1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Barclays asilia yafunga virago Afrika

4 Machi 2016

Magazeti ya Ujerumani wiki yameandika juu ya kuondoka barani Afrika kwa Benki ya Uingereza , Barclays na juu ya harakati za kupambana na Ebola

https://p.dw.com/p/1I7Wf
Nembo ya Barclays
Nembo ya BarclaysPicha: Getty Images/AFP/L.Venance

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine"limechapisha makala juu ya Benki kongwe ya Barclays iliyotangaza kuwa itafunga virago na kuondoka barani Afrika.Baada ya miaka mingi benki hiyo imetangaza kuwa itafunga virago na kuondoka.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaeleza kwamba hadi miaka ya hivi karibuni tu aliekuwa mkuu wa Benki hiyo Bob Diamond alilisifu bara la Afrika kuwa soko lenye kiwango kikubwa cha ustawi. Lakini sasa mkuu mpya ameamua kufunga virago.

Baada ya uvumi wa miezi kadhaa,Benki hiyo imeamua kusema buriani na kuuza sehemu ya hisa zake kwa Barclays ya Afrika-"Barclays Africa Group"

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limearifu kwamba mchakato huo wa kuuziana hisa utachukua miaka miwili hadi mitatu. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba ,taa ya benki hiyo itaendelea kuwapo barani Afrika lakini utambi wake umezimika!

Gazeti la "Franfurter Allgemeine" linaarifu kwamba nchini Afrika Kusini wateja walianza kuingiwa taharuki kutokana na uvumi juu ya Benki ya Barclays kufunga shughuli zake barani Afrika. Hisa zilianguka kwenye soko la hisa la mjini Johannesburg.

Benki ya "Barclays Africa Group " itaendelea kutoa huduma Afrika

Gazeti "Frankfurter Allgemeine" limemnukulu mkuu wa Barclays Afrika Group Maria Ramos akijaribu kuwatuliza wawekaji vitega uchumi nchini Afrika Kusini. Maria Ramos amenukuliwa akisema kwamba Benki yake ya "Barclays Afrika Group" itaendelea kuwahudumia wateja Milioni 12 katika nchi 12 za Afrika.

Gazeti la "Frankfuter Allgemeine" linaeleza kwamba Benki ya Barclays asilia ya Uingereza imefunga virago Afrika kutokana na masharti magumu yaliotolewa na Umoja wa Ulaya na pia kutokana na bei za malighafi kuanguka.

Gazeti la "Der Tagesspiegel" linazungumzia juu ya hatua iliyopigwa katika harakati za kupambana na maradhi ya Ebola.

Madaktari wakipambana na Ebola
Madaktari wakipambana na EbolaPicha: Getty Images/AFP/F. Leong

Gazeti hilo linafahamisha kwamba watafiti wamefanikiwa kuipata sehemu ya damu ya mtu aliewahi kukumbwa na ugonjwa huo, inayoweza kutumiwa katika kupambana nao. Gazeti hilo linaeleza kwamba mtu huyo alilazwa hospitalini akiwa taabani , kwa muda wa wiki nzima, lakini alipona.

Miaka 11 baadae alipimwa damu kwa hiari yake na watafiti waliweza kubainisha kwamba sehemu ya damu ya mtu huyo inaweza kutumika kama kinga dhidi ya maradhi ya Ebola yaani "antibody"

Gazeti "Der Tagesspiegel" linakumbusha kwamba kutokana na mlipuko wa maradhi ya Ebola katika nchi za Afrika magharibi watu 28,639 waliambukizwa na kati ya hao 11,316 walifuka.

Kasisi afurahia kapu la fedha

Gazeti la "Süddeutsche " linatupeleka Uganda. Safari hii halimzunguzii Yoweri Museveni bali Kasisi Joseph Serwadda.

Gazeti hilo linatupasha kuwa Kasisi Serwadda aliwaambia Waganda kwamba watakipata kile wanachokitaka mnamo mwaka huu wa 2016. Amesema Mungu atazitimiza ndoto zao.

Aliwauliza watu iwapo wanataka kuhamia Ulaya. Hakuna kinachoweza kumshinda Mungu, kasisi Serwadda aliwaambia watu. Gazeti la "Süddeutsche" linaarifu kwamba baada ya kutoa ahadi hizo kasisi huyo aliweka kapu kubwa chini na kuwaambia watu watoe fedha kwa ajili ya Mungu. Watu walisongamana na kuanza kulizaja fedha kapu hilo.


Licha ya kuwa Kasisi Dr. Joseph Serwadda anaamini kuwa mganga mwenye miujiza. Gazeti la "Süddeutsche" limemnukulu mtaalamu wa historia kutoka chuo kikuu cha Makerere Katono Nzwarwa akieleza kwa nini watu wanaamini anachosema kasisi huyo na kumjazia fedha kapu lake.

Mtaalamu huyo ameeleza kwamba ,kutokana na umasikini watu wanajenga imani juu ya miujiza inayoweza kuwaondolea shida zao. Mtaalamu huyo amesema kazi hiyo ya kufanya miujiza inatimizwa vizuri na makasisi kama Joseph Serwadda kwa kulitumia jina la Mungu.

Mwandishi:Mtullya Abdu/Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Yusuf Saumu