1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
19 Julai 2019

Yaliyozingatiwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika ni pamoja na makubaliano yaliyofikiwa kati ya wanajeshi na wapinzani ya kuunda baraza la pamoja la kusimamia kipindi cha mpito nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/3MJWM
Sudan Khartoum | Mohamed Hamdan Dagalo und Protestführer unterschreiben Abkommen
Picha: Getty Images/AFP/H. El-Tabei

Frankfurter Allgemeine 

Baada ya miezi kadhaa ya mvutano kati ya wanajeshi na wapinzani wamefikia suluhisho la kuunda baraza litakalokuwa na wajumbe watano kutoka kila upande. Hata hivyo baraza hilo kwa pamoja litamteua mjumbe wa 11 kutoka upande wa raia. Hatua  itakayofuatia ni kutia saini tamko la katiba katika siku zizajo. Ikiwa mkataba uliotiwa saini utatekelezwa, kwa mara ya kwanza, tangu mwaka1989, watu wa Sudan watapa fursa ya kuchagua serikali ya kidemokrasia. 

Hata hivyo gazeti la Frankfurter Allgemeine linatilia maanani kwamba mkataba uliofikiwa kati ya wapinzani na wanajeshi haukuwafurahisha wote. Wawakilishi wa jeshi la ukombozi ambalo ni kundi la waasi kutoka Sudan magharibi, wanapinga makubaliano hayo. Wawakilishi hao wamesema makubaliano hayo ni kitendo cha usaliti.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linatufahamisha juu ya njia mpya inayotumiwa na wakimbizi kutoka Eritrea wanaojaribu kukimbilia barani Ulaya. Gazeti hilo linasema njia hiyo mpya ni ya hatari kubwa zaidi, na linaeleza kwamba anayetaka kukimbilia Ulaya kutoka Eritrea sasa anazunguka hadi kwenye mpaka wa Mexico na Marekani. Idadi ya watu wanaotumia njia hiyo imeongezeka mara tatu tangu mwanzoni mwa mwaka huu. Magenge yanayowasafirisha watu kinyume cha sheria ndiyo yanayonufaika. Yanawapeleka wakimbizi kutoka Afrika hadi kwenye mpaka huo. Wakimbizi wa Eritrea kwanza wanapitia Ethiopia na kuingia Uganda kabla ya kuendelea na safari ya kwenda barani Ulaya.

Gazeti hilo la die tageszeitung linatilia maanani mkataba wa amani uliotiwa saini kati ya Ethiopia na Eritrea mwaka uliopita ambao umewezesha mpaka baina ya nchi mbili hizo kufunguliwa. Tangu mwezi wa Septemba mwaka jana watu wapatao 5000 kila mwezi, wanakimbia Eritrea kwa kupitia Ethiopia hadi Uganda ili kuelekea Ulaya. Watu hao wanapatiwa pasipoti bandia nchini Uganda zinazowazesha kufika hadi Amerika ya kusini.

Handelsblatt

Gazeti la Handelsblatt limeandika juu ya janga la Ebola katika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na linaeleza kwamba vifo kutokana na maradhi ya Ebola vinaongezeka katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kwamba shirika la afya duniani WHO linahofia huenda nchi jirani nazo zikakumbwa na janga hilo. Hadi sasa wameshakufa watu wapatao 1,680 nchini Kongo kwenyewe na  haionyeshi iwapo maambukizi yatadhibitiwa. Maradhi hayo yameshafika Uganda. Gazeti la Handelsblatt limemnukulu mkurugenzi wa shirika la afya duniani WHO bwanaTedros Adhanom Ghebreyesus akitahadharisha juu ya hatari kubwa ya virusi vya Ebola kuzikumba nchi jirani za Rwanda, Burundi na Tanzania. Gazeti hilo linasema licha ya hatua za haraka zilizochukuliwa kupambana na maradhi hayo, juhudi zinatatizika kutokana na mgogoro wa mashariki mwa Jamuhuri ya Kidempkrasia ya Kongo.

Süddeutsche

Mwimbaji maarufu wa Afrika Kusini alifariki dunia Jumanne iliyopita mjini Johannesburg. Gazeti la Südeutsche linatueleza zaidi juu ya mwanaharakati huyo aliimba wimbo unaoitwa Asimbonanga, yaani “hatujamwona” akimaanisha Nelson Mandela ambao ni maarufu sana.

Johnny Clegg aliyejulikana kama Mzulu mweupe alikuwa mwanaharakati aliyepinga mfumo wa kibaguzi nchini Afrika Kusini licha ya kuwa mtoto wa wazazi weupe. Aliimba nyimbo za kuupinga utawala wa makaburu. Nyimbo zake ziliwapa watu matumaini juu ya kujenga nchi mpya ya Afrika Kusini. Clegg alizaliwa nchini Uingereza mnamo mwaka 1953 na alikwenda Afrika Kusini akiwa na umri wa miaka saba. Baadaye alishirikiana na wanamuziki weusi katika harakati za kupigania haki. Alikufa mapema wiki hii kutokana na maradhi ya saratani katika kongosho. Alikuwa na umri wa miaka 66.

Vyanzo: Deutsche Zeitungen