1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pia barani Afrika wako wakimbizi

21 Septemba 2015

Wiki hii gazeti la "Süddeutsche" linakumbusha kwamba mzigo wa wakimbizi haubebwi na bara Ulaya tu. Linasema pia nchini Kenya ,Uganda na Tanzania wako wakimbizi kutoka nchi jirani

https://p.dw.com/p/1GZbR
Rais wa Gambia Yahya Jammeh
Rais wa Gambia Yahya JammehPicha: AFP/Getty Images

Gazeti la "Süddeutsche linakumbusha kwamba siyo bara la Ulaya tu linaloubeba mzigo wa wakimbizi katika dunia hii.Linasema katika muktadha wa idadi kubwa ya wakimbizi wanaokimbilia Ulaya, dunia inasahau kwamba wapo mamilioni ya wakimbizi wanaokimbilia Kenya kutoka nchi jirani zenye migogoro.

Gazeti la "Süddeutsche" linafahamisha kwamba mpaka sasa Umoja wa Ulaya umeshatenga Euro karibu Bilioni nne kwa ajili ya wakimbizi wa Syria.Linatilia maanani kwamba hali siyo ya kawaida katika Mashariki ya kati na barani Ulaya kuhusu wakimbizi.


Lakini gazeti hilo linasema dunia ni kubwa zaidi. Limezikariri takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi,UNHRC, zinazoenyesha kwamba wapo maalfu kwa maalfu ya wakimbizi kutoka Somalia waliopatiwa hifadhi kwenye kambi ya Dadaab nchini Kenya, inayohesabika kuwa kubwa kabisa duniani inayowahifadhi wakimbizi ,300,000.


Gazeti la "Südeutsche" pia linakumbusha kwamba, kwa miaka mingi sasa ,Tanzania na Uganda pia zimekuwa zinatoa mchango katika kuwahudumia wakimbizi kutoka Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo na Burundi.

Gazeti la "Südeutsche" pia linauliza kwa nini Mwendesha mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague,Fatou Bensouda hasemi chochote juu ya nchi yake Gambia.

Yahya Jammeh 02/2014
Picha: picture-alliance/AP/Sunday Alamba

Gazeti la "Süddeutsche " linaeleza kwamba Besouda anahesabika kuwa mtu mashuhuri duniani katika mambo ya sheria lakini hasemi lolote juu ya utawala wa Rais Yahya Jammeh anaewafunga watu jela kwa sababu ya mambo ya uchawi

Gazeti hilo linasema Rais huyo wa Gambia Jammeh hivi karibuni alitoa wazo la kuushtaki Umoja wa Ulaya mbele ya mahakama ya mjini the Hague kwa kosa la kusababisha vifo vya wakimbizi kutoka Afrika kwenye bahari ya Mediterania.

Gazeti la "Süddeutsche" linasema Rais Jammeh ni dikteta mkubwa na limeyanukulu mashirika ya kutetea haki za binadamu yakisema kwamba utawala wake ni wa kuwatisha watu na kwamba hana stahamala kwa watu wenye maoni yanayotafautiana na yake. Gazeti la "Süddeutsche" linauliza kwa nini mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Bensouda anaetokea Gambia hasemi chochote juu ya udhalimu wa Rais Jammeh? Gazeti hilo linakumbusha kwamba Bibi Besouda aliwahi kuwa waziri katika serikali ya Gambia.

Jarida la "Focus" wiki hii limeripoti juu ya matumaini ya kusonga mbele barani Afrika.

Jarida hilo linaeleza kwamba kwa muda mrefu bara la Afrika lilikuwa linazingatiwa na kampuni za Ujerumani kuwa bara la maradhi,migogoro na ufisadi lakini sasa kampuni hizo zimeyagundua masoko katika nchi za kusini ya jangwa la Sahara.


Jarida la "Focus" limeripoti kwamba hisia za kupambazuka zilionekana miongoni mwa mameneja wa kampuni za Ujerumani waliokutana hivi karibuni. Jarida hilo linasema baada ya mauzo ya bidhaa za Ujerumani kupungua nchini China, kampuni za Ujerumani sasa zinatafuta masoko kwingineko.Swali jee ni Afrika?


Jarida la "Focus" limemnukulu meneja wa kampuni ya kutengeneza mashine akisema anatumai baada ya muda mfupi tu kampuni yake itauza mashine nyingi katika nchi za Afrika. Jarida hilo limefahamisha kwamba kampuni za Ujerumani zinauza barani Afrika bidhaa thamani ya Euro Bilioni 23 na zinakusudia kuziboresha zaidi bidhaa hizo ili kushindana na China.


Mtaalamu wa masuala ya biashara baina ya Afrika,na Ujerumani, Friedrich Wagner amekaririwa na jarida la "Focus" akisema kwamba katika kipindi cha miaka 10 ijayo biashara baina ya kampuni za Ujerumani na Afrika itaongezeka kwa asilimia hadi 70.

Mwandishi:Mtullya Abdu.

Mhariri:Yusuf Saumu