1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Binadamu wanahitaji dunia tatu kujitosheleza kwa mahitaji

18 Julai 2016

Magazeti ya Ujerumani mnamo wiki hii yameandika juu ya wakimbizi wanaotolewa viungo vya mwili na juu ya uhaba wa raslimali duniani

https://p.dw.com/p/1JQa9
Wakimbizi kwenye bahari ya Mediterania
Wakimbizi kwenye bahari ya MediteraniaPicha: Reuters/D.Z. Lupi

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaarifu juu ya maafa yanayowafika wakimbizi kutoka Afrika, kwenye bahari ya Mediterania. Gazeti hilo linasema njia inayotumiwa na wakimbizi hao Afrika, ya kupitia Libya ili kufika barani Ulaya ni ya hatari kubwa sana.

Watolewa viungo vya mwili

Gazeti hilo linasema mamia ya watu hao wanakufa njaa kila mwaka wakati wa kuvuka jangwa.Linasema wengine wanatekwa nyara na kugeuzwa watumwa, na wale wanaoshindwa kuwalipa wasafirishaji wanauzwa nchini Misri ambako wanatolewa viungo vya mwili. Viungo hivyo vinauzwa ili kulipia gharama zao kwa wafasirishaji haramu.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limemnukulu msafirishaji mmoja aliefikishwa mahakamani nchini Italia akieleza kwamba ,kabla ya kutolewa viungo vya mwili wakimbizi hao wanauliwa na wale wanaowanunua nchini Misri.

Gazeti la "Berliner" linatahadharisha juu ya athari zinazotokana na kuongezeka idadi ya watu duniani na linaeleza, kuwa hali hiyo inazifanya harakati za kupambana na njaa ziwe ngumu. Limeyakariri mashirika ya misaada yakisema kwamba haitoshi kugawa misaada ya chakula ili kulitaua tatizo la njaa.

Gazeti hilo linasema mazingira yanayosababisha njaa yamebadilika barani Afrika pia. Linasema pamoja na ukame,mafuriko na mitetemeko ya ardhi, migogoro ya kivita pia inasababisha idadi kubwa sana ya wakimbizi wanaohitaji kusaidiwa.

Gazeti la "Berliner" linatoa mfano wa Sudan Kusini ambako linasema mipango ya kugawa chakula kwa maalfu ya wakimbizi, haileti tija tena katika kulitatua tatizo la njaa.

Vita vyazuka tena Sudan Kusini

Gazeti la " die tageszeitung" wiki hii linakumbusha kwamba mafahali wawili wanapopambana ni nyasi zinazoumia.

Wakimbizi wakisubiri kuhamishwa Sudan Kusini
Wakimbizi wakisubiri kuhamishwa Sudan KusiniPicha: Reuters/J. Solomun

Gazeti hilo linaizungumzia hali ya Sudan Kusni. Linaeleza kwamba mwaka mmoja baada ya mkataba wa amani kutiwa saini, vita vimezuka tena Sudan Kusini. Gazeti la "die tageszeitung" linaeleza kuwa katika muktadha wa nchi hiyo, mafahali wawili ni Rais Salva Kirr na makamu wake Riek Machar, na nyasi ni wananchi.

Gazeti hilo linasema mapigano baina ya majeshi ya viongozi hao wawili yanaifanya hali ya wananchi izidi kuwa mbaya. Kwani tayari nusu ya wananchi Milioni 11 wa nchi hiyo wanasibika na njaa. Gazeti la "die tageszeitung" limemnukuku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akisema , wanachokifanya Rais Salva Kirr na makamu wake ni kuwasaliti wananchi wao.

Gazeti hilo linaarifu kwamba watu Milioni 2 wa Sudan Kusini wanaishi katika kambi za wakimbizi, uchumi umesambaratika na watu hawawezi kuendesha shughuli za kilimo.

Kadri idadi ya watu inavyoengezeka duniani ndivyo nyenzo za kuendeshea maisha zinavyozidi kupungua. Hali hiyo inalihusu pia bara la Afrika linasema gazeti la "Der Tagesspiegel"

Gazeti hilo linaeleza kwamba karibuni tu dunia itashindwa kukidhi mahitaji yake.Linasema ongezeko la watu ni kubwa hasa katika nchi zinezoendelea. Barani Afrika idadi ya watu imeongezeka ambako asilimia 16 ya binadamu wanaishi.

Gazeti "Der Tagesspiegel" linatoa mfano wa Niger ambako kila mwanamke kwa wastani anazaa watoto wanane. Hata hivyo gazeti hilo linaeleza kwamba sababu ya wanawake katika nchi zinazoendelea , ikiwa pamoja na barani Afrika ,kutaka watoto wengi ni kujijengea mfumo wa pensheni, kwani watoto ndiyo wanaowaangalia wazazi wao wanapozeeka.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri:Iddi Ssessanga