1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz
10 Novemba 2017

Gazeti la Südeutsche Zeitung lasema rais Mugabe amfagilia mke wake.Mgombea urais nchini Liberia Joseph Boakai amtuhumu mshindani wake George Weah kwamba anawasiliana na rais wa zamani Charles Taylor.

https://p.dw.com/p/2nQUB
Simbabwe Robert Mugabe mit Ehefrau Grace in Harare
Picha: Reuters/P. Bulawayo

Makala ya gazeti la Südeutsche yanagusia juu ya hatua iliyochukuliwa na Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe ya kumfukuza makamu wake Emmerson Mnangagwa. Gazeti hilo linasema kila kitu nchini Zimbabwe kitabakia kwenye mikono ya familia ya Mugabe. Sababu ni kwamba Grace Mugabe anataka kurithi kiti cha mumewe na mama huyo haifichi dhamira yake ya kutaka kuwa rais wa Zimbabwe.

Hapo Jumatatu, hadharani alitaka makamu wa rais Emmerson Mnangagwa afukuzwe na kweli muda mfupi tu baadaye Mnangagwa alitimuliwa. Hata hivyo gazeti hilo la Süddeutsche linasema kutimuliwa kwa mwanasiasa huyo mkongwe kunaweza kuwa hatari kwa familia ya Mugabe. Gazeti hilo linaeleza kuwa Mnangagwa bado anaungwa mkono na mashujaa wa vita vya ukombozi. Nalo gazeti la die tageszeitung linatilia maanani kwamba kwa kumfukuza makamu wake, Rais Mugabe amekiondoa kizingiti kingine ili kumfagilia njia mkewe ya kumfikisha kwenye kilele cha mamlaka nchini Zimbabwe.

Fussball WM 2010  Qualifikationsgruppen - Auslosung Georg Weah
Mgombea wa urais nchini Liberia mwanasoka maarufu George WeahPicha: picture-alliance/dpa/Pressefoto ULMER/M. Ulmer

Der Spiegel

Jarida la Der Spiegel wiki hii linazungumzia juu ya madai yaliyotolewa na mgombea urais wa nchini Liberia Joseph Boakai ambaye ni makamu wa rais wa Liberia. Boakai ameliambia jarida hilo la Der Spiegel kwamba mshindani wake katika kinyang'anyiro cha kugombea urais George Weah anawasiliana na aliyekuwa rais wa Liberia Charles Taylor anayetumikia kifungo cha miaka 50 kwenye jela ya nchini Uingereza baada ya kupatikana na hatia ya kutenda uhalifu wa kivita nchini mwake. Boakai ameliambia jarida hilo kwamba endapo Goerge Weah, aliyekuwa mwanasoka maarufu duniani, atashinda uchaguzi, atawapa madaraka katika serikali yake washirika wa Taylor na hususan aliyekuwa mke wa Taylor.

Joseph Kabila Präsident der Demokratischen Republik Kongo
Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Joseph KabilaPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Uchaguzi wa Jamuhuri ya Kidemiokrasia ya Kongo

Na katika makala yake nyingine wiki hii gazeti la die Tageszeitung linafahamisha kwamba uchaguzi wa rais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliopaswa kufanyika muda mrefu uliopita sasa umepangiwa kufanyika mwaka ujao. Gazeti hilo linaeleza kuwa Baba Krismasi, ambaye ni rais Joseph Kabila atajitokeza mwaka ujao. Tume huru ya uchaguzi  imetangaza katika mji mkuu wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa, kwamba uchaguzi wa rais utafanyika tarehe 23 Desemba mwaka 2018. Hata hivyo tume hiyo wakati wote imeweza kutumia mbinu za kuhakikisha kwamba daftari la wapiga kura kila mara linapitwa na wakati.

Gazeti hilo la die Tageszeitung limeeleza kwamba wanapoanza kuzunguka nchini kote ili kuwaorodhesha watu, wajumbe wa tume ya uchaguzi huchukua muda wa miaka kadhaa na wanapomaliza zoezi hilo, daftari la wapiga kura linakuwa limeshapitwa na wakati. Gazeti hilo linaeleza kwamba kutokana na changamoto za kisheria, kisiasa, kifedha na za miundombinu, wachunguzi wengi wana mashaka iwapo uchaguzi kweli utafanyika mwezi Desemba mwaka ujao katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mtihani wa kwanza umeshajitokeza. Hadi mwishoni mwa mwezi wa Novemba bunge la nchi hiyo linatakiwa lipitishe sheria mpya ya uchaguzi.

Shinikizo la kimataifa

Gazeti hilo pia linaeleza kwamba kutokana na shinikizo la jumuiya ya kimataifa tume ya uchaguzi ya nchini Kongo inaligeuza shinikizo hilo kuwa mtaji na kusema kwamba ikiwa uchaguzi utaandaliwa kufanyika siku hiyo basi jumuiya ya kimataifa itapaswa kubeba gharama zote!

Vietnam Dak Lak Elefant
NdovuPicha: Getty Images/AFP/H. Dinh Nam

Na gazeti la Die Zeit linakumbusha juu ya hatari ya kutoweka kwa ndovu wanaouliwa na majangili kwa sababu ya meno yao barani Afrika. Gazeti hilo linafahamisha kwamba, kila baada za dakika 20 anauliwa tembo mmoja. Gazeti la Die Zeit linatahadharisha juu ya hatari ya kutoweka kwa wanyama hao barani Afrika, ikiwa walinzi wa wanyama pori hawatafanikiwa kuwashinda majangili lakini gazeti hilo la Die Zeit linasema sasa yapo matumaini kutoka China nchi iliyokuwa soko kubwa la biashara ya vipusa. China imetoa uamuzi wa kulifunga soko hilo hapo mwakani na kwamba tayari bei ya meno ya ndovu imeanguka kwa thuluthi mbili nchini China.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Josephat Charo