulio ya kigaidi nchini TunisiaPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Bounhar

Gazeti la "Süddeutsche" linatilia maanani kwamba uchaguzi wa bunge umefanyika nchini Burundi licha ya malalamiko makubwa na licha ya vyama vya upinzani kuususia uchaguzi huo. Gazeti la "Süddeutsche" pia linatilia maanani kwamba baadhi ya wanasiasa mashuhuri wameikimbia nchi ili kuonyesha msimamo wa kumpinga Rais Pierre Nkurunziza anaewania muhula mwingine wa urais kinyume na katiba.

Gazeti la "Neues Deutschland" pia limeandika juu ya uchaguzi wa bunge nchini Burundi na linasema ,ulifanyika katika muktadha wa ghasia.Gazeti hilo linasema utawala wa Rais Pierre Nkurunziza umepoteza imani miongoni mwa wananchi wake na duniani kote.

Mashambulio ya kigaidi Tunisia
Gazeti la "Die Zeit" limeandika juu ya mashambulio ya kigaidi,nchini Tunisia ambapo watu 38 waliangamizwa.

Gazeti hilo linatilia maanani kwamba baada ya mauaji hayo watu nchini Tunisia wamepigwa butaa,na moyo wa mapinduzi umedhoofika. Gazeti hilo pia linaizingatia hali ya utepetevu iliyojitokeza nchini baada ya mapinduzi. Habari kwamba wananchi sasa wanajiweka kando ya masuala ya siasa ni mbaya.

Tunisia sasa inaelekea kusikojulikana. Uchumi unaanguka, madeni yanaongezeka na migomo inaikwamisha nchi. Vijana waTunisia hawaoni iwapo wamefanikiwa katika harakati zao za kuleta haki na kukomesha ufisadi. Gazeti la"Die Zeit" linasema jambo baya zaidi ni kwamba idara za usalama hazifui dafu mbele ya magaidi. Hali hiyo ilithibitika Ijumaa ya wiki ya jana wakati kijana aliekuwa na umri wa miaka 23 alipowashambulia watalii kadamnasi.

Idara za usalama zimelala
Gazeti la "Die Zeit" linasema gaidi huyo,Seifeddine Rezgui aliweza kutembea umbali wa mita 200 akiwawinda watalii na kuwapiga risasi kabla ya yeye mwenyewe kuuliwa na maafisa wa usalama.

Gazeti hilo linasema polisi walikuwapo kwenye hoteli ambako kijana huyo aliwaua watu lakini limesema polisi hao walikuwa wanawasaka makobe wa mchana-wasiofunga mwezi wa Ramadhani.

Gazeti la "Süddeutsche" linaarifu juu ya wanajeshi na polisi zaidi ya 60 wa Misri waliouliwa kwenye rasi ya Sinai siku ya Jumatano. Magaidi wanaoitwa dola la kiislamu walidai kuhusika na mashambulio hayo. Gazeti la "Südeutsche" linasema shambulio hilo ni kubwa kabisa kuwahi kufanywa na magaidi nchini Misri mnamo muda mfupi wa siku tatu.

Gazeti hilo limeandika juu ya hali mbaya ya usalama kwenye rasi ya Sinai. Limezikariri taarifa za vyombo vya habari vya nchini Misri zinazosema kuwa ,licha ya kuwepo idadi kubwa ya wanajeshi katika sehemu hiyo,magaidi wanafanikiwa kufanya mashambulio mara kwa mara.

Bilionea wa kwanza Mwafrika nchini Afrika Kusini

Gazeti la "NZZ" wiki hii linamtambulisha Patrice Motsepe kutoka Afrika Kusini.Yeye ni Bilionea wa kwanza mwafrika nchini humo.

Gazeti hilo linaarifu kwamba Motsepe alianza kuyajua mambo ya biashara tokea alipokuwa na umri wa miaka sita. Wakati huo alikuwa anamsaidia baba yake kuuza dukani. Wateja wengi walikuwa wafanyakazi wa migodi. Na hapo ndipo alipoanza kuvutiwa na mambo ya migodi. Baada ya masomo ya shahada ya kwanza nchini Swaziland na ya sheria nchini Afrika Kusini Motsepe alianza kumiliki kampuni ya madini-African Rainbow Minerals.

Gazeti la "NZZ" linafahamisha zaidi kwamba Motsepe mwenye utajiri unaokadiriwa kufikia dola Bilioni 2.9 anakusudia kutoa nusu ya utajiri huo kwa ajili ya kuwasaidia masikini. Tajiri huyo alizaliwa katika kitongoji cha Soweto mnamo mwaka 1962.

Gazeti la "NZZ" linaaarifu kwamba Motsepe alitoa mchango wa mamilioni ya dola kwa ajili ya harakati za kupambana na maradhi ya Ebola.

Mwandishi: Mtullya abdu./Deutsche Zeitungen:

Mhariri: Yusuf Saumu