1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matajiri hawalipi kodi Afrika

22 Mei 2016

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya ushirikiano wa siri na watawala dhalimu na juu ya matajiri wasiolipa kodi barani Afrika pia yanalalamika kwamba Ujerumani inashirikiana na wadhalimu

https://p.dw.com/p/1IsZq
Ishara ya ufisadi: Panama Papers
Ishara ya ufisadi: Panama PapersPicha: picture-alliance/dpa/U. Zucchi

Gazeti la "Neues Deutschland" limeandika juu ya matajiri wakubwa wa barani Afrika wasiolipa kodi. Gazeti hilo linaeleza kwamba idadi ya matajiri wakubwa barani Afrika inaongezeka. Lakini matajiri hao hawalipi kodi.

Nchini Kenya ni matajiri 100 tu waliosajiliwa kati ya 40,000. Afrika Kusini inapoteza Euro Bilioni 9.7 kila mwaka kwa sababu matajiri hawalipi kodi.

Gazeti la "Neues Deutschland" linafahamisha kwamba nchini Afrika Kusini wapo matajiri wakubwa 114,000 ambao hawajasajiliwa . Gazeti hilo linasema juhudi za kupambana na ufisadi huo barani Afrika zinashindikana kwa sababu matajiri hao wana usemi mkubwa katika siasa za nchi zao.

Gazeti la "Neues Deutschland" limezikariri takwimu za shirika la utafiti la "New World Wealth" zinazoonyesha kwamba, watu wenye utajiri unaovuka dola Milioni moja barani Afrika wameongezeka mara mbili katika kipindi cha miaka 15 iliyopita.

Matajiri hao wakubwa wapatao 165,000 barani Afrika kwa pamoja wanao utajiri wa dola Bilion 860 .

Matumaini yaliyopungua

Gazeti la masuala ya kibiashara"Handelsblatt" linazungumzia juu ya matumaini yaliyozama katika nchi za Afrika. Na ili kuthibitisha kuzama kwa matumaini hayo gazeti hilo linasema Waafrika wengi wameacha kujiburudisha kwa vinywaji kama "Castle lager" kwenye mikahawa. Badala yake wafanyakazi wanajiburudisha kwa pombe zinazoitwa za kienyeji.

Almasi kubwa kabisa nchini Botswana
Almasi kubwa kabisa nchini BotswanaPicha: picture-alliance/dpa/Lucara Diamond Corp / Handout

Gazeti hilo linawazungumzia wafanyakazi wa nchini Botswana. Linasema hali hiyo inatokana na kuanguka kwa bei za malighafi duniani.

Gazeti la "Handelsblatt " linaeleza kwamba katika machimbo ya almasi ya mji wa Jwaneng, kilometa 120 kutoka mji mkuu, Gaborone, karati zaidi ya Milioni moja za almasi zinazalishwa kwa mwaka. Lakini gazeti hilo linasema biashara inaenda vibaya kwenye soko la dunia.

Gazeti la Handelsblatt linaeleza kwamba kurudi katika viburudisho vinavyoitwa vya kienyeji, kunathibitisha kushuka kwa utashi barani Afrika. Mfano wa Botswana gazeti linasema unawakilisha bara lote la Afrika!

Gazeti la Handelsblatt linakumbusha kwamba katika miaka ya hadi hivi karibuni ustawi wa uchumi ulikuwa unafikia hadi asilimia 7 katika bara la Afrika .Lakini limeukariri utabiri wa Shirika la Fedha la Kimataifa,IMF, unaosema kuwa mnamo mwaka huu ustawi wa uchumi utarudi nyuma hadi kufikia asilimia 3 tu.

Ushirikiano wa siri na wadhalimu

Jarida la "Der Spiegel" linafahamisha kwamba serikali ya Ujerumani inashirikiana na watawala dhalimu ili kuwazuia wakimbizi kuingia barani Ulaya. Jarida hilo linaeleza kuwa mabalozi wa nchi 28 za Umoja wa Ulaya walikutana kwa faragha mnamo mwezi wa Machi kuzungumzia mradi wa siri.

Kwa mujibu wa jarida la "Der Spiegel" mabalozi hao walikubaliana juu ya kushirikiana na madikteta wa pembe ya Afrika ili kuweza kuwazuia wakimbizi kwenda katika nchi za Ulaya.

Jarida la "Der Spiegel" limemnukulu msemaji wa Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya akieleza kwamba mradi huo ni wa siri kubwa na ikiwa utafichuka Umoja wa Ulaya utaumbuka. Jarida hilo linafahamisha kwamba nchi nane zimetengewa kiasi cha Euro Milioni 40 kutoka kwenye mfuko wa dharura wa Umoja wa Ulaya.

Chini ya uongozi wa Ujerumani nchi za Umoja wa Ulaya zitazipa nchi hizo nane za Afrika pia zana za kisasa kwa ajili ya kuwadhibiti wakimbizi kwenye mipaka.

Mradi huo utaongozwa na shirika la Ujerumani la ushirikiano wa kimataifa GIZ. Jarida la "Der Spiegel " limeripoti kwamba wanaolengwa ni wakimbizi kutoka Eritrea,Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaopitia Sudan ili kwenda Ulaya.

Mwandishi:Mtullya Abdu.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman