1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika Magazeti ya Ujerumani

Miraji Othman4 Desemba 2009

Yanavosema magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika

https://p.dw.com/p/KqZv
Kiongozi wa Libya, Muammar al-Gaddafi, bendera ya Libya, bendera ya Uswissi na Faranga ya UswissiPicha: picture-alliance/ dpa / KEYSTONE / Fotomontage: DW

Gazeti linalosomwa nchi nzima hapa Ujerumani, FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG, liliripoti juu ya shambulio kubwa la bomu lililofanywa katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, siku ya alhamisi na ambapo watu 22 waliuwawa, wakiwemo mawaziri watatu na waandishi wa habari watatu. Kati ya mawaziri waliouliwa ni waziri wa elimu ya juu, Ibrahim Hassan Addow, waziri wa elimu, Mohamed Abdullahi Waayei, na pia waziri wa afya, Bibi Qamar Aden Ali. Waziri wa nne alinusuruka, lakini alijeruhiwa vibaya sana. Shambulio hilo lilitokea wakati wa sherehe ya kutolewa hati za diploma kwa wanafunzi katika Hoteli ya Shamo ilioko katika eneo la Mogadishu ambalo bado linadhibitiwa na serekali ya mpito. Mamia ya wanafunzi na familia zao, wahadhiri na maafisa wa serekali walihudhuria sherehe hiyo ya wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Banadir. Gazeti hilo liliripoti kwamba nyuma ya shambulio hilo ni wanamgambo wa siasa kali wa al-Shabbab ambao wana maingiliano na mtandao wa kiagidi wa al-Qaida. Lakini wenyewe al-Shabbab walikana kuwa na dhamana na hujuma hiyo. Msemaji wao, Ali Mahmoud Rage, aliwaambia waandishi wa habari mjini Mogadishu kwamba wao hawahusiki na mkasa huo.

Siku mbili baada ya uamuzi wa kura ya maoni nchini Uswissi kuonesha kwamba wananchi wengi wa nchi hiyo wameunga mkono kupigwa marufuku kujengwa minara katika misikiti nchini humo, huko Libya wafanya biashara wawili wa Kiswissi walihukumiwa kwenda gerezani kwa miezi 16 na kulipa faini ya Euro 10,000. Mkasa huo uliripotiwa na gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG. Tangu mwezi July mwaka jana watu hao walikamatwa baada ya Hannibal Gaddafi, mtoto wa kiume wa kiongozi wa mapinduzi ya Libya, na mkewe kusumbuliwa na wafanya kazi wa hoteli mjini Geneva na kuwekwa kizuizini kwa muda. Rasmi ni kwamba Waswissi hao, Max Göldi na Rachid Hamdani, walihukumiwa huko Tripoli kutokana na sheria za ukaazi na udanganyifu. Wafanya biashara hao wanaweza kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.

Lakini kwenyewe huko Uswissi kukamatwa watu hao kumeonekana kama kitendo cha kulipizia kisasi kutoka utawala wa Libya. Majira ya kiangazi mwaka jana Göldi na Hamdani ilibidi wabakie gerezani kwa siku fulani, na baadae wakuu wa Libya wakawakabidhi kwa ubalozi wa Uswissi mjini Tripoli wawekwe katika kizuizi cha nyumbani. Katikati ya mwezi Septemba, kwa kisingizio cha kutaka kufanyiwa uchunguzi wa kitibabu, walipelekwa katika eneo lisilojulikana, kabla ya hapo Novemba kuweza kurejeshwa tena katika ubalozi wao.

Uhusiano baina ya Libya na Uswissi, kutokana na mkasa huu, umeingia sumu. Baada ya kukamatwa mwanawe, Gaddafi alizuwia kusafirishwa mafuta ya nchi yake hadi Uswissi na pia akaondosha akiba ya fedha za nchi yake - dola bilioni tano- kutoka nchi hiyo. Katika juhudi za kuurejesha uhusiano wa nchi mbili hizo kuwa wa kawaida na Wa-Swissi hao wawili waachwe huru, Rais Hans Rudolf Merz alikwenda Tripoli mwezi Agosti na akaomba radhi juu ya namna mtoto wa Gaddafi alivotendewa na mahakama za Uswissi. Huko alihakikishiwa kwamba Waswissi hao wawili waliokamatwa watapatiwa ruhusa ya kuondoka Libya mnamo wiki fulani. Hata hivyo, kuomba radhi hakujasaidia. Hivi sasa Wa-Libya wanadai kwamba walimuahidi Rais Merz tu kwamba wataharakisha kesi dhidi ya Waswissi hao wawili.

Baada ya kutolewa hukumu hiyo, sasa Uswissi inafikiria nini cha kufanya, japokuwa nchi hiyo haina uwezo mkubwa wa kulipiza kisasi. Mkutano wa uchumi wa dunia huko Davos umeamuwa katika kikao chake kijacho, mwisho wa Januari, kutoialika Libya. Hii ina maana kwamba mtoto wa Gaddafi na mtu ambaye anasemekana atachukuwa mahala Gaddafi, Seif-ul-Islam, hatashiriki.Yeye alitumainiwa kwamba atasaidia kuachiliwa huru Waswissi hao.

Tena gazeti la FRANKFURTER ALLGEMEINE ZEITUNG: Makala nyingine yake ilihusika na Danny Jordaan, raia wa Afrika Kusini ambaye sasa anatajika sasa kwa vile si miezi mingi kutoka sasa, kiangazi cha mwakani, nchi yake itakuwa mwenyeji wa michuano ya kambumbu kuwania Kombe la Dunia. Umarufu wa Muafrika Kusini huyo, aliye wa mchanganyiko wa rangi, umezidi tangu juzi baada ya kutangazwa nchi gani itamenyana na ipi katika michuano ya Kombe la Dunia. Kutayarisha michauno hiyo sio jambo rahisi, na mzigo huo umemuangukia Danny Jordaan, na mpaka sasa ameifanya vizuri kazi hiyo.Yeye alizaliwa Port Elizabeth mwaka 1951. Kwanza alijishughulisha na siasa katika ile jumuiya ya wanafunzi ilioanzishwa na Steve Biko, halafu na chama cha United Democratic Front na mwishowe na Chama cha African National Congress. Alikuwa mchezaji wa kriket na pia kandanda.

Mwaka 1997 aliacha ubunge na kutumia wakati wake kuliongoza shirikisho la kambumbu la Afrika Kusini, SAFA. Shirikisho hilo lilikuwa lina shida ya fedha, lakini chini ya uongozi wa Jordaan mapato yake yaliongezeka kutoka dola milioni 3.2 kwa mwaka na kufikia dola milioni 35. Licha ya nchi yake kukosa kuwa mwenyeji wa michuano ya kombe la dunia mwaka 2006, na Ujerumani kupata nafasi hiyo, hajavunjika moyo, na mwakani itakuwa ni kilele cha mafanikio yake: Amelitaka kandanda liliunganishe taifa lake la Afrika Kusini, na kulipa taifa hilo utambulisho mpya duniani. Ameweza kuiuza nje Afrika Kusini vizuri na jambo hilo amejifunza akiwa kama mwanachama wa kamati ya Shirikisho la Kabumbu Duniani, FIFA, inayohusika na masoko na televisheni.

Mwandishi:Othman Miraji /Dt Zeitungen

Mhariri:Abdul-Rahman

.