1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
18 Oktoba 2019

Katika yale yaliyoandikwa na magazeti ya Ujerumani juu ya Afrika mnamo wiki hii ni pamoja na makala ya gazeti la Die Zeit juu ya tuzo ya Amani ya Nobel aliyotunukiwa Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.

https://p.dw.com/p/3RVf2
Friedensnobelpreis 2019 Äthiopien | Ministerpräsident Abiy Ahmed
Picha: picture-alliance/dpa/B. Pedersen

Die Zeit

Gazeti la Die Zeit linatilia maanani kwamba Abiy amepewa nishani hiyo baada ya muda wa miezi 18 tu tangu kuingia madarakani. Gazeti hilo linasema licha ya heshima hiyo aliyopewa na jumuiya ya kimataifa, ndani ya nchi yake anakabiliwa na shinikizo. Gazeti hilo linaeleza kwamba Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameleta mageuzi nchini Ethiopia katika kipindi cha muda mfupi. Amechukua hatua kadhaa zinazostahili kutambuliwa ndani na nje ya nchi yake.

Pamoja na hatua hizo ni kufikia mkataba wa amani na nchi jirani ya Eritrea na kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa. Watu nchini mwake waliishangilia hatua hiyo kama jinsi wajerumani walivyoshangilia kuangushwa kwa kuta la Berlin! Hata hivyo baadhi ya watu wanahoji kwamba tuzo aliyotunukiwa imetolewa mapema mno kwa mfano idadi ya watu masikini imeongezeka nchini Ethiopia licha ya hatua ndefu za maendeleo ya kiuchumi. Gazeti la Die Zeit pia linatanabahisha kwamba mageuzi yaliyoletwa na Waziri Mkuu Abiy Ahmed nchini Ethiopia yanaandamana na mivutano inayoweza kusababisha mlipuko mkubwa katika nchi hiyo yenye makabila mengi.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung linatupeleka Msumbiji ambako uchaguzi wa Rais umefanyika. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba uchaguzi huo umefanyika katika muktadha wa misukosuko lakini hatua ya maendeleo imepigwa na linaeleza kwamba kwanza inapasa kusema kwamba uchaguzi huo ulifanyika kwa njia ya uwazi kabisa, kwa mara ya kwanza katika historia ya Msumbiji.

Na pia kwa mara ya kwanza nchini humo, siyo Rais tu na Wabunge wamechaguliwa bali pia Magavana wa majimbo. Gazeti la die tageszeitung linaeleza kuwa hiyo ni ishara kwamba chama tawala cha Frelimo kimekubali utaratibu wa kuchaguliwa kwa Magavana kutokana na kura za wananchi. Hapo awali magavana wa majimbo walikuwa wanateuliwa na chama tawala tu.

Ripota wa gazeti la die tageszeitung aliyeko mjini Maputo Arimando Domingos ameripoti kwamba licha ya wasiwasi uliokuwapo juu ya kutokea ghasia na mvutano wa kisiasa, watu wapatao milioni 13  waliojiandikisha kupiga kura walimimika kwenye vituo vya kupigia kura zaidi ya 20,000. Ripota huyo amemnukulu Rais wa Msumbiji Felipe Nyusi akisema kwamba watu wa Msumbiji wamechagua njia ya amani lakini ripota huyo wa  gazeti la die tageszeitung amekumbusha kwamba watu zaidi ya 40 waliuawa wakati wa kampeni za uchaguzi.

Gazeti la die tageszeitung linasema serikali ijayo nchini Msumbiji itakabiliwa na changamoto kubwa zinazotokana na kashfa za ufisadi. Kashfa hizo zimesababisha kuondoka kwa wawekezaji vitega uchumi na wafadhili wa kimataifa. Changamoto zingine zimetokana na maafa yaliyosababishwa na hali mbaya ya hewa na kupungua kwa mapato yanayotokana na bidhaa zinazouzwa nje.

Neues Deutschland

Gazeti la Neues Deutschland linasema katika makala yake kwamba ingewezekana kuyazuia maradhi ya homa ya Ebola nchini Kongo.  Maradhi ya Ebola yaligundulika katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mnamo mwaka 1976 kwa mara ya kwanza. Jina hilo la Ebola linatokana na mto Ebola uliopo kaskazini magharibi kwa nchi hiyo. Ugonjwa huo ambao hadi sasa umeshasababisha vifo vya watu 2144 nchini Kongo unaweza kuzuiwa ikiwa chanjo na tiba zinapatikana haraka lakini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inakabiliwa na changamoto kadhaa. Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita sehemu ya mashariki ya nchi hiyo imekuwamo katika vita vya  makundi yapatayo 200. Mapigano katika sehemu hiyo pia yanaathiri juhudi za kupambana na ugonjwa wa  Ebola.

Gazeti la Neues Deutschland pia linaeleza kwamba pana hali ya kutoelewana kati ya wananchi na wahudumu wa afya na hasa wale wanaotoka nchi za nje. Katika mji wa Ariwala unaopakana na Sudan na Uganda wananchi waliwakimbia wahudumu wa afya kutoka shirika la afya duniani WHO na makundi yenye silaha pia yanavishambulia vituo vya huduma za afya. Gazeti  hilo la Neues Deutschland linasema njia ya ufanisi ya kupambana na maradhi ya Ebola ni kujenga hali ya kuamianiana kati ya wahudumu na wanaohudumiwa. Ni kutokana na uhusiano mzuri ndipo itawezekana kutoa chanjo na tiba.

Neue Zürcher

Tunakamilisha makala wiki hii kwa kauli iliyotolewa na mwanariadha maarufu duniani Eliud Kipchoge kutoka Kenya. Gazeti la Neue Zürcher limefanya mahojiano na mkimbiaji huyo wa mbio za marathon ambaye ni binadamu wa kwanza kumaliza mbio hizo chini ya muda wa saa 2.

Kipchoge ameliambia gazeti hilo kwamba hakuna kisichowezekana na kwamba lengo lake lilikuwa kuvunja rekodi ya dunia. Amesema wanaraiadha wakati wote wanalenga shabaha hiyo. Kipchoge ameeleza kwamba binadamu anayo mipaka akilini mwake anayoweza kuivuka na ndiyo sababu anafanya mazoezi yaleyale lakini fikira zake zinabadilika. Wakati wote anataka kuthibitisha kwamba hakuna kisichowezekana kwa binadamu. Kipchoge ameliambia gazeti la Neue Zürcher kwamba kukimbia mbio za marathon, na kumaliza chini ya muda wa saa mbili ni sawa na binadamu kutua mwezini kwa mara ya kwanza!

Chanzo: Deutsche Zeitungen