Afrika katika magazeti ya Ujerumani
5 Januari 2018Süddeutsche Zeitung
Waziri mkuu Desalegn amesema anakusudia kuupanuza wigo wa kidemokrasia kwa manufaa ya wananchi wote wa Ethiopia. Kwa kulitoa tangazo hilo waziri mkuu huyo amekiri kwamba wapo wafungwa wa kisiasa katika jela za nchi yake, hata hivyo idadi ya watu hao haijulikani. Kinachojulikana ni kwamba maalfu ya watu wamekamatwa tangu kuanza kufanyika maandamano ya kuipinga serikali mnamo mwaka wa 2015. Gazeti hilo la Süddeutsche pia linatilia maanani kwamba serikali ya Ethiopia inakusudia kuifunga jela ya kinyama ya Maekelawi, inayojulikana kwa kuwatesa wafungwa.
Gazeti hilo la Süddeutsche limewakariri wapinzani, wanaharakati na watetezi haki za binadamu wakisema kwamba wafungwa wa kisiasa kwenye jela hiyo wamekuwa wanateswa kwa miaka mingi kwa lengo la kuwalazimisha wakubali makosa yao. Gazeti hilo pia linaeleza kwamba waziri mkuu wa Ethiopia anataka uchunguzi ufanyike juu ya kukiukwa haki za binadamu kwenye jela hiyo.
Neues Deutschland
Gazeti la Neues Deutschland wiki hii linaripoti kwamba wapinzani wamegawanyika nchini Sudan Kusini. Limeandika kwamba hali hiyo imetokea baada ya kuvunjika kwa mkataba wa amani uliotiwa saini mnamo mwaka 2015 baina ya rais Salva Kiir na hasimu wake ambaye pia aliwahi kuwa makamu wake, Riek Machar. Gazeti hilo linasema vita nchini Sudan Kusini vimekithiri kwa ukatili na kusababisha maalfu kwa maalfu ya watu waikimbie nchi yao.
Kwa mujibu wa gazeti hilo la Neues Deutschland idadi ya watu wanaokimbia Sudan Kusini na kuingia Uganda imekuwa inaongezeka kila siku, wakimbizi kutoka Sudan Kusini wameshafikia zaidi ya milioni moja nchini Uganda. Wanapowasili nchini humo watu hao wanatoa taarifa jinsi wapiganaji wa kabila la Dinka la rais Salva Kirr wanavyowaandama watu wa makabila madogo. Gazeti hilo linafahamisha zaidi.
Makundi ya waasi nchini Sudan Kusini pia yamegawanyika katika msingi wa makabila, ikiwa pamoja na yale ya Wakaakwa na Wakuku kiasi kwamba wapiganaji wa kabila la Nuer la aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar hasimu mkuu wa rais Salvar Kiir sasa hawana tena ushawishi mkubwa nchini Sudan Kusini. Hofu imetanda nchini humo kutokana na mauaji.
Hata hivyo gazeti hilo la Neues Deutschland linasema inashangaza kutambua kwamba Umoja wa Mataifa bado haujaiona hali hiyo kuwa ni mauaji ya halaiki. Vita vya hapo awali baina ya wanasiasa wawili, Salvar Kiir na Riek Machar sasa vimegeuka kuwa vya makabila karibu yote ya Sudan Kusini.
Berliner Zeitung
Gazeti la Berliner Zeitung linatupeleka katika jiji la Cape Town linalojulikana kuwa lulu ya utalii nchini Afrika Kusini. Gazeti hilo linafahamisha kwamba ugavi wa maji umo katika hali ya dharura na linaeleza kwamba maji yamezidi kuwa haba katika jiji la Cape Town kiasi kwamba kumtakia mtu heri ya mwaka mpya ni sawa na kumdhihaki. Katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wakaazi wa jiji hilo walipewa tahadhari nyingine wakitakiwa wabane zaidi matumizi ya maji.
Gazeti hilo la Berliner limesema ikiwa mvua haitanyesha katika kipindi cha miezi minne ijayo mabomba yatakuwa yanafoka hewa ya moto tu. Gazeti hilo linaeleza kuwa ikiwa hali itafikia hatua hiyo katika jiji la Cape Town, hiyo itakuwa mara ya kwanza katika historia ya miji kwa binadamu kukaukiwa maji kabisa. Gazeti la Berliner linasema dharura inayotokana na uhaba wa maji inatishia kuathiri miundo mbinu, kilimo na afya za wakaazi wa jiji la Cape Town.
Watu wapimiwa kiasi cha maji
Berliner Zeitung linafahamisha kwamba kuanzia jumatatu iliyopita, kila mtu anaruhusiwa lita 87 tu za maji kwa siku. Wakulima wanatakiwa wapunguze matumizi kwa asilimia 45, pia ni marufuku kumwagilia maji bustani au kuosha magari. Miaka15 iliyopita, viongozi wa jiji la Cape Town walitahadharishwa juu ya hatari ya jiji lao kukumbwa na ubaba wa maji wa kiwango kikubwa kutokana na kuongezeka idadi ya wakaazi.
Katika kipindi cha miaka 25 iliyopita idadi ya watu imeongezeka kutoka milioni mbili hadi kufikia zaidi ya watu milioni nne lakini ongezeko hilo la watu halikwenda sambamba na ongezeko la ugavi wa maji. Mbali na hayo jiji la Cape Town limekumbwa na ukame usiokuwa na kifani katika kipindi cha miaka miaka mia moja iliyopita. Kiasi cha dola milioni 210 kinahitajika kwa ajili ya kujenga mtambo wa kuchuja maji ya chumvi ya kutoka baharini ili kuweza kukidhi mahitaji ya wakaazi wote.
Mwandishi:Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Gakuba, Daniel