1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz
18 Agosti 2017

Wiki hii magazeti ya Ujerumani yamechapisha habari juu ya maafa yaliyotokea nchini Sierra Leone, mashambulio mengine ya kigadi nchini Burkina Faso na magazeti yameripoti kuhusu sakata linalomkabili Grace Mugabe.

https://p.dw.com/p/2iS5x
Sierra Leone Freetown nach dem Erdrutsch
Picha: Imago/Xinhua

Ripoti iliyochapishwa na gazeti la Frankfurter Allgemeine juu ya msiba mkubwa uliowafika watu wa Sierra Leone.  Mamia ya watu wamekufa kutokana na maporomoko ya ardhi yaliyosababishwa na mvua kubwa sana iliyoleta mafuriko hayo.  Idadi kubwa ya watu waliokufa walikumbwa na maporomoko ya udongo katika mji mkuu wa Sierra Leone, Freetown.  Vijiji vilizolewa na kufunikwa chini ya matope mazito.

Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linasema, hadi sasa hakuna maelezo ni kwa nini idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini Sierra Leone haikutoa taarifa za kuwatahadharisha wananchi juu ya mvua kubwa zilizokuwa zinajikusanya? Gazeti hilo linatilia maanani kwamba miezi ya Agosti na Septemba ni msimu wa mvua kubwa zinazosabisha mafuriko.

Mashambulio ya kigaidi

Gazeti la Die Welt limeripoti juu ya mashambulio mengine yaliyofanywa na magaidi nchini Burkina Faso.  Gazeti hilo linasema nchi hiyo inaandamwa na magaidi kutoka sehemu mbalimbali za dunia.  Gazeti hilo la Die Welt linasema magaidi walifyatua risasi kila upande na kuwaua watu zaidi ya 20 ndani na karibu ya mkahawa wa Kituruki katika mji mkuu wa Burkina  Faso, Ouagadougou.  Gazeti hilo la Die Welt linakumbusha kwamba mashambulio hayo ya kigaidi yanafanana na yale yaliyofanyika mnamo mwezi Januari mwaka uliopita ambapo magaidi wa kundi la Al - Qaida waliwaua watu 30 karibu na hoteli ya Splendid katika mji wa Ouagadougou,

Gazeti la Die Welt linaendelea kueleza sababu kadhaa za kushambuliwa kwa Burkina Faso.  Mojawapo ni kuongezeka kwa ugaidi kaskazini mwa nchi hiyo.  Gazeti linasema magaidi waliowashambulia watu kwenye hoteli ya Splendid mwaka uliopita walitoka nchi za nje lakini safari hii pana uwezekano mkubwa kwamba wauaji hao walitokea ndani ya Burkina Faso.  Gazeti hilo la Die Welt linatilia maanani kwamba magaidi wanakwenda Kaskazini mwa nchi hiyo ambako watu wameikasirikia serikali kwa sababu ya kutenga fedha kidogo kwa ajili ya maendeleo ya sehemu yao.

Umoja wa Ulaya

Na gazeti la Handelsblatt limeripoti  kwamba Umoja wa Ulaya unatafakari wazo la kuanzisha Umoja wa Forodha na nchi za Afrika Kaskazini.  Gazeti hilo linaeleza kuwa mpango huo unakusudia kuutatua mgogoro wa wakimbizi wanaotokea Afrika.

Gazeti hilo la Handelsblatt linafahamisha kwamba kansela wa Ujerumani Angela Merkel alitumia fursa ya uenyekiti wa mkutano wa kundi la nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani  (G 20) kuhamasisha juhudi za kushughulikia kiini au sababu za mgogoro wa wakimbizi kutoka barani Afrika. Gazeti hilo limemnukulu kansela Merkel akisema ikiwa hali ya kukatisha tamaa inaendelea kutanda barani Afrika ni wazi kuwa vijana wa bara hilo watayatafuta matumaini kwingineko.

Gazeti la Handelsblatt linasema kwingineko maana yake ni barani Ulaya.  Gazeti hilo limezikariri takwimu za shirika la kimataifa la uhamiaji IOM zinazoonyesha kwamba takriban wahamiaji wote laki moja na themanini alfu waliovuka bahari ya Mediterania mwaka jana ili kufika Ulaya walikuwa watu kutoka nchi za Afrika wanaotafuta maslahi ya kiuchumi.  Gazeti hilo linaloshughulikia maswala ya kiuchumi limetabiri kwamba idadi ya wahamiaji kutoka nchi za Afrika itaongezeka barani Ulaya kutokana na ongezeko kubwa la watu katika nchi za Afrika.

Grace Mugabe

Gazeti la Die Tageszeitung linasema sheria si msumeno kwa mke wa rais wa Zimbabwe Robert Mugabe. Gazeti hilo linaripoti kwamba Grace Mugabe pamoja na wanawe walifanya fujo mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini. Gazeti hilo la Die Tageszeitung linafahamisha kwamba Grace Mugabe alimshambulia kwa kumchapa mwanamitindo wa Afrika Kusini Gabriella Engels kwa kutumia waya na kumjeruhi usoni.  Mrembo huyo alikuwa amewatembelea watoto wa Mugabe kwenye hoteli moja ya kifahari ya mjini Johannesburg lakini bibi Grace Mugabe aliwaamuru walinzi wake wamfurushe dada huyo.

Gazeti hilo la Die Tageszeitung limesema, mwanamitindo huyo alimripoti bi Grace Mugabe kwa polisi lakini mama huyo hakukamatwa sababu ni kwamba yeye anayo kinga ya kidiplomasia sawa na mumewe rais Mugabe.  Gazeti hilo linafahamisha kwamba mke wa rais Mugabe alienda Afrika Kusini kutibiwa mguu kwa gharama za serikali wakati nchini Zimbabwe watu wanakufa sababu hakuna dawa mahospitalini.

Mwandishi: Zainab Aziz/Frankfurter Allgemeine/Die Welt/Handelsblatt/Die Tageszeitung

Mhariri:Iddi Ssessanga