1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz
24 Novemba 2017

Wiki hii magazeti yametilia maanani mabadiliko yaliyotukia nchini Zimbabwe yanasema Emmerson Mnangagwa aliyechukua nafasi ya Robert Mugabe kwa  muda mrefu alikuwa kiranja katika mfumo wa kidikteta nchini humo.

https://p.dw.com/p/2oDZ9

Gazeti la Süddeutsche limeandika kwamba chini ya utawala wa Mugabe Mnangagwa alikuwa mkuu  wa shirika la ujasusi na pia waziri wa sheria. Watetea haki za binadamu nchini  Zimbabwe  wanasema Mnangagwa alihusika na mauaji ya maalfu ya watu yaliyofanyika katika jimbo la Matabeleland mnamo miaka ya 80. Gazeti hilo linaeleza kwamba kutokana na unyama alioufanya, watu wa Zimbabwe wamempa Mnangawa jina la mamba. Hatahivyo gazeti hilo la Süddeutsche limemnukuu shujaa huyo wa vita  vya ukombozi akisema yuko tayari kuleta mabadiliko ya amani na kuimarisha demokrasia.

Robert Mugabe und Grace Mugabe
Robert Mugabe na Mkewe Grace enzi zaoPicha: Getty Images/J.Njikizana

Gazeti la  Der Spiegel pia limeandika juu ya tufani la kisiasa lililoikumba familia  ya  Mugabe. Linasema utawala wa Gucci umefikia mwisho baada ya miaka 37 likiwa na maana ya mtindo wa maisha ya mke wa Mugabe, Grace na watoto wake. Lakini kuhusu mabadiliko yaliyotokea mtu hana uhakika iwapo yataleta demokrasia na uhuru nchini Zimbabwe.

Nalo gazeti la  Die Welt wiki hii linatanabahisha  juu  ya njia mpya inayotumiwa sasa na wakimbizi kwenda Ulaya. Njia  hiyo ni Morocco na limemnukuu  Mkameruni mmoja, Patou Sedrick  akisema hajawahi kuona boti nyingi zilizojaa  wakimbizi  kama anazoziona a sasa nchini Morocco zikianza  safari kutokea kila upande. Gazeti la Die Welt linaeleza kuwa kijana huyo mwenyewe aliwahi kuwa mkimbizi na aliyosema yanathibitisha takwimu za shirika la kimataifa la uhamiaji-IOM. Wakimbizi wapatao 18,000 waliwasili nchini Uhispania tangu mwanzoni mwa mwaka huu kwa kutumia mashua.

Wakimbizi huko Tripoli, Libya
Wakimbizi katika boti nchini LybiaPicha: Reuters/H. Amara

Kulinganisha na  mwaka  uliopita idadi  hiyo maana yake ni ongezeko la mara tatu. Njia ya hapo  awali ambayo ni Libya ilifungwa kuanzia mwezi wa Julai baada ya Italia kuchukua hatua. Serikali ya nchi hiyo ilitoa fedha na misaada mingine yenye thamani ya mamilioni kwa serikali ya Libya na  tangu wakati huo hakuna wakimbizi wanaotumia njia hiyo ya Libya. Dunia nzima ilishtushwa  na habari  juu  ya masoko ya watumwa nchini  Libya. Watumwa hao wanatoka nchi kadhaa za Afrika.

Katika makala yake  wiki hii gazeti  la die  tageszeitung limeuzingatia mkasa huo na linaeleza kwamba wimbi la ghadhabu lilienea barani Afrika kote baada ya shirika la televisheni la Marekani CNN kuonyesha jinsi waafrika walivyokuwa wanapigwa mnada kwenye masoko nchini Libya kuanzia dola mia nne. Gazeti hilo la die tageszeitung limeeleza kwamba maripota wa CNN walipatiwa ukanda wa video uliokuwa unaonyesha jinsi vijana 12 kutoka Niger walivyokuwa wanauzwa.

Koffi Olomide
Koffi Olomide Mwanamuziki gwiji wa barani AfrikaPicha: Getty Images/AFP/Seyllou

Habari hizo zilienea  haraka barani  Afrika na kuwafanya wasanii mahiri  waje  juu  ikiwa pamoja na Alpha Blondy,Youssou N~Dour na  Koffi Olomide. die tageszeitung limeandika kwamba viongozi  wa Afrika walifuatia  kwa kutoa kauli zao. Mwenyekiti  wa  sasa  wa Umoja wa  Afrika Alpha Conde ameitaka  serikali ya  Libya ichukue hatua mara moja. Niger inataka  mkasa huo ujadiliwe kwenye mkutano wa  viongozi wa Umoja wa Afrika na  wa Umoja wa  Ulaya  utakaofanyika  wiki  ijayo nchini Cote d'voire

Na gazeti la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba nchi za Afrika zinahitaji kuwekeza kwa kiwango kikubwa  katika  miundo mbinu. Linasema bila ya  barabara na njia nzuri  za reli, bara la  Afrika  halitapata maendeleoya haraka. Bila ya miundombinu hayatapatikana maendeleo barani Afrika. Kiasi kikubwa sana cha  fedha kinahitajika kwa ajili ya kujenga miundombinu.Lakini swali ni jee  fedha hizo zitatoka wapi? Gharama kubwa za usafirishaji ni sababu mojawapo ya nchi za Afrika kushindwa kufanya biashara miongoni mwao kwa kiwango kikubwa. Pamoja na hayo linasema gazeti la Frankfurter Allgemeine, pana tatizo la nishati.  Kutokana na umeme kukatika mara kwa mara wafanyabiashara wanapoteza takriban asilimia 5 ya faida zao.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutschen Zeitungen

Mhariri: Mohammed Khelef