1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
13 Septemba 2019

Yaliyoandikwa katika magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika mnamo wiki hii ni pamoja na habari kuhusu kifo cha Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe na matukio ya kisiasa ya nchini Sudan.

https://p.dw.com/p/3PXK4
World News - July 29, 2018
Picha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com/M. Baloyi

Der Tagesspiegel

Der Tagesspiegel ambalo limeandika juu ya hayati Robert Mugabe aliyekuwa Rais wa Zimbabwe aliyefariki Singapore wiki hii. Gazeti hilo linasema kila mtu nchini Zimbabwe ameguswa na  kifo chake kwa namna fulani. Na linaeleza kwamba baadhi wamemsifu Mugabe kwa kusema kwamba alijitolea kwa ajili ya ukombozi wa watu wake. Wamesema Mugabe alikuwa shujaa wao. Lakini wengine wamesema kwa sauti za juu kwamba hakuwa shujaa. Hata hivyo kwa wananchi wazee nchini Zimbabwe, Mugabe alikuwa mwana-Afrika halisi, aliyejitolea kutetea haki za waafrika waliokuwa wanakandamizwa na wakoloni. 

Gazeti hilo  linasema watu wanaokumbuka udhalimu uliotendwa na wakoloni nchini  Zimbabwe kwa kauli moja wamemsifu Mugabe, na wamesema alitoa mchango mkubwa katika harakati za kuikomboa nchi yake. Lakini pia gazeti hilo linasema Mugabe aliyekuwa Rais wa Zimbabwe kwa karibu miaka 40 alikuwa dikteta aliyeuangusha uchumi wa nchi yake na kuwaletea watu wake umasikini mkubwa hata hivyo  linatilia maanani kwamba viongozi karibu wote wa Afrika wamemwita Mugabe shujaa wa ukombozi.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung wiki hii linazungumzia juu ya matukio ya nchini Sudan. Linasema nchi hiyo imeingia katika enzi mpya ya matumaini na linaeleza kuwa kuundwa kwa baraza la mpito linaloiongoza Sudan baada ya dikteta Omar al -Bashir kuondolewa madarakani ni hatua ya kimapinduzi nchini Sudan. Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo, wanawake wanne wameteuliwa katika serikali ya mpito ya Waziri mkuu Abdallah Hamdok ikiwa pamoja na waziri wa mambo ya nje Asmaa Abdallah.

Hata hivyo gazeti la die tageszeitung linasema inapasa kutilia maanani kwamba wanawake walitoa mchango mkubwa katika harakati za kuung'oa utawala wa dikteta Omar al- Bashir. Gazeti hilo linakumbusha kwamba wakati mwingine waandamanaji walishambuliwa na majeshi ya usalama na mamia waliuliwa lakini wanawake hawakutishika. Hata hivyo gazeti la die tageszeitung  linatahadharisha kwamba serikali ya kipindi cha mpito imepewa muda wa miaka mitatu ili kuleta hali bora ya maisha kwa watu wa Sudan. Gazeti la die tageszeitung limemnukuklu waziri mpya wa fedha Ibrahim Elbadawi akisema kuwa watu wa Sudan wako huru kisiasa lakini bado wanakandamizwa kiuchumi.

Neue Zürcher

Gazeti la Neue Zürcher linasema Rais Paul Kagame anajitahi kujenga wajihi mzuri wa nchi  yake, Rwanda na linaeleza kuwa Rwanda imefikia mapatano na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika, juu ya kuwachukua wakimbizi  wapatao 500 waliokuwa wamekwama nchini Libya. Wakimbizi hao kutoka Somalia, Eritrea na Sudan wanatarajiwa kupelekwa nchini Rwanda wiki ijayo. Uamuzi wa kuwachukua wakimbizi hao si jambo jipya  nchini Rwanda. 

Miaka miwili iliyopita Rais Kagame alikuwa tayari kuwachukua  wakimbizi 30,000 waliokwama nchini Libya na hasa baada ya taarifa za vyombo vya habari juu ya kukiukwa kwa haki za wakimbizi hao ambao wengine waliuzwa na kutumbukizwa kwenye utumwa. Gazeti hilo la Neue Zürcher linakumbusha kwamba nchi za Ulaya hazikuonyesha utayarifu wa kuwasaidia wakimbizi hao nchini Libya na ingawa nchi hizo zimesema zitasaidia kwa kutoa fedha lakini jambo hilo pia bado halijawa la uhakika.

Juu ya hatua ya Rwanda ya kuwachukua wakimbizi hao 500 gazeti la Neue Zürcher limemnukuu mtaalamu wa masuala ya wakimbizi Camille Le Coz aliyesema mwezi uliopita kwamba Rais Kagame analenga shabaha ya kuvuna katika diplomasia ya kimataifa. Mtaalamu huyo wa masuala ya uhamiaji ameeleza katika makala aliyoandika kwa vyombo vya habari kwamba Kagame anataka macho ya nchi za Ulaya yaelekezwe kwingineko na siyo katika kukiukwa haki za binadamu nchini mwake Rwanda.

Süddeutsche

Gazeti la Südeutsche linatupasha habari juu ya filamu kuhusu watoto waliotumiwa kama askari na kundi  la kigaidi la Lords Resistance Army LRA lililoanzishwa nchini Uganda miaka iliyopita na Joseph Kony. Gazeti hilo linasema filamu hiyo inayoitwa "Rong Elements" inaonyesha jinsi watoto hao walivyokuwa wahalifu na wahanga kwa wakati mmoja. Inaonyesha jinsi walivyobadilishwa akili hadi kufikia kiasi cha kuwaua wazazi wao. Gazeti la Südeutsche linasema filamu hiyo inabainisha historia ya watoto waliodhulumiwa utoto wao kutokana na kutumiwa kama wauaji. Nusu yao hawakurudi hai nyumbani na wale waliorejea wameathirika kiakili na kimaadili. 

Vyanzo:/Deutsche Zeitungen