1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz
21 Desemba 2018

Katika makala haya yaliyozingatiwa mnamo wiki hiini pamoja na mkutano wa kilele baina ya viongozi wa Afrika na Umoja wa Ulaya uliofanyika mjini Vienna, Austria na Rwanda yapiga marufuku mkorogo.

https://p.dw.com/p/3AVPM
Tanzania President John Pombe Magufuli in Dar es Salaam
Picha: DW/S. Khamis

die tageszeitung

gazeti la die tageszeitung juu ya mkutano wa kilele baina ya viongozi wa Afrika na Umoja wa Ulaya uliofanyika katika mji mkuu wa Austria, Vienna, mapema wiki hii kujadili masuala ya dijitali, maendeleo ya uchumi na mbinu za ubunifu limetilia maanani kwamba ni wakuu wa nchi wanne tu kutoka Afrika waliohudhuria mkutano huo. Gazeti hilo linaeleza: Hapo awali kansela wa Austria Sebastian Kurz ambaye kwa sasa ni rais wa zamu wa Umoja wa Ulaya alipanga kuitisha mkutano mkubwa. Lakini viongozi wengi wa Afrika hawakuuchangamkia sana mwaliko huo kama walivyoufurahia mwaliko wa China ambako wakuu wa nchi 50 wa Afrika walikwenda.

China inawekeza mabilioni ya fedha katika maendeleo ya miundombinu. Ulaya haifui dafu mbele ya China na kutokana na hali hiyo Kansela wa Austria aliamua kuitisha mkutano mdogo, uliohudhuriwa na wakuu wa nchi wanne tu kutoka Afrika. Gazeti la die tageszeitung limearifu kwamba  viongozi hao wanne walikuwa rais Paul Kagame, rais Sahle-Work Zewde wa Ethiopia, Uhuru Kenyatta wa Kenya na Abdel Fattah al -Sisi wa Misri. Akifungua mkutano huo Kansela wa Austria Sebastian Kurz alisema „Ulaya haipaswi kuliacha bara la Afrika kwa Wachina peke yao". Hata hivyo gazeti la die tageszeitung limemnukulu rais wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker akisema kwamba Umoja wa Ulaya umechelewa kuingia Afrika.

Frankfurter Allgemeine

Gazeti la Frankfurter Allgemeine linazungumzia juu ya mradi wa bwawa la kuzalishia umeme kwenye mbuga ya wanyama ya Seleous kusini-magharibi mwa Tanzania. Walinzi wa mazingira wametahadharisha kwamba wanyamapori watakuwamo hatarini kutokana na mradi huo. Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine linasema rais John Magufuli anawania kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na kwa hivyo inahitaji kuwa na nishati ya uhakika lakini gazeti hilo linasema sera zake nyingine zinatatanisha: mara  anatoa kauli dhidi ya mashoga,mara anayafungia magazeti na mara anawatia ndani wapinzani. Gazeti la Frankfurter Allgemeine  linafahamisha kwamba mradi huo wa bwawa la  kuzalishia nishati ya umeme utajengwa kwenye mto rufiji katika bonde la Stigler kwa gharama ya dola bilioni 3.6 na utarajiwa kukamilishwa mnamo mwaka 2021.

Juu ya kutekelzwa kwa mradi huo gazeti la Frankfurter allgemeine linaeleza kwamba wiki iliyopita Tanzania ilitiliana saini na Misri juu ya ujenzi wa bwana hilo. Kampuni mbili za Msiri zitashiriki katika ujenzi wa mradi huo. Gazeti linasema kwa sasa bado wako wanyama pori wengi kwenye mbuga ya Selous, lakini walinzi wa mazingira wametahdahrisha juu ya kutokea maafa ya kiikolojia kwenye sehemu hiyo.

Gazeti hilo limelikariri shirika la ulinzi wa wanyama pori duniani, WWF likisema, kujengwa kwa mradi huo wa nishati kutateketeza uhai anuai kwenye mbunga hiyo ya wanyama. Gazeti hilo pia limetahadharisha kwamba maisha ya watu laki mbili, wanaoitegemea sehemu hiyo kiuchumi yataathirika. Na kwa ajili ya ujenzi wa bwawa, miti milioni 2 na laki sita itakatwa na mbao zitakazotokana na miti hiyo zitauzwa kwa Euro milioni 53.

Berliner

Nalo gazeti la Berliner wiki hii linatupasha habari juu ya mkutano wa kwanza wa  masuala  ya kidijitali  barani Afrika. Gazeti linaarifu kwamba mkutano huo uliondaliwa na kikosi kinachoitwa Republica, ulifanyika katika mji mkuu wa Ghana, Accra ambapo wajumbe walijadili njia za kuwaingiza watu katika matumizi ya mitandao. Wajumbe hao zaidi ya 2000 kutoka duniani kote pia walijadili maadili ya matumizi ya mitandao, namna ya  kulinda taarifa za watumiaji na pia walijadili juu ya haki za raia.

Wizara ya Ujerumani inayoshughulikia ushirikiano wa kiuchumi pia ilishiriki katika kufanikisha maandalizi ya mkutano huo wa siku mbili maarufu kama tamasha la kidijitali. Wajumbe wa Afrika walisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za kuendeleza tekinolojia za nchi zao ili kueneza huduma za kidijitali.

Süddeutsche

Gazeti la Süddeutsche linatupeleka Rwanda ambako serikali imeanzisha kampeni ya kupambana na, mafuta ya kujipaka, vidonge na sabuni za kuchubua ngozi. Gazeti hilo linasema katika makala yake inayoitwa uzuri wa hatari: Rais Paul Kagame ameandika kwenye twitter kuwaambia watumiaji wa bidhaa hizo kuwa zinaleta madhara. Polisi wametwaa aina zaidi ya1000 ya mafuta na dawa zinazotumiwa kama mkorogo.

Waziri wa afya wa Rwanda Diane Gashumba amenukuliwa na gazeti la Süddeutsche akisema kwamba kupiga marufuku tu matumizi ya bidhaa hizo hakutoshelezi. Amesema watu wanapswa kuelimishwa juu ya madhara yanayosababishwa na vitu hivyo, kama vile kuchanika kwa ngozi na kupata maradhi ya saratani.

 

Mwandishi Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri:  Mohammed Khelef